Kenya, Afghanistan, Ukraine baadhi ya nchi ambako mikakati sahihi ya kilimo imeepusha njaa - FAO
Kenya, Afghanistan, Ukraine baadhi ya nchi ambako mikakati sahihi ya kilimo imeepusha njaa - FAO
Ukosefu wa uhakika wa kupata chakula na utapiamlo kwa watoto uliongezeka kwa mwaka wa sita mfululizo mwaka 2024, na kuwatumbukiza mamilioni ya watu karibu na baa la njaa, huku wengine wakiepuka kutokana na misaada ya kimkakati. Imesema Ripoti ya Kimataifa kuhusu Janga la Chakula (GRFC) iliyotolewa leo Marekani, Italia na Uswisina shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO.
Ripoti inasema kuwa mwaka 2024, zaidi ya watu milioni 295 katika nchi na maeneo 53 walikumbwa na viwango vya juu vya njaa – idadi hiyo ikiwa ni ongezeko la watu milioni 13.7 ikilinganishwa na mwaka 2023.
Rein Paulsen, Mkurugenzi wa FAO Idara ya Dharura na Mnepo anasema hii ni mara ya tano mfululizo ambapo idadi hii imebaki juu ya asilimia 20
Vichochezi vikuu vitatu
Sababu kuu tatu zinazochochea ongezeko hili ni zifuatazo: Kwanza kabisa, migogoro na ukosefu wa usalama ndiyo chanzo kikuu cha ukosefu mkubwa wa chakula. Hali mbaya za hewa kupindukia, ni sababu ya pili muhimu. Na, changamoto za kiuchumi ni sababu ya tatu muhimu zaidi. Na uchambuzi unaonesha kwamba, katika mazingira mengi ya migogoro, sababu hizi tatu mara nyingi huingiliana.
Ripoti hiyo ya kurasa 254, inaeleza kuwa baa la njaa limethibitishwa nchini Sudan, huku maeneo mengine yaliyo katika hatari zaidi ambako watu wanakumbwa na viwango vya juu vya ukosefu wa uhakika wa chakula kuwa ni pamoja na Ukanda wa Gaza, Sudan Kusini, Haiti, na Mali.
Kufurushwa nako kumeleta hali tete ya chakula
Ripoti hiyo pia inaangazia ongezeko kubwa la njaa linalochochewa na watu kufurushwa makwao, ambapo takriban watu milioni 95 waliolazimika kuhama – wakiwemo wakimbizi wa ndani, wasaka hifadhi, na wakimbizi – wanaishi katika nchi zinazokabiliwa na hali tete ya chakula, kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, Colombia, Sudan, na Syria, kati ya jumla ya watu milioni 128 waliolazimika kuhama duniani kote.
Misaada ya kimkakati imenusuru mamilioni
Licha ya taswira ya kukatisha tamaa, bado kuna matumaini yaliyoonekana mwaka 2024 ambapo FAO inasisitiza uwekezaji katika mifumo ya uzalishaji wa chakula katika eneo husika.
Bwana Paulsen anafafanua zaidi akisema, “tukilinganisha hali ya mwaka huu na mwaka uliopita, tunaona kuwa katika nchi 19, hali ilizorota zaidi kwa upande wa ukosefu mkali wa chakula, lakini katika nchi 15, hali iliimarika. Baadhi ya nchi hizo ni Afghanistan, Ukraine, Guatemala, Kenya.”
Amesema hizi zote ni nchi ambazo, kwa sababu ya misaada ya kibinadamu, na kwa sababu ya aina sahihi za msaada – ikiwa ni pamoja na mikakati ya dharura ya usaidizi kwenye kilimo, – kuna mamilioni ya watu wachache wanaohitaji msaada mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana.