Kufuatia taarifa za kutoswa baharini wakimbizi wa Rohingya Mtaalamu wa UN aanzisha uchunguzi
Kufuatia taarifa za kutoswa baharini wakimbizi wa Rohingya Mtaalamu wa UN aanzisha uchunguzi
Mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameanzisha uchunguzi wa dharura kuhusu kile alichokiita “matendo yasiyovumilika na yasiyokubalika” kufuatia ripoti zinazodai kuwa wanajeshi wa wanamaji wa India waliwalazimisha wakimbizi wa Rohingya kuruka kutoka kwenye meli hadi baharini wiki iliyopita. Ripoti hizo zinadai kuwa wakimbizi hao walitakiwa kuogelea hadi kisiwa kilicho ndani ya ardhi ya Myanmar baada ya kusafirishwa kutoka Delhi wakiwa wamefungwa macho na kuwekwa kwenye meli ya kijeshi ya India.
Katika taarifa yake iliyotolewa leo mtaalam huyo wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Myanmar Tom Andrews, amelaani vikali madai hayo, akiyataja kuwa ni ya “kushtua na ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa.
“Wazo la kuwa wakimbizi wa Rohingya wametoswawq baharini kutoka kwenye meli za kijeshi ni la kusikitisha mno,” amesema Andrews.
Ametoa wito kwa serikali ya India kutoa taarifa kamili kuhusu kilichotokea na mahali walipo wakimbizi hao kwa sasa.
Ukiukwaji wa sheria ya kimataifa kuhusu ulinzi wa wakimbizi
Andrews ameeleza kuwa matendo hayo yanakiuka kanuni ya msingi ya kimataifa ya kutowarudisha watu mahali wanapokumbana na mateso au hatari ya maisha yao.
“Vitendo vya kikatili kama hivi ni fedheha kwa utu wa binadamu,” amesema. Watu wa Rohingya, ambao ni wachache wa Kiislamu kutoka Myanmar, wameendelea kukumbwa na ukatili, ikiwemo mashambulizi ya kijeshi, kuhamishwa kwa lazima, na kunyimwa uraia.
India yatuhumiwa kuongeza operesheni za kuwafukuza wakimbizi
Kwa mujibu wa mtaalam huyo Ripoti zaidi zinaeleza kuwa mamlaka za India zimeongeza msako dhidi ya jamii ya Rohingya.
Mbali na tukio la Andaman, wakimbizi wengine wapatao 100 waliripotiwa kuhamishwa kutoka kituo cha mahabusu jimboni Assam na kupelekwa mpakani na Bangladesh na mahali walipo kwa sasa bado hakufahamiki.
Tukio hili linajiri baada ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa kutumwa kwa Serikali ya India mwezi Machi 2025 ukitaka kukomeshwa kwa kuwekwa kizuizini kiholela na kurejeshwa kwa wakimbizi wa Myanmar.
Wito wa hatua za haraka na ulinzi kwa wakimbizi
Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza tena wito kwa India kutekeleza wajibu wake wa kimataifa na kusitisha mara moja urejeshaji wowote wa Rohingya kwenda Myanmar.
“Serikali ya India lazima ipinge vikali matendo haya dhidi ya wakimbizi wa Rohingya,” amesema Andrews, akiongeza kuwa wahusika wote lazima wawajibishwe.
Tukio hili limezua wasiwasi mkubwa duniani huku mashirika ya kibinadamu yakionya kuhusu kuzorota kwa hali ya maisha kwa wakimbizi wa Rohingya katika maeneo mbalimbali ya Asia.