UNHCR yaomba haraka dola milioni 781 kufuatia ongezeko la wakimbizi Kutoka DRC
UNHCR yaomba haraka dola milioni 781 kufuatia ongezeko la wakimbizi Kutoka DRC
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR leo limetoa ombi la dharura la msaada kufuatia ongezeko kubwa la wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, ambapo sasa zaidi ya ya milioni moja wahitaji msaada katika nchi saba
Kadri machafuko yanavyozidi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, UNHCR pamoja na mashirika washirika 107 wameomba msaada wa haraka wa dola milioni 781 ili kuendelea kutoa msaada wa kuokoa maisha mwaka 2025. Mpango ulioratibiwa wa kukabiliana na wakimbizi (RRP) unalenga kusaidia zaidi ya wakimbizi na waomba hifadhi milioni moja wa Congo DRC walioko katika nchi jirani, pamoja na zaidi ya watu milioni moja katika jamii zinazowapokea huko Angola, Burundi, Jamhuri ya Congo, Rwanda, Uganda, Tanzania, na Zambia.
Chansa Kapaya, Mkurugenzi wa Kanda wa UNHCR Kusini mwa Afrika amesema
“Kiwango cha janga hili ni cha kutisha, na jamii zinazowapokea haziwezi kuhimili peke yao.”
Wakimbizi wengi wanatoka Mashariki mwa DRC
UNHCR inasema hali Mashariki mwa DRC imezidi kudorora, huku mapigano yakiendelea kuwalazimisha watu kukimbia kwa kiwango kisichowahi kushuhudiwa tangu Januari.
Takribani watu 150,000 wamekimbia nchi hiyo mwaka huu pekee na tayari wamezidi idadi ya mwaka mzima uliopita wengi wakitafuta hifadhi Burundi na Uganda.
“Kwa mara nyingine tena, ni familia, hasa wanawake na watoto, wanaolazimika kukimbia kuokoa maisha yao wakati vurugu zinapotawala,” amesisitiza Kapaya. Ndani ya DRC, idadi ya watu waliofurushwa makwao imefikia kiwango cha juu zaidi, cha takriban watu milioni 7.8 kufikia mwisho wa 2024.
Nchi jirani zazidiwa na shinikizo la wakimbizi wapya
Ingawa mataifa jirani yanaonyesha ukarimu, kwa mujibu wa UNHCR yanaelemewa na wimbi la wakimbizi wapya.
Vituo vya mpito na mapokezi vimefurika kupita kiasi na havina rasilimali za kutosha kutoa makazi salama, maji safi, huduma za usafi, huduma za afya na ulinzi.
“Bila kuongezwa kwa ufadhili, mashirika yaliyo mstari wa mbele yatakabiliwa na maamuzi magumu, kama vile kufunga huduma za afya, kupunguza msaada wa chakula, au kuwaacha waathirika wa ukatili wa kingono bila msaada,” ameonya Kapaya.
Ukata wa fedha wasababisha huduma muhimu kukatwa
Licha ya kuongezeka kwa mahitaji, ufadhili wa kibinadamu kwa ajili ya DRC umesalia kuwa mdogo sana.
Mwaka 2024, UNHCR na washirika walipokea chini ya nusu ya fedha zilizohitajika, jambo lililolazimisha mashirika ya misaada kupunguza mgao wa chakula, kupunguza huduma muhimu na kupunguza msaada kwa makundi yaliyo hatarini zaidi.
Mpango wa RRP unaweka vipaumbele kwenye makazi ya dharura, chakula, huduma za afya, na huduma za ulinzi, huku pia ukikuza ujumuishwaji wa kijamii na suluhisho za muda mrefu kwa watu waliofurushwa makwao.
Wito wa mshikamano wa kimataifa kwa janga lililosahaulika
Ombi la UNHCR linakamilisha mpango mkubwa wa kukabiliana na hali ya kibinadamu nchini DRC, uliozinduliwa Februari.
Pamoja, juhudi hizi zinakusudia kushughulikia mahitaji ya haraka na ya muda mrefu katika moja ya migogoro mikubwa duniani ambayo haijapewa uzito unaostahili.
“Jumuiya ya kimataifa lazima iongeze msaada wake kwa haraka ili kusaidia juhudi za serikali zinazowapokea wakimbizi na mashirika yote ya kibinadamu kutoa ulinzi na msaada muhimu,” Kapaya amesisitiza na kuongeza kuwa “Wakimbizi wasipopata msaada na ulinzi wanaohitaji katika nchi wanazotafuta usalama, mara nyingi wanalazimika kuendelea na safari hatari wakitafuta utu na matumaini kwingine.”