Marekani: Kamishna wa haki za binadamu UN aeleza wasiwasi uhamishaji watu
Uhamishaji wa idadi kubwa ya watu wasio raia wa Marekani katika miezi ya hivi karibuni, hasa kwa kuwapeleka katika nchi ambazo si za asili yao, umeibua wasiwasi mkubwa kuhusu haki za binadamu, amesema Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, leo Jumanne Mei 13 mjini Geneva, Uswisi.
Kulingana na takwimu rasmi za Marekani, kati ya tarehe 20 Januari na 29 Aprili 2025, watu 142,000 walifukuzwa kutoka Marekani. Kwa namna ya kipekee, hatima na mahali walipo takribani raia 245 wa Venezuela na takriban raia 30 wa El Salvador waliorejeshwa nchini El Salvador bado haijulikani.
Wengi wao walifukuzwa chini ya Sheria ya Maadui Wageni (Alien Enemies Act) kama washukiwa wa kuwa wanachama wa makundi maalum ya kihalifu. Inaripotiwa kuwa wamefungwa katika Kituo cha Usalama wa Juu cha "Centre for Terrorism Confinement" (CECOT) nchini El Salvador, ambako wanatendewa kwa ukatili mkubwa, bila kupata msaada wa kisheria, kuonana na ndugu zao, au mawasiliano mengine na dunia ya nje.
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imepokea taarifa kutoka kwa wanafamilia na mawakili kuhusu zaidi ya raia 100 wa Venezuela wanaoaminika kushikiliwa katika CECOT. Ripoti hizi zinaonesha kuwa wengi wao hawakupewa taarifa kuhusu nia ya Serikali ya Marekani kuwahamisha hadi nchi ya tatu, hawakupata wakili na hawakuwa na uwezo wa kupinga kisheria uhalali wa uhamishaji wao kabla ya kuondolewa Marekani kwa ndege.
“Hali hii inaleta wasiwasi mkubwa kuhusu haki nyingi muhimu chini ya sheria za Marekani na sheria za kimataifa – haki ya kufanyiwa mchakato wa haki, kulindwa dhidi ya kufungwa kiholela, usawa mbele ya sheria, kulindwa dhidi ya mateso au madhara mengine yasiyorekebishika katika nchi nyingine, na haki ya kupata suluhisho la kisheria,” amesema Türk.
Hakuna orodha
Mpaka sasa, hakuna orodha rasmi ya waliokamatwa iliyotolewa na mamlaka za Marekani au El Salvador, huku hali yao ya kisheria nchini El Salvador ikiwa haijafahamika. Wanafamilia wengi waliohojiwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu walieleza huzuni kuu kwa kutofahamu walipo na hali waliyo nayo wapendwa wao.
Baadhi yao waligundua tu baada ya kuwaona wapendwa wao kupitia video zilizosambaa mitandaoni wakiwa wamefikishwa au wakipelekwa CECOT. Kwa mujibu wa taarifa zilizopokelewa, wale waliohamishwa kutoka Marekani hadi El Salvador hawajapata fursa halisi ya kupinga kifungo chao huko.
“Familia tulizozungumza nazo zimeeleza hali ya kukata tamaa kabisa kuhusu yaliyowakuta wapendwa wao na maumivu ya kuwaona wakiitwa wahalifu wa kutumia nguvu, hata magaidi, bila ya hukumu yoyote ya mahakama kuthibitisha madai hayo,” anasema Türk.
“Namna baadhi ya watu walivyokamatwa na kufukuzwa – ikiwemo kufungwa pingu – pamoja na lugha ya dharau inayotumiwa dhidi ya wahamiaji, pia ni jambo la kusikitisha sana.”
Pongezi na wito
“Napongeza mfumo wa mahakama wa Marekani, jumuiya ya sheria, na jamii ya kiraia kwa jukumu lao muhimu katika kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinalindwa katika muktadha huu,” ameongeza Türk.
“Nimeitaka Serikali ya Marekani kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kufuata utaratibu wa haki, kutekeleza kikamilifu maamuzi ya mahakama zake, kulinda haki za watoto, na kusitisha uhamishaji wa mtu yeyote hadi nchi ambayo kuna hatari halisi ya mateso au madhara mengine yasiyorekebishika.”