Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres ataka hatua za kimataifa juu ya Akili Mnemba na  uandishi wa Habari

Wapiga picha wenye lenzi ndefu kwenye mkutano wa waandishi wa habari.
© UNFCCC/Kiara Worth Waandishi wa habari wakati wakichukua picha na taarifa wakati wa mkutano wa mabadiiko ya tabianchi

Guterres ataka hatua za kimataifa juu ya Akili Mnemba na  uandishi wa Habari

Haki za binadamu

Kuelekea siku ya kimataifa ya uhuru wa vyombo vya habari Mei 3, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema waandishi wa habari wanakabiliwa na hatari kila uchao huku teknolojia mpya ya akili mnemba au AI ingawa licha ya manufaa nayo pia inaibua hatari mpya kwenye uhuru wa kujieleza.

Katika ujumbe wake wa siku hiyo Guterres amesema uhuru wa vyombo vya habari si anasa bali ni hitaji muhimu kwa ajili ya haki, uwajibikaji, na ulinzi wa haki za binadamu.

Wanahabari wakishindwa kufanya kazi yao, dunia inapotea

“Uhuru wa watu unategemea uhuru wa vyombo vya Habari. Uandishi huru na wa kujitegemea ni huduma ya msingi kwa umma.  Waandishi wa habari wanaposhindwa kufanya kazi yao, sisi sote tunapoteza,” amesema Guterres.

Akifafanua hatari wanazokumbana nazo waandishi wa habari, Katibu Mkuu amesema pamoja na kudhibitiwa kwenye kazi zao, wanakumbwa pia na vitisho, ghasia, na hata kuuawa.

“Masikitiko yangu makubwa kwa ongezeko la mauaji ya waandishi wa habari, hasa katika maeneo yenye migogoro kama Gaza,” amesema Katibu Mkuu.

Mwandishi wa habari wa Palestina amevaa jina la vyombo vya habari na kofia ya usalama akizungumza kwenye kipaza sauti kando ya kamera ya video huko Gaza.
© UNDP PAPP/Abed Zagout Mwandishi wa TV Mustafa Al-Bayed, akiripoti kutoka Gaza.

Akili mnemba ni upanga wenye makali pande mbili

Akigeukia maudhui ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uhuru wa vyombo vya habari mwaka huu yanayomulika matumizi ya akili mnemba kwenye uandishi wa habari, Guterres amefananisha akili mnemba na upanga wenye makali pande mbili.

“Ingawa akili mnemba au AI inaweza kusaidia kukuza uhuru wa kujieleza, teknolojia hiyo hiyo pia inaweza kusambaza habari potofu, kuchochea ubaguzi, na kuendeleza hotuba za chuki,” amesema Katibu Mkuu.

“Mchakato wa upendeleo wa kukublika kwa taarifa, uongo wa wazi, na hotuba za chuki ni kama mabomu yaliyofichwa kwenye njia kuu za kusambaza taarifa,” amesema Katibu Mkuu.

Ameongeza kuwa “habari sahihi, thabiti, na zinazotegemea ukweli ni silaha bora ya kuzuia taarifa hizo za uongo.”

Mikakati ya UN kudhibiti udanganyifu mtandaoni

Guterres ametaja juhudi za karibuni za Umoja wa Mataifa za kulinda uadilifu wa taarifa, ikiwemo Mkataba wa Kidijitali wa Kimataifa na Kanuni za Kimataifa za Uadilifu wa Taarifa, ambazo zote zilizinduliwa mwezi Septemba mwaka jana wa 2024.

Amesema mipango hii inalenga kuhakikisha teknolojia za kidijitali zinatengenezwa na kutumiwa kwa njia zinazolinda haki za binadamu na kuendeleza mazungumzo ya kweli na yenye heshima.

Amehitimisha ujumbe wake kwa kutoa wito wa kimataifa wa kutetea na kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari kwa kila namna akisema, "tujitolee kuhakikisha hili linatimia na kulinda uhuru wa vyombo vya habari popote duniani."

Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 3 Mei, hutambua nafasi muhimu ya uandishi wa habari katika jamii za kidemokrasia na kuwaenzi waandishi wa habari waliopoteza maisha wakitekeleza majukumu yao.

Wapiga picha na kamera nyingi za video wamepangwa kwenye mkutano wa waandishi wa habari huko Mogadishu, Somalia.
UN Photo/Fardosa Hussein Waandishi wa habari nchini Somalia wakihudhuria mkutano. (Maktaba)

Ukiritimba wa vyombo vya habari na AI

Hoja ya matumizi ya akili mnemba au AI imezungumziwa pian a Volker Türk, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu kwenye ujumbe wake wa siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.

“Sheria kuhusu ukiritimba wa umiliki wa vyombo vya habari lazima ziangaliwe upya ili ziakisi nguvu ya AI na majukwaa ya kiteknolojia na kuendeleza fursa pana za aina mbali mbali za vyombo vya habari ili kuweka nafasi ya uandishi huru wa habari,” amesema Türk

Kampuni za teknolojia na madhara ya teknolojia zao kwa wanahabari

Ameongeza kuwa kampuni za teknolojia nazo zina nafasi muhimu na ndio maana “leo tunazindua pamoja na UNESCO mwongozo wa kusaidia kampuni za teknolojia kutathmini madhara  ya teknolojia zao kwa waandishi wa habari na sauti muhimu.”

Hivyo amesema siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani iwe ni fursa ya kila mtu kujitolea kwa dharura kubadili mwelekeo sio tu kwenye AI lakini pia kwenye usalama wa waandishi wa habari wanapofanya kazi.

Amesema “hii inaanza na mataifa. Lazima yahakikishe kuwa waandishi wa habari wako salama, hawashambuliwi, hawakumbwi na kampeni za chuki, ufuatiliaji, na unyanyasaji wa kimwili na wa kisheria. Serikali lazima zitathmini madhara yake kwa haki za binadamu.”

Amesisitiza kuwa ni muhimu kuwe na uwazi zaidi kuhusu jinsi data zinavyotumika, jinsi maudhui yanavyochaguliwa, na jinsi algoridhimu  zinavyoundwa. Vyombo vya habari huru, vinavyojitegemea na vyenye utofauti vinaweza kusaidia kuondoa migawanyiko katika jamii zetu. Lazima tufanye kila tuwezalo kuvilinda na kuviwezesha kustawi.