Sudan: Wataalamu huru walaani mashambulizi ya kikatili dhidi ya wanawake na wasichana
Sudan: Wataalamu huru walaani mashambulizi ya kikatili dhidi ya wanawake na wasichana
Wataalamu huru wa haki za binadamu leo Mei 14 wamekemea vikali ukiukwaji mkubwa na wa kimfumo dhidi ya wanawake na wasichana nchini Sudan, ukiwemo ukatili wa kingono unaohusiana na vita, utekaji nyara, na mauaji, ambayo mengi yameripotiwa kufanywa na kundi la kijeshi la Rapid Support Forces (RSF).
“Tumeshtushwa sana na ripoti za kusikitisha za ukatili wa kingono, utekaji nyara, na mauaji yanayolenga wanawake na watoto, hata katika kambi za wakimbizi wa ndani, ambazo zinaonesha kampeni ya kikatili na ya kimfumo dhidi ya walioko katika hatari kubwa zaidi katika jamii ya Sudan,” wamesema wataalamu hao jijini Geneva, Uswisi.
Wakiangazia kuwa mgogoro huo ambao umeingia mwaka wa tatu, wataalamu hao wa haki za binadamu wameeleza kuwa athari kwa raia zinaendelea kuwa mbaya zaidi, huku wanawake na wasichana wakikabiliwa na hatari kubwa ya kubakwa kwa magenge, utumwa wa kingono, usafirishaji haramu wa binadamu, na ndoa za kulazimishwa, hasa katika maeneo ya Al Gezira, Sinnar, Darfur, na Kordofan Kusini. Katika baadhi ya mashambulizi, familia nzima zinaripotiwa kutawanywa, wanawake kubakwa mbele ya ndugu zao au kutekwa kwa ukatili wa muda mrefu wa kingono. “Ukatili wa kingono unaendelea kutumika kimfumo kama silaha ya vita nchini Sudan,” wameonya.
Wengine wamejiua
Wamesema katika vijiji kama vile Al Seriha, Azrag, Ruffa, na Abu Gelfa, wanawake wamejiua baada ya kushambuliwa kwa ukatili, na wakabainisha kuwa manusura wanazidi kufikiria hadharani kujiua kama njia ya kukimbia madhila ya vita.
“Taarifa hizi za kutisha zinaonesha ukubwa wa tatizo la afya ya akili miongoni mwa wanawake na wasichana, ukosefu wa msaada na huduma, pamoja na uhuru wa waovu kufanya vitendo vyao bila kuadhibiwa, hasa katika maeneo ambayo mifumo ya msaada imeporomoka kabisa,” wamesema.
“Nyuma ya kila taarifa kuna mwanamke au msichana ambaye maisha yake yameharibika kabisa,” wataalamu wameongeza. “Mgogoro huu unahitaji si tu kuangaliwa, bali hatua za haraka ili kukomesha ukatili huu kwa misingi ya haki na utu.”
Wameeleza kuwa tangu mwaka 2025, matukio zaidi ya 330 ya ukatili wa kingono unaohusiana na vita yameripotiwa, ingawa idadi halisi inaaminika kuwa kubwa zaidi kutokana na watu kushindwa kuripoti. Manusura, wakiwemo watoto, wanakumbana na vikwazo vikubwa kupata huduma za afya au msaada wa kisaikolojia. Katika maeneo kama El Fasher, mfumo wa afya umeporomoka, na mashambulizi katika kambi za wakimbizi yamewafanya wanawake kujifungua katika mazingira yasiyo salama na yasiyo safi. Vifo vya wanawake wajawazito vimeongezeka kwa kasi, huku huduma za dharura za uzazi zikiwa karibu kutokuwepo kabisa.
Utekaji
Utekaji nyara wa wanawake na wasichana umeongezeka kwa kasi katika maeneo yanayodhibitiwa na RSF, wengi wakiaminika kutekwa kwa ajili ya utumwa wa kingono na unyonyaji, walisema wataalamu. Waathiriwa wanachukuliwa kutoka kwenye kambi za wakimbizi, masokoni, na makazi ya muda, wakati mfumo wa ulinzi ukivunjika. Hali katika maeneo haya imezidi kuwa mbaya, na kuwaweka wanawake na wasichana katika hatari kubwa zaidi ya ukatili wa kingono.
Watetezi
Wataalamu pia wameelezea wasiwasi wao kuhusu mashambulizi dhidi ya watetezi wa haki za wanawake na wafanyakazi wa mstari wa mbele, ambao wameripotiwa kubakwa, kuuawa, au kunyanyaswa kwa kuwasaidia manusura au kwa kuandika ripoti za ukiukaji wa haki.
“Ukiukaji huu unaleta madhara makubwa kwa watu binafsi na jamii, huku ukibomoa mifumo iliyosalia ya ulinzi na kuharibu matumaini ya kupona na haki,” wamesema na kuongeza kwamba, “kiwango kikubwa cha ukatili ambacho wanawake na wasichana wanaendelea kukumbana nacho ni ushahidi wa kusikitisha wa kuanguka kwa ulinzi wa wanawake na wasichana wakati wa migogoro, na kuzoeleka kwa ukatili huo. Jumuiya ya kimataifa lazima iingilie kati kwa haraka ili kuzuia hali kuzidi kuwa mbaya.”
Aidha wataalamu hao wamesema wamewasiliana na Serikali kuhusu masuala haya.