Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali mbaya ya hewa na mabadiliko ya tabianchi vyaliacha hoi bara la Afrika, yaonya WMO

Hali mbaya ya hewa na mabadiliko ya tabianchi vyaliacha hoi bara la Afrika.
WMO
Hali mbaya ya hewa na mabadiliko ya tabianchi vyaliacha hoi bara la Afrika.

Hali mbaya ya hewa na mabadiliko ya tabianchi vyaliacha hoi bara la Afrika, yaonya WMO

Tabianchi na mazingira

Ripoti mpya kuhusu “Hali ya Hewa Afrika 2024” iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani WMO imeonya kwamba muongo wa joto zaidi kuwahi kushuhudiwa Afrika umeleta madhara makubwa kwa bara hilo. Katika ripoti hiyo iliyotolewa mjini Addi Ababa na Geneva WMO imesema “Afrika imeshuhudia muongo wa joto zaidi katika historia, huku joto kali, mawimbi ya joto baharini yasiyokuwa ya kawaida, mafuriko na ukame unaokatili maisha ya watu vikizidi kuongezeka kote barani humo”.

Katibu Mkuu wa WMO, Celeste Saulo amesema "Ripoti ya Hali ya Hewa Afrika inaonesha uharaka na uhalisia unaoongezeka wa mabadiliko ya tabianchi barani humo. Tunaona mwelekeo wa wazi wa matukio ya hali mbaya ya hewa yanayotishia maisha, kipato, na uchumi."

Athari za mafuriko katika nchi mbalimbali za  Afrika
OCHA/Lokuju Peter
Athari za mafuriko katika nchi mbalimbali za Afrika

Mafuriko na ukame wa muda mrefu ni janga kubwa

Mwaka 2024, kwa mujibu wa ripoti Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ilikumbwa na ukame mbaya zaidi katika angalau miongo miwili, huku nchi kama Zambia na Zimbabwe zikishuhudia kupungua kwa mavuno ya nafaka kwa asilimia 43 Zambia na asilimia 50 Zimbabwe chini ya wastani wa miaka mitano.

Wakati huo huo, Afrika Mashariki ilipata mafuriko mabaya yaliyowafurusha zaidi ya watu 700,000 na kuua mamia nchini Kenya, Tanzania, na Burundi.

Dkt. Mary Kambona, mtaalamu wa tabianchi wa Kikanda amesema “Tunapambana na majanga kwa pande zote mbili, maeneo mengine yamekauka wakati mengine yanafurika. Hili ni janga la kibinadamu na la maendeleo kwa wakati mmoja."

Mawimbi ya joto baharini yaathiri jamii za pwani

Joto la uso wa bahari kuzunguka Afrika lilifikia rekodi mpya mnamo 2024, imesema ripoti hiyo huku mawimbi ya joto baharini yakikumba takribani kilomita za mraba milioni 30 kutoka Januari hadi Aprili eneo kubwa zaidi tangu ufuatiliaji uanze mwaka 1993.

Jotola kiwango cha juu la bahari WMO inasema linavuruga mifumo ya ikolojia ya baharini na kuongeza nguvu za dhoruba za kitropiki, na hivyo kuwa tishio zaidi kwa jamii za pwani.

"Mchanganyiko wa kupanda kwa kina cha usawa wa bahari, dhoruba kali, na maji ya bahari yenye joto ni bomu linalosubiri kulipuka kwa miji ya pwani Afrika," ameonya Dkt. Emmanuel Osei, mtaalamu wa tabianchi za baharini kutoka shirika la WMO.

Kaunti ya Turkana, kaskazini mwa Kenya, hukumbwa na ukame mara kwa mara.
© UNCCD/Mwangi Kirubi
Kaunti ya Turkana, kaskazini mwa Kenya, hukumbwa na ukame mara kwa mara.

Hali mbaya ya hewa inahatarisha uhakika wa chakula na nishati

Ripoti hiyo ya WMO kuhusu hali ya hewa Afrika 2024 imesema “Afrika Kaskazini ilirekodi mavuno yake ya nafaka chini ya wastani kwa mwaka wa tatu mfululizo kutokana na ukame na joto kali, huku uzalishaji wa Morocco ukishuka kwa asilimia 42 chini ya wastani wa miaka mitano.”

Pia imesema uzalishaji wa umeme wa kutumia maji Afrika Kusini ulipungua kwa sababu ya viwango vya chini vya maji, na kusababisha kukatika kwa umeme kwa muda mrefu na usumbufu wa kiuchumi.

“Matukio ya hali mbaya ya hewa pia yanahatarisha uhakika wa chakula, maji, na nishati Afrika kwa wakati mmoja," Saulo amebainisha akiongeza kuwa "Athari hizi zinazofuatana zinachochea umaskini na kuhatarisha mafanikio ya maendeleo."

Mabadiliko ya kidijitali yaleta matumaini ya mnepo dhidi ya tabianchi

Licha ya matokeo mabaya, ripoti ya WMO inaangazia juhudi zinazoongezeka barani Afrika kutumia zana za kidijitali kwa tahadhari za mapema na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa ripoti “Nchi kama Nigeria, Kenya, na Afrika Kusini zinatumia AI, majukwaa ya simu, na mifumo ya utabiri wa hali ya hewa ya kisasa kutoa taarifa za wakati kwa wakulima, wavuvi, na jamii.” Pia Saulo amesema "Mabadiliko ya kidijitali ndiyo nafasi bora zaidi ya Afrika kujijengea menepo dhidi ya janga la tabianchi. Lakini yanahitaji uwekezaji wa dharura katika miundombinu, ushirikiano wa takwimu, na huduma shirikishi."

Kama shirika mdau wa UNEP, CVTL inawajibika kwa mipango ya kutoa onyo la mapema kwa jamii katika vijiji sita kote Timor-Leste.
UN News/Felipe de Carvalho
Kama shirika mdau wa UNEP, CVTL inawajibika kwa mipango ya kutoa onyo la mapema kwa jamii katika vijiji sita kote Timor-Leste.

Wito wa hatua za dharura kuimarisha tahadhari za mapema

Ripoti hiyo ya WMO imezihimiza serikali, washirika wa maendeleo, na sekta binafsi kuharakisha uwekezaji wa tabianchi unaozingatia ujasiri na kupanua wigo wa mifumo ya tahadhari za mapema kote barani Afrika.

"Bila mifumo imara ya tahadhari za mapema na hatua za mabadiliko, hatari zitaendelea kuongezeka," amesisitiza Saulo akiongeza kwamba "Ripoti hii ni wito wa kuchukua hatua za pamoja kwa suluhu za changamoto ya tabianchi inayozidi kuwa ngumu."

Matokeo haya yanakuja wakati mataifa ya Afrika yakijiandaa kwa mazungumzo muhimu ya tabianchi baadaye mwaka huu, ambapo ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi na ujenzi wa mnepo vinatarajiwa kutawala ajenda.