Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM kusaidia wanaohama kwa hiari Marekani kurejea katika nchi zao za asili

Jengo la Bunge la Marekani, Washington, DC.
© Unsplash/Harold Mendoza
Jengo la Bunge la Marekani, Washington, DC.

IOM kusaidia wanaohama kwa hiari Marekani kurejea katika nchi zao za asili

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limethibitisha tena dhamira yake ya muda mrefu ya kulinda haki na heshima ya wahamiaji kupitia mpango wake wa Kurudi kwa Hiari na kwa Usaidizi (AVR), ambao sasa unatekelezwa nchini Marekani kwa ombi la serikali ya Marekani.

Katika taarifa iliyotolewa leo Mei 12 na msemaji wa IOM, imefafanua jukumu la shirika hilo katika kuwasaidia wahamiaji walioko Marekani wanaoamua kwa hiari kurejea katika nchi zao za asili.

 

IOM haihusiki na kurejesha watu kwa nguvu

 
Shirika hilo limesisitiza kuwa linaanza kutoa msaada tu baada ya mtu kutoa idhini ya hiari, na likabainisha kwamba halihusiki na wala halitekelezi hatua za kuwarejesha wahamiaji kwa nguvu.
 
“Kwa miongo kadhaa, IOM imekuwa ikisaidia programu za AVR katika zaidi ya nchi 100—ikisaidia watu wasio na rasilimali, chaguo za kisheria au msaada wowote kurudi katika nchi zao kwa usalama na heshima,” amesema msemaji wa IOM. “AVR ni njia iliyothibitishwa inayozingatia haki, inayowawezesha wahamiaji wanaokumbana na changamoto za mifumo tata ya uhamiaji duniani kupata uwezo wa kufanya maamuzi sahihi.”
 

Kinachofanyika

 
Mpango wa AVR huwapatia wahamiaji taarifa sahihi, msaada wa usafiri, na huduma muhimu ili kuwezesha kurejea kwa usalama na heshima. Juhudi hii ni muhimu zaidi nchini Marekani, ambako wahamiaji wengi hukumbana na hali ngumu na chaguzi chache katika mfumo wa uhamiaji uliochangamana.
 
“IOM huwasaidia watu kuelewa ugumu wa mifumo ya uhamiaji ili waweze kupata utulivu, usalama, na uwezo wa kufanya uamuzi wa maana kuhusu maisha yao ya baadaye,” taarifa hiyo iliendelea. “Mpango huu unatoa msaada kwa wale wanaochagua kurudi, na kuwasaidia kufanya uamuzi wa kubadilisha maisha yao kwa umakini na ufahamu.”
 
Shirika hilo limesisitiza wajibu wake wa kimataifa wa kuwalinda watu walio hatarini na kutetea kanuni za heshima ya kibinadamu na uhamiaji salama, unaopangwa na unaozingatia haki—iwe ni kwenda makazi mapya au kurejea nyumbani.