Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa misaada wa UN aishutumu Israel kwa kuendelea kuzuia misaada Gaza

Wanawake na watoto wa Kipalestina wanapokea mgao wa chakula katika kituo cha usambazaji WFP katika kambi ya Nusierat, Ukanda wa Gaza.
© WFP Watu huko Gaza wanakosa chakula huku kizuizi cha misaada kikiendelea.

Mkuu wa misaada wa UN aishutumu Israel kwa kuendelea kuzuia misaada Gaza

Amani na Usalama

Mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher leo ametoa wito wa kuondoa vizuizi vya misaada mara moja Gaza, aonya kuhusu mateso yanayoendelea kwa raia miezi mwili tangu kuanza kwa vizuizi hiyo Gaza.

Tweet URL

Katika taarifa yake afisa mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA amesema vizuizi hivyo vya makusudi vya Israel dhidi ya misaada vinagharimu maisha ya raia na vinakiuka sheria za kimataifa.

Katika taarifa nzito Tom Fletcher, amezitaka mamlaka za Israel “kuondoa kizuizi hiki cha kikatili cha misaada na kuruhusu msaada unaookoa maisha kuingia katika eneo hilo lililozingirwa nakukaliwa kimabavu”.

Kuzuia misaada kunakatili maisha

Fletcher amesema kwamba miezi miwili iliyopita, Israel ilifanya “uamuzi wa makusudi kuzuia misaada yote ya kibinadamu kuingia Gaza, na hivyo kusimamisha juhudi za Umoja wa Mataifa za kuwasaidia walionusurika kutokana na mashambulizi ya kijeshi”.

Aongeza kuwa Israel imekuwa “wazi kwa uthubutu kuhusu nia yake ya kuishinikiza Hamas”, lakini alisisitiza kuwa mbinu kama hizo hazikubaliki chini ya sheria za kimataifa na zinaowaathiri zaidi ni raia  wasio na hatia.

Ameonya kwamba “Kuzuia misaada kunawanyima raia chakula, kunawaacha bila huduma za msingi za afya, kunawavua utu na matumaini na kunaweka katika adhabu ya pamoja isiyo na huruma”.

Ameendelea kusisitiza kwamba “Kuzuia misaada kunaua.”

Mfanyakazi wa Mpango wa Chakula Duniani anatembea kati ya safu za malori ya msaada wa chakula nje ya Gaza.
© WFP Malori yaliyobeba chakula yakisubiri kuingia Gaza.

Misaada haipaswi kuwa kadi ya masharti

Akiendelea kukemea utekaji nyara, Fletcher amesisitiza kwamba Hamas lazima iwaachilia mateka wote sasa, huku akisisitiza kuwa misaada ya kibinadamu haiwezi kutumika kama chombo cha shinikizo katika mazungumzo ya kisiasa au kijeshi.

Pia Fletcher amesema “Sheria za kimataifa ziko wazi, kama nguvu inayokalia, Israel lazima iruhusu msaada wa kibinadamu kuingia Gaza,” akiongeza kuwa “Misaada inayookoa na maisha ya raia, havipaswi kamwe kuwa kadi ya masharti.”

Mapendekezo ya Israel hayafikii kiwango cha chini cha msaada

Fletcher pia amekosoa mapendekezo ya hivi karibuni kutoka kwa mamlaka za Israel, akisema hayafikii “kiwango cha chini cha msaada wa kibinadamu unaozingatia misingi ya kanuni.”

Amesisitiza msimamo wa usawa na uhuru wa harakati za misaada ya kibinadamu, na kuongeza kuwa timu za Umoja wa Mataifa ziko tayari kuokoa maisha “licha ya hatari kubwa zilizopo.”

Mvulana mdogo huko Gaza ameshika bakuli la chuma akiwa amesimama nyuma ya uzio, sehemu ya mstari wa watu wakisubiri msaada wa chakula.
UN News Mtoto wa Kipalestina huko Gaza baada ya kupokea chakula wakati wa usambazaji wa chakula katikati mwa Gaza.

Hatutakata tamaa

Katika hitimisho lenye hisia la taarifa yake Fletcher amewaomba radhi raia wa Gaza kwa kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kumaliza kizuizi hicho.

Amesema “Kwa raia waliobaki bila ulinzi, hakuna ombi la msamaha linaloweza kutosha kutimiza lengo hilo” akiongeza kuwa “Lakini kwa kweli naomba radhi kwamba tumeshindwa kuishawishi jumuiya ya kimataifa kuzuia dhuluma hii. Hatutakata tamaa, hata kama dunia imewapa kila sababu ya kukata tamaa na sisi.”

Shinikizo la kimataifa laanza kuongezeka

Taarifa hiyo inaongeza sauti katika ukosoaji unaoongezeka duniani kote dhidi ya hatua za Israel huko Gaza katikati ya janga la kibinadamu linalozidi kuongezeka.

Familia ya Kipalestina imesimama karibu na jiko lililochomwa moto katika hema lililoharibiwa katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Mawasi, Khan Younis, Ukanda wa Gaza.
© UNICEF Familia moja huko Gaza wanatazama nyumba yao iliyoharibiwa.

Makundi ya haki za binadamu yameonya kuhusu njaa, magonjwa, na kuanguka kwa mifumo ya afya katika eneo hilo lenye msongamano mkubwa.

Juhudi za kidiplomasia za kufanikisha kusitisha mapigano na kupata fursa ya upatikanaji wa misaada hadi sasa hazijazaa matunda, huku mzozo ukiendelea kuingia mwezi wa saba.