Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kazi 1 kati ya 4 duniani iko hatarini kubadilishwa na AI: ILO

Mwanamume anainua barua ya njano yenye maandishi 'AI' juu yake, na skrini ya kompyuta nyuma.
© Unsplash/Hitesh Choudhary Shule kote ulimwenguni zinahimizwa kubuni sera kuhusu matumizi ya programu za AI au akili bandia katika elimu.

Kazi 1 kati ya 4 duniani iko hatarini kubadilishwa na AI: ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Utafiti mpya wa pamoja uliofanywa na wa Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa  Duniani ILO, na Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti ya Poland NASK, umebaini kuwa kazi moja kati ya nne duniani iko kwenye hatari ya kuathiriwa na akili mnemba ya kizazi kipya GenAI.

Hata hivyo, ripoti ya utafiti huo inaonyesha kuwa badala ya kusababisha ukosefu mkubwa wa ajira, teknolojia hii ina uwezekano mkubwa wa kubadilisha majukumu ya kazi kuliko kuondoa kabisa nafasi za kazi.

Ripoti hiyo, iliyopewa jina Akili Mnemba ya Kizazi Kipya na Kazi: Kiashiria Kilichoboreshwa Kimataifa cha Uhusiano wa Ajira na AI, inatoa tathmini ya kina zaidi hadi sasa kuhusu jinsi GenAI inaweza kuathiri ajira kote duniani.

Kwa kuchanganya zaidi ya majukumu 30,000 ya kazi na uchambuzi wa wataalamu pamoja na tathmini ya AI, kiashiria hicho kinawapa watunga sera chombo thabiti cha kuchambua jinsi kazi katika sekta mbalimbali zinaweza kubadilika kutokana na maendeleo ya teknolojia.

Wanawake na wafanyakazi wako hatarini zaidi

Matokeo ya utafiti huo yanaonesha tofauti kubwa za kijinsia, hasa katika nchi zenye kipato cha juu.

Katika maeneo haya, asilimia 9.6 ya ajira za wanawake ziko kwenye kazi zilizo kwenye hatari kubwa zaidi ya kuondolewa kabisa na GenAI, ikilinganishwa na asilimia 3.5 kwa wanaume.

Kwa mujibu wa ripoti pia kazi za ofisini zinaonekana kuwa na kiwango kikubwa zaidi cha kuathiriwa, kwani GenAI ina uwezo wa kinadharia wa kutekeleza majukumu mengi ya kazi hizi.

Kadhalika, kazi za kiakili katika sekta za vyombo vya habari, programu za kompyuta na fedha zinaathiriwa kwa kasi kutokana na uwezo unaokua wa teknolojia hii.

Mama akiwa amembeba mtoto wake huku mwanamke akifanya kazi kwenye kompyuta mpakato nyuma ya kliniki ya afya.
GAVI Alliance/Evelyn Hockstein Mtoto mchanga anachunguzwa afya yake ya jumla iikirekodiwa na karani wa data, kama sehemu ya juhudi za kufuatilia viwango vya nimonia baada ya chanjo katika Wilaya ya Kilifi, Kenya.

Ripoti hiyo inatambulisha dhana mpya ya “viwango vya athari vinavyopanga kazi kulingana na kiwango chake cha kuathiriwa na GenAI”.

Viwango hivi vinawezesha watunga sera kutofautisha kati ya kazi zitakazobadilika na zile zilizo katika hatari ya kubadilishwa kabisa na mashine, hivyo kuwezesha hatua za kisera kuwa za kulenga zaidi.

Ubadilishaji kamili wa kazi ni mdogo, uwepo wa binadamu bado muhimu

Licha ya uwezo mkubwa wa GenAI, ripoti inaonesha kuwa matumizi yake hayawezi kubadilisha kikamilifu kazi nyingi.

Na kwamba Majukumu mengi ya kazi bado yanahitaji usimamizi, maamuzi au mawasiliano ya kibinadamu jambo linalosisitiza umuhimu wa kukuza ujuzi wa kidijitali.

Ikitoa mfano ripoti imesema, kazi zilizozoea mabadiliko ya kiteknolojia kama waandaaji wa programu zinaweza kufaidika kwa kuongeza tija, huku sekta zisizo na ujuzi wa kidijitali zikikabiliwa na changamoto zaidi.

“Swali la msingi si kama GenAI itaathiri kazi, bali ni kwa jinsi gani,” amesema Pawel Gmyrek, Mtafiti Mkuu wa ILO na mwandishi mkuu wa ripoti hiyo.

Ameongeza kuwa “Kwa kuenda zaidi ya nadharia na kutumia takwimu halisi za kazi, tumeunda njia inayoweza kuigwa na mataifa mbalimbali kutathmini hatari na kuchukua hatua stahiki.”

Sera za kidijitali zitaamua mustakabali wa ajira

Ripoti inasisitiza kuwa sera zitakazochukuliwa ndizo zitakazoamua iwapo GenAI itaimarisha ubora wa ajira au kuendeleza ukosefu wa usawa.

Ripoti imesisitiza kuwa Mazungumzo ya kijamii kati ya serikali, waajiri na vyama vya wafanyakazi yatakuwa muhimu katika kusimamia mabadiliko haya ya kidijitali.

Kiashiria hiki kimetengenezwa kama chombo cha kisera kusaidia kuweka misingi ya soko la ajira jumuishi na la haki, hasa katika sekta zilizo hatarini zaidi.

“Kiashiria hiki kinasaidia kubaini ni wapi GenAI itakuwa na athari kubwa zaidi, ili mataifa yaweze kujiandaa na kuwalinda wafanyakazi,” ameongeza Marek Troszyński, Mtaalamu Mkuu wa NASK na mwandishi mwenza wa ripoti hiyo.

Ripoti zaidi kutoka kwa ILO na NASK zinatarajiwa kufuatia, zikiangazia athari katika masoko ya kazi ya kitaifa, zikianzia Poland, na kutoa mwongozo wa kiufundi wa kusaidia sera katika nchi zinazoendelea.