Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya Kituo cha Nyuklia cha Zaporizhzhya nchini Ukraine ni ya mashaka - IAEA

Kituo kidogo kilichoharibika huko Enerhodar, Ukraine, kilitembelewa na wataalamu wa IAEA mnamo Juni 20, 2024.
© IAEA Kituo kidogo kilicho karibu na Kiwanda cha Nguvu za Nyuklia cha Zaporizhzhya kimeharibiwa huku mzozo wa Ukraine ukiendelea.

Hali ya Kituo cha Nyuklia cha Zaporizhzhya nchini Ukraine ni ya mashaka - IAEA

Amani na Usalama

Kwa zaidi ya wiki moja, Kituo cha Nyuklia cha Zaporizhzhya (ZNPP) cha Ukraine kimekuwa kikitegemea njia moja tu ya umeme ili kupata umeme unaohitajika kwa ajili ya kazi muhimu za usalama wa nyuklia, huku mzozo wa kijeshi ukizuia juhudi za kurejesha njia ya akiba, amesema leo Mei 15 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA), Rafael Mariano Grossi.

Njia ya pekee ya akiba yenye volti 330 kilovolt (kV) ya ZNPP ilikatika tarehe 7 Mei, na kuacha kituo hicho kikitegemea kabisa njia pekee inayofanya kazi ya 750 kV. IAEA iliarifiwa kuwa uharibifu huo umetokea katika eneo linalodhibitiwa na Ukraine mbali kidogo na kituo hicho, na kwamba waendeshaji wa gridi ya umeme ya Ukraine kwa sasa hawawezi kufanya matengenezo kutokana na hali ya kijeshi iliyo hai katika eneo hilo.

Mitambo yote sita ya ZNPP imezimwa tangu katikati ya mwaka 2022, lakini bado inahitaji umeme kutoka nje kwa ajili ya kupooza mafuta ya nyuklia na kupunguza hatari ya ajali. Kabla ya mzozo, kituo hicho kilikuwa na njia kumi za umeme, hali ambayo ilihakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kutoka nje.

“Katika kipindi chote cha vita, upatikanaji wa umeme kutoka nje umekuwa udhaifu mkubwa wa usalama wa nyuklia katika Kituo cha Nyuklia cha Zaporizhzhya. Kwa bahati mbaya, hali hii haijaimarika. Wataalamu wetu walioko eneo hilo wataendelea kufuatilia kwa karibu hali hiyo, na tutaendelea kuuarifu ulimwengu kuhusu usalama wa nyuklia katika kituo hicho, ambacho bado kiko katika hali ya hatari,” anasema Mkurugenzi Mkuu Grossi.

Timu ya IAEA imeendelea kusikia shughuli za kijeshi kila siku katika wiki iliyopita, ikiwa ni pamoja na milipuko kwa umbali tofauti na ZNPP, na mapema asubuhi ya Jumanne, timu hiyo pia ilisikia milio ya risasi na sauti inayodhaniwa kuwa ni ya ndege isizo na rubani (droni).

IAEA inaendelea kusaidia

Kama sehemu ya shughuli zao za kila siku za kufuatilia na kutathmini usalama wa nyuklia, timu ya IAEA ilikagua jenereta sita kati ya 20 za dharura zinazotumia dizeli (EDGs). Jenereta hizi hutoa msaada wa dharura endapo kituo cha nyuklia kitapoteza kabisa upatikanaji wa umeme kutoka nje, jambo ambalo limewahi kutokea mara nane katika ZNPP wakati wa mzozo.

Mashaka

Timu hiyo iliona skrubu iliyolegea kwenye jenereta mbili, na iliona viashiria kuwa huenda kulikuwa na shughuli fulani zilizofanyika hivi karibuni kwenye mojawapo ya jenereta hizo. ZNPP ilieleza kuwa hakuna matengenezo yaliyofanywa hivi karibuni, lakini ilikubali kuwa skrubu hizo hazikupaswa kulegea, moja ikiwa imesababishwa na mtetemo. Timu ya IAEA inapanga kushuhudia majaribio ya jenereta moja kati ya hizi katika siku chache zijazo.

Mitambo inavyotumia dizeli ambayo ilikuwa ikitoa huduma ya joto kwa ZNPP na mji wa karibu wa Enerhodar wakati wa miezi ya baridi sasa vimezimwa ili kuruhusu majaribio ya mfumo wa maji wa gridi, timu hiyo pia iliripoti.

Mkurugenzi Mkuu Grossi amesema anaendelea kujadiliana kwa kina na pande zote mbili ili kupanga mzunguko ujao wa wataalamu wa IAEA katika kituo hicho, jambo ambalo tayari limechelewa kutokana na hali tata na ngumu ya eneo hilo ambalo liko kwenye mstari wa mbele wa mzozo.

Shughuli za matengenezo na kuongeza mafuta zimeendelea katika vituo vitatu vya nyuklia vinavyoendelea kufanya kazi nchini Ukraine – Khmelnytskyy, Rivne na South Ukraine. Mitambo mmoja katika kituo cha Rivne umeanza tena kuzalisha umeme kwa kiwango cha juu wiki hii, na kufanya jumla ya mitambo sita kuwa inafanya kazi kwa sasa nchini Ukraine.

Katika vituo hivyo vitatu na eneo la Chornobyl, timu za IAEA ziliripoti uwepo wa ving’ora vya tahadhari ya mashambulizi ya anga mara kadhaa katika wiki iliyopita. Timu za Shirika zilizoko Rivne, South Ukraine na Chornobyl zilibadilishana nafasi wiki hii, na wafanyakazi kutoka makao makuu ya Vienna kuchukua nafasi ya wenzao waliokuwa kazini.