Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mali: Mkuu wa OHCHR atoa wito wa kufutwa amri ya kimila inayopiga marufuku vyama vya kisiasa

Mwanajeshi akipiga doria katika mji wa Ménaka kaskazini mwa Mali.
© MINUSMA/Harandane Dicko
Mwanajeshi akipiga doria katika mji wa Ménaka kaskazini mwa Mali.

Mali: Mkuu wa OHCHR atoa wito wa kufutwa amri ya kimila inayopiga marufuku vyama vya kisiasa

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk ametoa wito kwa serikali ya Mali kurekebishe amri inayovunja vyama vya siasa na irejeshe kikamilifu haki za kisiasa katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Tarehe 13 Mei, Rais wa mpito wa Mali Assimi Goïta “alitia saini amri inayopiga marufuku vyama vyote vya kisiasa na mashirika ya kisiasa na ametangaza sheria inayofuta sheria zilizokuwepo hapo awali ambazo zilikuwa zinalinda na kusimamia vyama vya siasa.

Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Bwana amesema Volker Türk  amesema “Rais wa mpito lazima aifute amri hii ya kiimla. Masharti yoyote yanayozuia ushiriki wa kisiasa yanapaswa kuendana na wajibu wa Mali chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu,”.

Kulingana na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa sheria mpya zinazozuia ushiriki wa kisiasa nchini Mali zinaleta hatari ya kuzima sauti za upinzani na zinaweza kuchochea matatizo makubwa zaidi ya haki za binadamu.

Takriban wanasiasa watatu wa upinzani wamekamatwa baada ya maandamano dhidi ya mpango wa kufuta vyama vya siasa, na hadi sasa hawajulikani walipo.

Kutoa ratiba ya uchaguzi bila kuchelewa

“Hawa ni waathirika wa hivi karibuni katika mfululizo wa matukio ya kutoweshwa kwa nguvu ambayo yamekuwa yakiripotiwa tangu mwaka 2021,” Türk amesema, huku akieleza matumaini kuwa mamlaka itawaachilia wafungwa wa kisiasa na irejeshe kikamilifu “haki za kisiasa nchini humo.” Ameongeza kuwa uhuru wa msingi unapaswa kuhakikishwa.

Kamishna Mkuu pia amehimiza mamlaka ya mpito ya Mali, ambayo ipo madarakani tangu mwaka 2020, isiongeze kipindi cha mpito tena na itangaze ratiba ya uchaguzi bila kuchelewa.

Pia amekumbusha agizo la Rais wa Mpito kwa Baraza la Mawaziri mnamo Novemba 2024 la “kuweka mazingira muhimu ya kuandaa uchaguzi huru na wa amani utakaohitimisha kipindi cha mpito.”

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, “mikwamo ya karibuni katika nyanja ya haki za binadamu inajitokeza wakati ambapo hali ya usalama bado ni tete na inaathiri watu kote Mali, hasa baada ya kuondoka kwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani nchini humo  MINUSMA, tarehe 31 Desemba 2023.”

Ongezeko la asilimia 120 la Ukiukaji wa haki kati ya 2023 na 2024

Vyanzo vya kuaminika vilivyonukuliwa na Umoja wa Mataifa vinaonesha kuwa matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu yameongezeka kwa takribani asilimia 120 kati ya mwaka 2023 na mwaka uliopita.

Makundi yenye silaha, yakiwemo yale ya Dola ya Kiislamu IS, yanaendelea kuua na kuwateka raia. Pia yanaendelea kuwanyanyasa wanawake na wasichana kwa ukatili wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na ubakaji na ndoa zashuruti.

Wakati huo huo, ripoti zingine zinaonesha kuwa Jeshi la Mali, likishirikiana na wanajeshi wa kigeni kutoka Kundi la Wagner la Urusi, limewaua raia kadhaa mwezi uliopita. Waathirika wanaripotiwa kuuawa kwa kunyongwa baada ya kukamatwa huko Sebagougou, kusini-magharibi mwa mkoa wa Kayes.

Türk  amesema kuwa “Uchunguzi kadhaa uliotangazwa na mamlaka ya Mali kuhusu mashambulizi haya na mauaji unapaswa kufanyika haraka iwezekanavyo, na waliohusika wawajibishwe kupitia kesi zinazoendana na wajibu wa Mali chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu, ili kuhakikisha haki ya waathirika ya kupata ukweli, haki na fidia”.