Wanaokata ufadhili wafike Afghanistan wajionee madhara kwa macho yao - Fletcher
Wanaokata ufadhili wafike Afghanistan wajionee madhara kwa macho yao - Fletcher
MKuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, OCHA, Tom Fletcher, amezungumzia madhara makubwa ya binadamu yatokanayo na kupunguza kwa misaada ya kimataifa, akiwataka watunga sera kujionea wenyewe madhara ya uamuzi wao huo kwa macho yao wenyewe kwa kutembelea Afghanistan.
Katika mahojiano ya maalum na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kutoka Afghanistan aliko ziarani, Fletcher hakumung’unya maneno akisema, “hatimaye, bila shaka, watu watakufa kwa sababu ya kupunguzwa huku kwa misaada. Hilo ndilo janga kubwa lililo katikati ya hali hii sasa,”
Amerejelea kufungwa kwa kliniki 400 hivi karibuni nchini Afghanistan, na kufutwa kazi kwa wafanyakazi wengi wa mashirika yasiyo ya kiserikali kote nchini humo.
Mashirika ya misaada ya ndani ndio yamedhurika zaidi
Akiwa ametoka kwenye mkutano na mashirika ya misaada ya ndani nchini Afghanistan, Fletcher amesisitiza madhara makubwa kwa mashirika madogo ya kijamii—ambayo mara nyingi hutambuliwa kama nguzo muhimu katika maeneo ya migogoro.
“Mashirika ya ndani tunayojaribu kulinda raia katikati ya hali hii ndiyo yameathirika zaidi,” amesema.
Alipoulizwa kama hutumia lugha hiyo hiyo ya wazi anapozungumza faraghani na watunga sera wa kimataifa, Fletcher amesema, “ndiyo, ninatumia.”
Ukijitenga na dunia janga unalokwepa litakuja kwako
Fletcher, ambaye aliwahi kuwa mshauri wa sera za nje kwa Mawaziri Wakuu watatu wa Uingereza na alitetea ahadi ya asilimia 0.7 ya bajeti ya misaada, amesema mazingira ya sasa ya kimataifa yanahitaji utetezi mpya wa bajeti za kibinadamu.
“Huwezi kujitenga na dunia; lazima ukabiliane na changamoto za kimataifa pale zilipo,” amesisitiza, “la sivyo, janga lijalo, msukosuko wa kiuchumi au wimbi la uhamiaji linalosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, umasikini na migogoro litakuja kuelekea kwenu, na huwezi kujenga ukuta mkubwa wa kutosha kuzuia matatizo hayo.”
Wanasiasa wanaosherehekea kukatwa ufadhili
Amesema kuwa kuna makundi mawili tofauti kati ya watunga sera wa sasa: wale wanaofanya maamuzi magumu kutokana na shinikizo la kiuchumi, na wale ambao “husherehekea” na “kujivunia” kupunguza misaada.
Fletcher amesema kuwa kundi hilo la pili linapaswa kupelekwa “wakakae na mama aliyempoteza mtoto wake kwa sababu alilazimika kuendesha baiskeli akiwa mjamzito kwa saa tatu hadi hospitali.”
Akisisitiza wajibu wa maadili na umuhimu wa kimkakati, Fletcher ametoa wito kwa sekta ya misaada ya kibinadamu kuendelea kuwa na fahari na kusimama imara. “Tumeondoa mamilioni kutoka kwenye umasikini na kuokoa maisha ya mamia ya mamilioni ya watu,” amesema Fletcher na kuongeza kuwa, “hilo ni jambo la kujivunia—kwa sauti ya juu.”
Pata mahojiano yote hapa.