Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia wauawa kwenye shambulio la ndege zisizo na rubaniUkraine: UN

Waokoaji wakisaka manusura katika jengo lililosambaratishwa Kyiv Ukraine
© Human Rights Monitoring Mission in Ukraine/Anastasiia Honcharuk
Waokoaji wakisaka manusura katika jengo lililosambaratishwa Kyiv Ukraine

Raia wauawa kwenye shambulio la ndege zisizo na rubaniUkraine: UN

Amani na Usalama

Shambulio la Ndege zisizo na rubani au droni lililotokea mashariki mwa Ukraine leo linaweza kuwa baya zaidi katika wiki za hivi karibuni, kwa mujibu wa Tume ya Ufuatiliaji wa Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Ukraine HRMMU.

Kwa mujibu wa mamlaka za eneo hilo, watu wasiopungua tisa wameuawa na saba kujeruhiwa wakati Ndege isiyo na rubani ya Urusi ilipolenga basi dogo karibu na mji wa Bilopillia, katika mkoa wa Sumy.
Wachunguzi wa HRMMU wapo katika mchakato wa kukusanya taarifa zaidi kuhusu mazingira ya shambulio hilo na wahanga wake.

Walengwa ni raia waliokuwa wakihamishwa

Ripoti za awali zinaonyesha kuwa basi hilo lilikuwa linabeba raia waliokuwa wakihamishwa kutoka eneo lililo karibu na uwanja wa mapigano, wengi wao wakiwa ni wanawake.
Shambulio baya zaidi la hivi karibuni
“Kwa raia tisa kuripotiwa kuuawa, hili linaweza kuwa shambulio baya zaidi katika wiki za hivi karibuni,” amesema Danielle Bell, Mkuu wa HRMMU.
“Hili ni ukumbusho wa kusikitisha kuwa raia bado wanaendelea kuuawa na kujeruhiwa kila siku kote nchini Ukraine.”
Iwapo idadi hiyo ya vifo itathibitishwa, basi litakuwa shambulio baya zaidi tangu tarehe 24 Aprili, ambapo raia wasiopungua 11 waliuawa na wengine 81 kujeruhiwa katika mji mkuu, Kyiv.
HRMMU imeeleza kuwa ingawa idadi ya vifo vya raia mwezi Mei imekuwa chini kidogo ukilinganisha na Aprili, bado inaendelea kurekodi vifo na majeruhi kila siku, hususan katika maeneo ya uwanja wa mapigano.