Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

India na Pakistani: Katibu Mkuu UN akaribisha makubaliano ya kusitisha mapigano

Katibu Mkuu UN António Guterres akizungumza kwenye jukwaa wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama UN mjini New York.
UN Photo/Mark Garten Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi wa habari (Picha Maktaba)

India na Pakistani: Katibu Mkuu UN akaribisha makubaliano ya kusitisha mapigano

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amekaribisha makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya India na Pakistan, akiyataja kama “hatua chanya” kuelekea kupunguza uhasama na kuimarisha amani ya kudumu katika eneo hilo.

Katika taarifa iliyotolewa leo Mei 10 asubuhi saa za New York, Marekani na msemaji wake, Stéphane Dujarric, Katibu Mkuu ameeleza matumaini kuwa makubaliano hayo yatasaidia kupunguza mvutano na kuweka mazingira ya kushughulikia masuala mapana na ya muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili ya Asia Kusini.
 
"Katibu Mkuu anakaribisha makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya India na Pakistan kama hatua chanya ya kumaliza uhasama wa sasa na kupunguza mvutano," ameandika Dujarric. "Anatumaini kuwa makubaliano haya yatachangia amani ya kudumu na kuimarisha mazingira ya kushughulikia masuala ya muda mrefu kati ya nchi hizo mbili."
 
Umoja wa Mataifa umesisitiza utayari wake wa kusaidia juhudi zozote zinazolenga kukuza amani na utulivu katika eneo hilo. “Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia juhudi zinazolenga kukuza amani na utulivu katika kanda hii,” taarifa hiyo iliongeza.
 
Makubaliano haya ya kusitisha mapigano yanaonekana kama hatua muhimu katika uhusiano wa India na Pakistan, ambao kwa muda mrefu umekuwa na migogoro ya mara kwa mara ya kijeshi na mvutano wa kisiasa, hususan kuhusu eneo la Jammu na Kashmir.