Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres atuma pongezi kwa Papa Leo wa XIV

Mtazamo wa angani wa Jiji la Vatikani na Roma kutoka juu ya Basilica ya Mtakatifu Petro.
UN News/Li Zhang Mtazamo wa mji wa Vatikani.

Guterres atuma pongezi kwa Papa Leo wa XIV

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma salamu za pongezi kwa Kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo wa XIV.

Taarifa hiyo ya pongezi imetolewa leo Alhamisi alasiri jijini New York, Marekani na Msemaji wa Umoja wa Mataifa, na inafuatia kuchaguliwa hii leo kwa Papa Leo XIV ambaye anakuwa mmarekani wa kwanza kushika wadhifa huo wa kuongoza madhehebu ya katoliki yenye waumini takribani bilioni 1.4 duniani kote.

Guterres amesema “natuma salamu zangu za dhati kwa Baba Mtakatifu Leo XIV pamoja na waumini wote wa kikatoli duniani.”

Amesema “uchaguzi wa Papa mpya ni tukio lenye umuhimu mkubwa wa kiroho kwa mamilioni ya waumini kote duniani, na unakuja wakati wa changamoto kubwa za kimataifa.”

Dunia yahitaji sauti za kusongesha haki na amani

Katibu Mkuu amesema “dunia yetu inahitaji sauti zenye nguvu zaidi kwa ajili ya amani, haki ya kijamii, heshima ya utu wa binadamu, na huruma.”

Ameongeza kuwa “ninatarajia kuendeleza utamaduni wa muda mrefu wa ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Holy See utamaduni  uliodumishwa zaidi miaka ya karibuni na Hayati Papa Francis ili kuimarisha mshikamano, kukuza upatanisho, na kujenga dunia ya haki na endelevu kwa wote.”

Guterres amesema mambo hayo yamejidhihirisha kwenye kauli yake ya mwanzoni kabisa baada ya kuchaguliwa hii leo ambapo amemnukuu “licha ya utofauti mkubwa wa asili na imani, watu kila mahali wanashiriki lengo la pamoja: Amani na iwe duniani kote.”

Kuchaguliwa kwa Papa Leo XIV ambaye jina lake halisi ni Robert Prevost kunafuatia kifo cha Papa Francis tarehe 21 mwezi Aprili mwaka huu.