Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa lishe wa KSrelief wawafikia zaidi ya wanawake na watoto 6,000 Sudan Kusini

Wanawake wakikagua msaada wa virutubisho vya lishe nchini Sudan Kusini.
© WFP/Eulalia Berlanga
Wanawake wakikagua msaada wa virutubisho vya lishe nchini Sudan Kusini.

Msaada wa lishe wa KSrelief wawafikia zaidi ya wanawake na watoto 6,000 Sudan Kusini

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limefanikiwa kuwafikia zaidi ya wanawake na watoto 6,000 walio katika mazingira hatarishi katika eneo lililoathiriwa na mafuriko la Bentiu, Jimbo la Unity, Sudan Kusini, kwa msaada wa lishe wa kuokoa maisha, kufuatia ufadhili wa ukarimu kutoka Saudi Arabia kupitia kituo cha msaada wa kibinadamu cha mfalme Salman (KSrelief. Imesema taarifa iliyotolewa leo na Wfp huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini.

Mchango wa dola za Kimarekani 400,000 uliwezesha WFP kununua na kusambaza vyakula maalum chenye lishe bora, vikiwemo Super Cereal Plus (mchanganyiko wa unga wenye virutubisho maalumu unaotumiwa kuboresha lishe) na Lipid-based Nutrient Supplements – Plumpy’Doz. Bidhaa hizi zimetengenezwa ili kuzuia utapiamlo mkali kwa watoto kuanzia umri wa miezi sita na zaidi, pamoja na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha.

Viwango vya utapiamlo Bentiu vinaendelea kuwa vya kutisha baada ya miaka ya mafuriko makubwa yaliyozamisha maeneo makubwa, kuwahamisha watu wengi na kuongeza hatari ya magonjwa ya maji, hali inayoongeza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa utapiamlo hasa kwa watoto.

“Kadri njaa na utapiamlo unavyoendelea kuzidi rasilimali zilizopo, msaada kwa programu za lishe ni muhimu. Kuwapatia watoto wadogo na akina mama lishe sahihi kwa wakati unaofaa si tu kuokoa maisha, inawapa watoto nafasi ya kukua, kujifunza, na kufikia uwezo wao kamili. Kupitia ushirikiano wetu na KSrelief haya yote yatawezekana.”

Msaada huu unakuja wakati ambapo takriban watu milioni 7.7 nchini Sudan Kusini wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula (kiwango cha IPC Awamu ya 3 au zaidi), ikiwa ni kiwango cha juu kabisa kuwahi kurekodiwa. Takribani watoto milioni 2.1 wako katika hatari ya kupata utapiamlo mwaka huu.

WFP na KSrelief wamekuwa wadau wa kimataifa kwa muongo mmoja, tangu KSrelief ilipoanzishwa mwaka 2015 mjini Riyadh. Mashirika haya mawili yamekuwa yakishirikiana nchini Sudan Kusini tangu 2018, na mchango huu wa karibuni unaimarisha dhamira yao ya pamoja ya kuboresha afya na lishe kwa watu walio katika mazingira magumu zaidi.