Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Papa Francis atajwa kuwa bingwa wa kimataifa wa misingi ya Umoja wa Mataifa

Katibu Mkuu UN António Guterres akizungumza kwenye jukwaa wakati wa hafla ya Mkutano Mkuu UN katika Kumbukumbu ya Mtakatifu Papa Francis, huku picha ya Papa ikionyeshwa karibu.
UN Photo/Evan Schneider Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika Kumbukumbu ya Utakatifu wake Papa Francis.

Papa Francis atajwa kuwa bingwa wa kimataifa wa misingi ya Umoja wa Mataifa

Masuala ya UM

Katika tukio la heshima katika Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo Jumanne Aprili 29, Mkuu António Guterres ametoa hotuba ya kukumbuka maisha na mchango wa Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani aliyeaga dunia tarehe 21 mwezi huu wa Aprili huko Vatican, Italia.

Tweet URL

Guterres ametoa hotuba wakati Baraza Kuu lilipokutana kwa tukio maalum la kukumbuka na kuenzi maisha ya Papa Francis, kwa kuwa alikuwa kiongozi wa Vatican yenye uanachama wa hadhi ya uangalizi kwenye Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu amemsifu kwa kujitolea kwake bila kuyumba kwa maadili ya msingi ya Umoja wa Mataifa. Kuanzia kutokomeza umaskini hadi haki kwa tabianchi na amani ya kimataifa.

Amesema “maisha ya Papa Francis aliyeongoza kanisa katoliki tangu 2013 hadi mauti yalipomkuta, yalionekana kuwa dira ya maadili kwa jamii ya kimataifa. Mjenga daraja wa imani na ubinadamu. Alikuwa mtu wa imani — na mjenga daraja kati ya imani zote."

Guterres ameongeza kuwa maono yake ya familia ya binadamu iliyoungana yalionesha matarajio ya Chata ya Umoja wa Mataifa, akikumbuka hotuba ya Papa kwa Baraza Kuu mwaka 2015 ambapo aliunga mkono wazo la Umoja wa Mataifa la "familia ya binadamu iliyoungana ikiishi kwa amani, ikifanya kazi si tu kwa ajili ya amani, bali katika amani."

Wajumbe wakisimama kimya kimya katika Mkutano Mkuu UN wakati wa kumbukumbu ya Papa Francis huko New York.
UN Photo/Evan Schneider Kabla ya kuanza kwa kikao mahsusi cha kumkumbuka Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis aliyeaga dunia Aprili 21, 2025, wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa walisimama kwa ukimya kwa dakika moja.

Mtetezi wa watu duni

Mchango wa Papa Francis kama mtetezi wa maskini na wasio na sauti ulijikita katika huduma yake ya mapema katika mitaa ya Buenos Aires nchini mwake Argentina.

Akiwa anajulikana kama "Askofu wa mitaa duni,” alileta hali halisi za umaskini kwenye jukwaa la kimataifa.

Guterres amesema Papa Francis "aliona changamoto kupitia macho ya wale walio pembezoni mwa maisha" na kusisitiza kwamba "imani lazima iwe injini ya hatua na mabadiliko."

Utetezi wake ulipanuka zaidi kivitendo mwaka 2013, alipotembelea Lampedusa kisiwa kilicho chini ya Italia katika bahari ya Mediteranea kuomboleza wahamiaji waliopotea baharini, akiweka mwangaza wa kimataifa kwenye mgogoro wa wakimbizi.

Guterres amesema katika Siku ya Wakimbizi Duniani mwaka 2024, alihimiza mataifa "kuwapokea, kuwahamasisha, kuwasindikiza na kuwajumuisha wale wanaobisha milango yetu."

Mjumbe wa matumaini katika nyakati za mgawanyiko

Katika mojawapo ya matendo yake ya mwisho, Papa Francis alitangaza mwaka 2025 kuwa "Mwaka wa matumaini," ujumbe ambao Katibu Mkuu wa UN ameihimiza dunia kuupokea. "Daima alikuwa mjumbe wa matumaini. Sasa ni juu yetu sote kuendeleza tumaini hilo," amesema Katibu Mkuu

Amegusia umoja uliodhihirika wakati wa mazishi ya Papa Francis ambapo viongozi kutoka mirengo mbalimbali ya kisiasa na kidini walikusanyika kwa mshikamano. "Dunia yetu ingekuwa mahali pazuri zaidi ikiwa tungefuata mfano wake — kwa umoja, huruma, na lengo la pamoja."

Mchango wa kudumu

Wakati UN na jamii ya kimataifa inaomboleza kifo cha Papa Francis, Guterres amesihi mataifa yote kuheshimu mchango wake kwa kuzingatia amani, haki, na heshima ya binadamu — maadili yaliyoanzisha Umoja wa Mataifa.

Soma hotuba nzima ya Katibu Mkuu hapa

Tazama video ya tukio zima hapa