Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuongezeka kwa ghasia Darfur Kaskazini, Katibu Mkuu UN ataka hatua za haraka

Sudan. WFP inasambaza msaada wa chakula huko Omdurman, eneo la Greater Khartoum
© WFP/Abubakar Garelnabei Sudan. WFP inasambaza msaada wa chakula huko Omdurman, eneo la Greater Khartoum

Kuongezeka kwa ghasia Darfur Kaskazini, Katibu Mkuu UN ataka hatua za haraka

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameonesha wasiwasi mkubwa kuhusu kuzorota kwa hali ya kibinadamu katika Jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan, kufuatia mashambulizi ya kikatili yanayoendelea katika mji mkuu wa jimbo hilo, Al Fasher, na mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya kambi za wakimbizi wa ndani ambazo zimesababisha vifo vya mamia ya raia, wakiwemo wafanyakazi wa misaada.

Katika taarifa iliyotolewa leo Aprili 30 na msemaji wake, Stéphane Dujarric jijini New York, Katibu Mkuu ameeleza huzuni yake kuhusu hali inayoendelea kuzorota, hasa ukatili uliotokea katika kambi za wakimbizi wa ndani za Zamzam na Abu Shouk. Kambi hizi, ambazo tayari zinakabiliwa na baa la njaa na mahitaji makubwa ya misaada ya kibinadamu, zimeshambuliwa na kusababisha vifo vingi vya raia.

Zaidi ya watu 400,000 wanaripotiwa kukimbia kambi ya Zamzam mapema mwezi huu. Wengi wao sasa wamekimbilia eneo la Tawila katika Darfur Kaskazini, ambako Umoja wa Mataifa na washirika wake wa kibinadamu wanajaribu kuongeza msaada wa dharura licha ya ukosefu wa usalama na upungufu mkubwa wa fedha.

Familia ambazo zilikimbia mapigano huko Zamzam na El Fasher eneo la Darfur Kaskazini, zinatafuta hifadhi huko Tawila.
© UNICEF/Mohammed Jamal Familia ambazo zilikimbia mapigano huko Zamzam na El Fasher eneo la Darfur Kaskazini, zinatafuta hifadhi huko Tawila.

Wasiwasi

“Katibu Mkuu ana wasiwasi mkubwa kuhusu taarifa za unyanyasaji, vitisho na ukamatwaji holela wa watu waliokimbia makazi yao kwenye vituo vya ukaguzi,” amesema Dujarric. Guterres pia anasisitiza kuhusu mateso wanayopitia raia, hasa wanawake na watoto, ambao wanaripotiwa kuvuka mpaka kuingia Chad kutafuta usalama na msaada.

Hata hivyo, ghasia hazijaishia Darfur pekee. Katibu Mkuu amebainisha kuwa ukatili unaendelea katika maeneo mengine ya Sudan, ikiwemo taarifa za mauaji ya halaiki huko Omdurman katika Jimbo la Khartoum.

Mgogoro huu, ambao sasa umeingia mwaka wake wa tatu, unaendelea kuvuruga utulivu wa eneo zima. Guterres amezitaka pande zote zinazohusika kuheshimu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu, akisisitiza haja ya kutoa fursa ya haraka na isiyo na vikwazo kwa misaada ya kibinadamu, pamoja na kuwalinda raia. “Wale wote waliohusika na ukiukaji mkubwa lazima wawajibishwe,” imesema taarifa hiyo.

Umoja wa Mataifa unatoa msaada wa chakula kwa jamii ambazo zimelazimika kukimbia makazi yao.
© UNICEF/Mohammed Jamal Umoja wa Mataifa unatoa msaada wa chakula kwa jamii ambazo zimelazimika kukimbia makazi yao.

Wito

Katibu Mkuu amerudia wito wake wa kusitisha mapigano mara moja, na kuutaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na madhubuti. “mateso na uharibifu huu havipaswi kuendelea,” amesisitiza.

Mgogoro nchini Sudan unaendelea kuleta wasiwasi wa kimataifa huku mashirika ya misaada yakionya kuwa bila msaada wa haraka, hali inaweza kuzidi kuwa mbaya zaidi.