Janga la njaa Gaza wanawake na watoto wachanga wako hatarini
Janga la njaa Gaza wanawake na watoto wachanga wako hatarini
“Kuna upungufu mkubwa wa chakula na dawa muhimu, hasa wakati huu wa migogoro,” amesema daktari mmoja katika Hospitali ya Al-Awda, iliyoko katika mkoa wa kati wa Deir Al-Balah,huko Gaza Palestina. “Imeleta athari kubwa kwa wanawake wajawazito, akina mama wanaonyonyesha na watoto kwa ujumla.”
Daktari huyo amezungumza na shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi, UNFPA baada ya zaidi ya miezi miwili ya kuzuiliwa kwa msaada wa kibinadamu na Israel huko Gaza, ambapo usambazaji wote ikiwemo chakula, dawa, makazi na mafuta ulikatizwa.
“Tunaona ongezeko kubwa la watoto wachanga wanaozaliwa na uzito mdogo kutokana na utapiamlo wa mama na upungufu wa damu wakati wa ujauzito,” anaendelea kusema daktari huyo, ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa sababu za usalama.
Aya Hassan, anayeishi kwa sasa katika kambi ya wakimbizi ya Deir Al-Balah katikati mwa Gaza anasema, “tunaishi kwa chakula kinachotolewa na majiko ya jamii. Kliniki zinatoa virutubisho kwa wanawake wajawazito, na ninahudhuria kliniki kila siku kwa sababu nina hofu ya kupata upungufu wa vitamini. Hali ni ngumu sana.”
Kwa kuwa hakuna upatikanaji wa maji safi wala vifaa vya usafi, magonjwa ya kuambukiza na magonjwa ya zinaa pia yameripotiwa kuongezeka.
“Ukosefu wa bidhaa za usafi ni mojawapo ya vichochezi vikuu vya hali hii,” ameongeza daktari huyo. “Pia tunakabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa, ikiwa ni pamoja na ukosefu kamili wa dawa za afya ya uzazi, hali ambayo imesababisha ongezeko la mimba kuharibika na kutoka.”
Mfumo wa afya umedhoofika
Mashambulizi dhidi ya hospitali, vituo vya afya na wafanyakazi wa afya yameuacha mfumo wa afya ukiwa katika hali mbaya kabisa. Hospitali ya Nasser kusini mwa Gaza, mojawapo ya hospitali nane pekee zinazofanya kazi kwa kiasi, ilishambuliwa kwa bomu na jeshi la Israel tarehe 13 Mei, ikiwa ni mara ya nne kushambuliwa tangu Oktoba 2023. Muda wa chini ya saa 24 baadaye, Hospitali ya Ulaya huko Khan Younis pia ilishambuliwa.
Upatikanaji wa huduma muhimu umekua mgumu sana huku vifaa vya kujifungua salama na vya huduma kwa watoto wachanga vikiwa vimekwama mpakani. Katika hali hii ya kutisha, karibu wanawake wajawazito 11,000 tayari wameripotiwa kuwa katika hatari ya njaa kali, na karibu wanawake wajawazito na wanaonyonyesha 17,000 watahitaji matibabu ya dharura dhidi ya utapiamlo mkali katika miezi ijayo. Kwa wengi, athari ni mbaya sana.
“Nilitibu mwanamke aliyekuwa na matatizo ya kupata ujauzito kwa karibu miaka saba,” anaendelea kusema daktari wa Hospitali ya Al-Awda. “Hatimaye alipata ujauzito wakati wa vita, lakini kutokana na athari za migogoro, ukosefu wa lishe bora, na mshtuko wa mabomu alipolazimika kukimbia, alijifungua mapema kabla ya wakati na kumpoteza mtoto wake.”
Janga la kibinadamu linazidi kuongezeka
UNFPA ina malori zaidi ya 190 yenye misaada inayohitajika haraka Gaza, lakini yamezuiliwa kuingia mipakani. Hii inajumuisha vitengo vya uzazivinavyohamahama, mashine za mionzi, na mashine za kuhifadhi watoto njiti au incubator zinazobebeka ambazo ni muhimu kwa watoto wachanga waliozaliwa kabla ya wakati, vifaa vya usafi, vifaa vya makazi na dawa za afya ya uzazi, ikiwemo zile za kushughulikia dharura wakati wa uzazi.
Katika kituo cha uzazi cha Al-Awda, Wafa mwenye umri wa miaka 38 ameambia UNFPA, “Huyu ni mtoto wangu wa saba. Nilipata ujauzito mwezi Machi 2024, wakati wa vita. Mwanzo wa ujauzito wangu ulikuwa mgumu sana kutokana na utapiamlo.”
Akiwa amefukuzwa na familia yake, anaeleza, “nililazimika kutegemea maji ya mishipa (IV fluids) katika Hospitali ya Al-Awda na nilianza kupata uchungu wa kujifungua kabla ya wakati mapema mwezi wa nane. Hata hivyo, timu ya matibabu walinifuatilia kwa karibu na kunipa huduma endelevu, na hatimaye nilijifungua hospitalini.”
Katika miezi miwili ya mwanzo ya usitishaji mapigano, UNFPA inakadiria kuwafikia wanawake na wasichana 146,000 kwa huduma za afya ya uzazi na watu zaidi ya 100,000 kwa huduma za ulinzi kupitia vituo vya afya na kliniki tembezi.
“Tumaini letu kuu ni kwamba vita hii iishe.” daktari wa Hospitali ya Al-Awda anasema.
Mwaka 2025, UNFPA inahitaji dola milioni 99 kukabiliana na mahitaji yanayoendelea na yanayoibuka Palestina, lakini kufikia mwezi Aprili, ni dola milioni 12.5 pekee zilizopokelewa.