Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaonya kuhusu mahitaji makubwa ya ulinzi kufuatia wimbi la wakimbizi wa Sudan kuingia Chad

Mama ambaye amekimbia machafuko Sudan anasubiri usaidizi katika kituo cha usambazaji chakula nchini Chad.
© WFP/Eloge Mbaihondoum
Mama ambaye amekimbia machafuko Sudan anasubiri usaidizi katika kituo cha usambazaji chakula nchini Chad.

UNHCR yaonya kuhusu mahitaji makubwa ya ulinzi kufuatia wimbi la wakimbizi wa Sudan kuingia Chad

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia  Wakimbizi UNHCR leo limeonya a kuhusu ongezeko kubwa la wakimbizi waliokimbia machafuko ya Darfur Sudan na kuingia katika nchi Jirani ya Chad.

Katika taarifa yake iliyotolewa mjini Geneva Uswisi UNHCR imetoa wito wa dharura kwa msaada wa kimataifa baada ya karibu wakimbizi 20,000 kutoka Sudan, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kuvuka na kuingia mashariki mwa Chad katika kipindi cha wiki mbili zilizopita wakikimbia ukatili unaoongezeka katika eneo la Darfur Kaskazini, Sudan.

Magatte Guisse, Mwakilishi wa UNHCR nchini Chad, akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva amesema “Uharaka na ukubwa wa wimbi hili la wakimbizi ni jambo la kutisha. Tunashuhudia familia zilizochoka, zikiwa na majeraha ya kisaikolojia, zikifika bila chochote, baada ya kukimbia mashambulizi ya kutisha.”

Kituo cha mpakani cha Tiné kimefurika

Kwa mujibu wa shirika hilo la wakimbizi idadi kubwa zaidi ya wakimbizi imeandikishwa katika kituo cha mpakani cha Tiné kilichopo mkoa wa Wadi Fira, Chad, ambako karibu watu 6,000 walivuka katika kipindi cha siku mbili wiki iliyopita.

Tangu Aprili 21, zaidi ya watu 14,000 wamewasili Wadi Fira, huku wengine 5,300 wakikimbilia Ennedi Est jirani.

Limeongeza kuwa wakimbizi hao wanatoroka mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na makundi yenye silaha huko Darfur Kaskazini, ikiwa ni pamoja na mashambulizi kwenye kambi za wakimbizi wa ndani kama Zamzam na Abu Shouk, pamoja na mapigano makali katika mji mkuu wa eneo hilo, El Fasher.

Wakimbizi wameripoti mauaji ya watu, ukatili wa kijinsia na nyumba kuchomwa moto wakati vurugu zikiongezeka.

“Zaidi ya watu 10,000 bado wako njiani, wakijaribu kwa udi na uvumba kuvuka mpaka kuingia Chad,” amesema Guisse.

Hatari za ulinzi na changamoto za kibinadamu

Tathmini za haraka zilizofanywa na UNHCR zimeonyesha hali mbaya ya ulinzi. Asilimia 76 ya wakimbizi wapya wameripoti kupitia visa vikubwa vya ukiukaji wa haki ikiwa ni pamoja na uporaji, ulaghai, na ukatili wa kingono  katika safari zao. Timu za ulinzi zimewatambua watu wengi walio katika mahitaji maalum, wakiwemo watoto waliotengwa na wazazi, wanawake wajawazito na wanaonyonyesha, pamoja na wazee walionusurika.

Kwa mujibu wa Guisse “Wengi waliowasili walikuwa na majeraha, na baadhi wakiripotiwa kuanguka kutoka kwenye magari yaliyokuwa yamejazwa kupita kiasi wakati wa kukimbia kwa hofu. Hadithi tunazozisikia ni za kusikitisha sana,”

UNHCR imeonya kwamba uwezo wa Chad kuwahifadhi wakimbizi unakabiliwa na changamoto kubwa.

Nchi hiyo tayari inawahifadhi wakimbizi milioni 1.3, wakiwemo karibu 800,000 kutoka Sudan tangu mzozo ulipoanza zaidi ya miaka miwili iliyopita. Ingawa jamii za wenyeji na mamlaka zimeonyesha mshikamano wa kipekee, rasilimali zimekuwa chache sana.

Wito wa mshikamano wa kimataifa na ufadhili

Tangu mwishoni mwa Aprili, UNHCR imehamisha karibu wakimbizi 1,850 waliowasili hivi karibuni kwenda Iridimi, eneo la wakimbizi katika mkoa wa Wadi Fira, na inatoa msaada wa dharura katika vituo vya mipakani.

Hata hivyo, mashirika ya kibinadamu yanaonya kwamba juhudi za sasa hazitoshelezi mahitaji ya dharura. Mashambulizi dhidi ya raia Sudan lazima yakome, na njia salama lazima zipatikane kwa wale wanaokimbia machafuko,” amesisitiza Guisse, akiomba msaada zaidi wa kimataifa.

“Kati ya dola milioni 409 zinazohitajika kwa kukabiliana na janga la wakimbizi Chad mwaka 2025, ni asilimia 20 tu iliyopatikana hadi sasa. Tunahitaji mshikamano zaidi na ufadhili wa haraka ili kuhakikisha watu hawa walio hatarini wanapata ulinzi na msaada wanaouhitaji, sasa,” amesema Guisse.

Janga linaloongezeka bila dalili ya kukoma

Kadri machafuko yanavyozidi Darfur, hali ya kibinadamu pande zote za mpaka inazidi kuzorota.

UNHCR inaonya kuwa bila hatua za haraka kutoka kwa jamii ya kimataifa, watu walio hatarini watakabiliwa na matatizo makubwa zaidi.

“Watu wa Chad wamefungua mikono yao kuwapokea,” amesema Guisse. “Sasa, dunia pia lazima ifanye vivyo hivyo.”