WHO inasaidia kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Kimeta nchini DRC
WHO inasaidia kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Kimeta nchini DRC
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni WHO linashirikiana na Mamlaka za afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kuongeza juhudi za dharura ili kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa kimeta ulioripotiwa katika mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa leo na WHO kutoka Kinshasa Congo imeeleza kuwa mpaka sasa mtu mmoja ameripotiwa kufa, mmoja amethibitishwa kuugua na wengine 16 wanashukiwa kuwa na ugonjwa huo. Takiwmu hizo ni kutoka katika manne ya huduma za afya yaliyo karibu na Ziwa Edward, mpakani mwa DRC na Uganda.
Mlipuko huu umehusishwa na ule unaoendelea upande wa Uganda, hususan katika wilaya ya Kabale Magharibi ambako pia watu saba wanashukiwa kuugua ugonjwa huo.
WHO wanafanya nini?
Kwa kushirikiana na serikali, jamii na wadau, WHO inahakikisha kuwa maambukizi kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu yanazuiliwa haraka.
Mwakilishi wa WHO nchini DRC Dkt. Boureima Sambo ameeleza wamefanya tathmini kubaini hatari ya maambukizi kuenea zaidi na inasaidia mamlaka za afya nchini DRC kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa na uchunguzi wa vyanzo vya maambukizi pamoja na minyororo ya maambukizi.
“Juhudi zetu zimeelekezwa katika kukomesha maambukizi kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu. Tunafanya kazi kwa karibu na serikali, jamii na wadau kuimarisha hatua za kukabiliana na mlipuko huu ili kulinda afya ya umma kwa sasa na baadaye.”
WHO inatoa vifaa tiba na kusaidia matibabu na pia inaratibu jitihada za pamoja kati ya DRC na Uganda ili kuimarisha mwitikio wa pamoja wa mipakani.
Jitihada za kukabiliana na mlipuko huo pia zinajumuisha chanjo kwa mifugo.
Kimeta ni nini na unaambukizwa vipi?
Kimeta ni ugonjwa wa bakteria unaoathiri zaidi wanyama. Binadamu wanaweza kuambukizwa kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja kutoka kwa wanyama walioambukizwa au kupitia bidhaa zilizotengenezwa kutoka kwa wanyama hao. Ingawa ni nadra sana, kuna matukio machache ya maambukizi kutoka kwa binadamu kwenda kwa binadamu yaliyowahi kuripotiwa.
Ugonjwa huu huonekana kwa njia tatu kwa binadamu:
- Kimeta cha ngozi (cutaneous): aina ya kawaida zaidi, husababishwa na kugusana na vimelea kupitia ngozi iliyojeruhiwa, na huanza kwa uvimbe unaowasha na kisha kuwa kidonda cheusi.
- Kimeta cha tumbo (gastrointestinal): hutokana na kula nyama iliyoambukizwa, na huweza kuleta maumivu makali ya tumbo, kutapika damu na kuharisha.
- Kimeta cha kupumua (inhalation): aina nadra na hatari zaidi, hutokea kwa kuvuta vimelea na huanza kama mafua lakini huweza kusababisha matatizo makubwa ya upumuaji na mshtuko wa mwili.
Mbinu ya "One Health" yaunganisha afya ya binadamu, wanyama na mazingira
WHO na washirika wake wanatumia mbinu ya Afya Moja (One Health), inayotambua kuwa afya ya binadamu, wanyama na mazingira zinahusiana kwa karibu. Kupitia ushirikiano huu, hatua za kudhibiti ugonjwa huu zinaweza kuchukuliwa kikamilifu kutoka katika kuzuia, kugundua, kujiandaa, kukabiliana na kusimamia hali, hivyo kuchangia katika usalama wa afya ya dunia kwa ujumla.