Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maendeleo ya kidijitali yanawaacha nyuma wanawake: Guterres

Mchoro wa kiisometriki wa mandhari ya teknolojia ya wakati ujao inayoangazia seva, kompyuta za mkononi, mikono ya roboti, na wafanyabiashara katika mazingira ya kidijitali.
ITU Graphic Uchambuzi wa hivi punde wa kimataifa wa ITU unaonesha bei za huduma za mawasiliano ya simu zinaendelea kupungua lakini haziendani na viwango vinavyoongezeka kwa kasi vya bei ya intaneti.

Maendeleo ya kidijitali yanawaacha nyuma wanawake: Guterres

Utamaduni na Elimu

Leo tarehe 17 Mei 2025, Siku ya Kimataifa ya Mawasiliano na Teknolojia ya habari, ulimwengu unaadhimisha miaka 160 tangu kuanzishwa kwa Muungano wa Kimataifa wa MawasilianoITU, kwa kuangazia mchango wa teknolojia katika kubadilisha maisha ya binadamu kuanzia kwenye telegrafu hadi redio, kutoka mtandao wa intaneti hadi akili mnemba AI.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, katika ujumbe wake wa siku hii ametoa wito wa kuhakikisha mabadiliko ya kidijitali yanakuwa ya usawa wa kijinsia.

Ametahadharisha kuwa licha ya maendeleo makubwa kiteknolojia, faida zake bado zinapatikana kwa njia isiyo na usawa.

“Upendeleo wa kihisia unaosababisha ubaguzi katika algorithmi unadumaza usawa. Ukatili na udhalilishaji wa mtandaoni unanyamazisha sauti za wanawake na kuwafanya wajitenge na mifumo ya kidijitali,” amesema Katibu Mkuu.

Wasichana watatu wa Kiasia wameketi kwenye viti vya waridi katika chumba cha kisasa, kila mmoja akiangalia kifaa cha mkononi mikononi mwake.
ITU/R. Farrell Umoja wa Mataifa umesema , ulimwenguni asilimia 17 zaidi ya wanaume na vijana wanapata huduma ya ntandao ilikinganishwa na wanawake na wasichana.

Idadi ndogo ya wanawake na wasaichana katika STEM

Aidha Guterres ameelezea wasiwasi kuhusu uwakilishi mdogo wa wanawake na wasichana katika taaluma za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) maeneo ambayo yanaathiri moja kwa moja mwelekeo wa maendeleo ya baadaye.

“Uonevu unatuumiza sote. Hatupaswi kuukubali mustakabali wa kidijitali unaowaacha wanawake nyuma. Tunapaswa kuwekeza katika stadi za kidijitali kwa wote, kutumia teknolojia kuboresha maisha ya wanawake, kuondoa vizuizi vinavyowazuia kushiriki kikamilifu na kuongoza katika sekta ya teknolojia, na kuendelea kupambana na ukatili wa kijinsia mtandaoni na nje ya mtandao,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, mikataba mipya kama "Mkataba wa Zama Zijazo" na "Mkataba wa kimataifa wa dijitali" ni fursa muhimu ya kuunganisha nguvu duniani kote ili kufunga pengo la kidijitali na kulinda haki za wanawake katika majukwaa ya kidijitali.

Amehitimisha ujumbe wake kwa kusisitiza kuwa“Wakati teknolojia inapotumika kwa manufaa ya wote, kila mtu hunufaika."