Walinda amani wa UN kutoka Bangladeshi na Indonesia wapewa medali huko DRC
Walinda amani wa UN kutoka Bangladeshi na Indonesia wapewa medali huko DRC
Huko Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, walinda amani kutoka Bangladesh na Indonesia, wanaohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO wamepatiwa medali kwa mchango wao wa ulinzi wa raia, moja ya jukumu kubwa la ujumbe huo.
Gwaride mahsusi la kuwavika medali walinda amani wa Umoja wa MAtaifa kutoka Bangladesh na Indonesia. Kofia zao za bluu, hii alama ya kuwa wanahudumia Umoja wa Mataifa.
Jenerali Urbain Ntambuka ambaye ni Kamanda wa kikosi cha 32 cha jeshi la serikali ya DRC, FARDC anasemaKwetu sisi jeshini, tunatambua mchango na kujitoa kwa wanajeshi kwa kuwapatia medali. Na kwa washirika wetu, wabangladeshi na waindonesia, tumetambua matokeo ya kazi yao sio tu katika operesheni za usalama bali pia kwenye mafunzo kwa askari wetu.
Akaenda mbali zaidi kueleza manufaa waliyopata kutoka walinda amani hawa akisema, leo hii hapa tuna zaidi ya vikosi viwili ambavyo vimefundishwa upya. Na hizi ni vitengo vinavyotoa matokeo mazuri wakiwa kwenye operesheni. Lengo letu kila wakati ni amani. Kwa mantiki hiyo tunashirikiana na MONUSCO kwenye operesheni ziwe za kijeshi au sio za kijeshi.
Video ya MONUSCO inaonesha walinda amani hao wakipeperusha bendera za nchi zao na ya Umoja wa Mataifa.
Naibu Gavana wa kijeshi hapa Ituri, Jenerali Raus Chalwe Mukuntu anasema
“Ni mchango muhimu sana kwetu kwa ajili ya kuonesha ushirikiano mzuri ulioko kati ya FARDC na MONUSCO, bila kusahau pia polisi wa kitaifa na MONUSCO ambao wana ushirikiano mzuri sana kwenye operesheni. KWa sasa jimbo linajielekeza kwenye maendeleo na ninaamini kila mtu anatambua kuwa amani ndio maendeleo.
Furaha ilikuwa bayana kwa walinda amani waliovishwa medali..