Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suluhu ya amani ya mataifa mawili Gaza na Israel iko hatarini kutoweka: Guterres

Katibu Mkuu UN António Guterres akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali katika Mashariki ya Kati, ikiwemo suala la Palestina.
UN Photo/Loey Felipe Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati.

Suluhu ya amani ya mataifa mawili Gaza na Israel iko hatarini kutoweka: Guterres

Msaada wa Kibinadamu

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataita limekutana leo Mjini New York Marekani katika kikao cha ngazi ya mawaziri kujadili hali ya Mashariki ya Kati ikiwemo suala la Palestina.

Katika mkutano huo ulioongozwa na Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa ambayo ni Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Aprili Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António amesema “ahadi ya suluhisho la mataifa mawili Palestina na Israeli iko hatarini kufifia hadi kutoweka kabisa, na kwamba utashi wa kisiasa wa kufanikisha lengo hili la muda mrefu bado haujafikiwa”.

Amesisitiza kuwa amani ya kweli na endelevu katika eneo hilo inategemea swali moja kuu  kufikiwa kwa suluhisho la mataifa mawili kati ya Israeli na Palestina.

Lakini ameonya kuwa suluhisho hilo la mataifa mawili linaelekea kufikia hatua ya kutoweza kurekebishwa.

Amesisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa ina wajibu wa kuzuia uendelezaji wa uvamizi na vurugu za muda mrefu huku akizitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua zisizoweza kutenduliwa ili kufanikisha suluhisho la mataifa mawili, na kutoruhusu misimamo mikali kutoka pande zote mbili kuvuruga mabaki ya mchakato wa amani.

Kundi kubwa la watoto na watu wazima wa Kipalestina wanakusanyika wakiwa na vyungu na vyombo kupokea chakula wakati wa usambazaji wa misaada huko Gaza.
© UNRWA Watu wakipigania chakula huko Gaza.

Mashariki ya Kati inakabiliwa na mabadiliko makubwa

Guterres ameongeza kuwa Mashariki ya Kati inakabiliwa na mabadiliko makubwa, yanayoambatana na vurugu na hali ya kutoeleweka, lakini pia fursa na uwezo wa mabadiliko chanya.

Amesema watu kote katika eneo hilo wanataka mustakabali bora wanaoustahili, badala ya migogoro isiyoisha na mateso.

Amesisitiza haja ya kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha kuwa kipindi hiki cha misukosuko na mpito kinatimiza matarajio haya, na kuzaa haki, heshima, haki za binadamu, usalama, na amani ya kudumu.

Kutokana na hali hiyo, alisema, haki za Waisraeli na Wapalestina za kuishi kwa amani na usalama zimedorora, na ndoto halali za kitaifa za watu wa Palestina zimekataliwa.

Amesema hali imekuwa mbaya zaidi tangu mashambulizi ya kigaidi ya kutisha ya tarehe 7 Oktoba 2023 yaliyofanywa na Hamas, akitaja kuendelea kwa vita vikali na uharibifu huko Gaza pamoja na operesheni za kijeshi za Israeli na vurugu za walowezi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Ulimwengu hauwezi kujitia upofu huku suluhisho la mataifa mawili likitoweka,” alisema.

Wakimbizi wanapokea chakula kutoka kwa wafanyakazi wa misaada katika kituo cha usambazaji huko Gaza.
© WFP Zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa Gaza wanakabiliwa na hali mbaya ya njaa.

Misaada ya kibinadamu si jambo la kujadiliwa lazima irejee

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewaambia wajumbe wa Baraza la Usalama kuwa hakuna dalili ya mwisho wa mauaji na mateso katika Ukanda wa Gaza.

Ingawa usitishaji mapigano ulileta mwanga wa matumaini kwa kuachiwa kwa mateka na kufikishwa kwa misaada ya kibinadamu ya kuokoa maisha, “miale hiyo ya fursa ilizimwa kikatili pale makubaliano ya kusitisha mapigano yalipovunjika mnamo tarehe 18 Machi.”

Amesema hali ya kibinadamu katika ukanda huo “imebadilika kutoka mbaya ,mbaya zaidi  hadi jinamizi lisolofikirika.”

Ameongeza kuwa “Kwa takriban miezi miwili mfululizo, Israeli imezuia chakula, mafuta, dawa na bidhaa nyingine muhimu za kibiashara, ikiwanyima zaidi ya watu milioni mbili misaada ya kuokoa maisha huku dunia ikikodoa macho tu,”.

Bwana Guterres amesisitiza kuwa “misaada ya kibinadamu si jambo la kujadiliwa na kwamba Israeli lazima ilinde raia na ikubali, na kusaidia, mipango ya misaada.”

Ameitaka Israeli kuruhusu misaada kuingia Gaza mara moja. Aidha, amesisitiza kuwa usalama wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na washirika wa misaada ya kibinadamu lazima uhakikishwe, na mashirika ya Umoja wa Mataifa yaruhusiwe kufanya kazi kwa kuzingatia kikamilifu misingi ya kibinadamu ya utu, kutoegemea upande wowote, usawa na uhuru wa kiutendaji.

“Hakuna kinachopaswa kuzuia misaada ya kibinadamu  ikiwemo kazi muhimu ya UNRWA,” amesema, akilitaja shirika la Umoja wa Mataifa linalotoa msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina.

Mtazamo mpana wa mkutano wa Baraza la Usalama UN kuhusu hali katika Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na suala la Palestina, katika chumba kikubwa cha mikutano.
UN Photo/Eskinder Debebe Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lakutana kujadili hali ya Mashariki ya Kati.

Jumuiya ya kimataifa chukueni hatua

Akihitimisha hotuba yake kwenye Baraza la Usalama Guterres amerejea tena onyo kuwa suluhisho la mataifa mawili liko karibu kabisa kufikia hatua ya kutoweza kurekebishwa, na kwamba jumuiya ya kimataifa ina wajibu wa kuzuia uvamizi wa kudumu na vurugu zisizoisha

Amesema “Wito wangu kwa nchi wanachama ni wazi na wa dharura, “ Chukueni hatua zisizoweza kutenduliwa kuelekea utekelezaji wa suluhisho la mataifa mawili. Msiruhusu misimamo mikali kutoka upande wowote kuvuruga mabaki ya mchakato wa amani.”

Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa ameelekeza matumaini yake kwa mkutano wa ngazi ya Juu unaotarajiwa kufanyika mwezi Juni, ambao utaongozwa kwa pamoja na Ufaransa na Saudi Arabia, kama fursa muhimu ya kufufua uungwaji mkono wa kimataifa.

“Katika wakati huu wa mabadiliko ya kihistoria kwa watu wa Mashariki ya Kati na katika suala hili ambalo mengi yanategemea viongozi lazima wasimame na kutimiza wajibu wao,” amesema Bwana Guterres.

“Onyesheni ujasiri wa kisiasa na muonyeshe dhamira ya kisiasa ya kutimiza suluhisho hili kuu kwa ajili ya amani kwa Wapalestina, Waisraeli, eneo lote na ubinadamu kwa ujumla.”

Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Israel akihutubia Baraza la Usalama UN kuhusu hali ya Mashariki ya Kati.
UN Photo/Loey Felipe Brett Jonathan Miller, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Israeli katika Umoja wa Mataifa akihutubia Mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu Mashariki ya kati..

Israeli yasema Iran ndiyo chanzo cha machafuko Mashariki ya Kati

Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Israeli katika Umoja wa Mataifa amekaribisha mjadala kuhusu Mashariki ya Kati, akilitaja eneo hilo kuwa katika “mwendo wa mabadiliko makubwa, huku akionya kwamba vitisho vipo karibu na ni hatari zaidi kuliko wakati mwingine wowote.”

Brett Jonathan Miller amesema kuwa kuna vikundi vinavyotafuta kugeuza mwenendo wa sasa na kutumia hali ya sintofahamu kwa faida yao, vikionekana kuwa na mienendo ya vurugu inayozidi kuwa sugu.

“Tunapotazama hali ya eneo hili, kuna jambo moja linalounganisha machafuko haya yote,” amesema.
“Iran si mchochezi wa kawaida. Ni mbunifu wa machafuko katika eneo letu kupitia kundi la Hezbollah nchini Lebanon, Hamas na Islamic Jihad huko Gaza, wanamgambo nchini Iraq na Syria, na Wahouthi wa Yemen.”

Ameongeza kuwa “Iran inahusika moja kwa moja na hali ya Gaza, ambapo washirika wake Hamas wamesababisha uharibifu mkubwa kwa watu wake na kutuletea sisi hofu na ugaidi.”

Akizungumzia hali ya kibinadamu huko Gaza, Miller amesema kuwa wakati wa usitishaji mapigano, zaidi ya malori 25,000 ya misaada yaliingia katika ukanda huo, kwa msaada wa Israeli.

“Israeli inafuatilia kwa karibu hali ilivyo na inashirikiana na mashirika husika ya Umoja wa Mataifa na taasisi za kibinadamu zilizo mashinani. Tathmini yetu inaonyesha kuwa kwa sasa hakuna ushahidi wa kuwepo kwa janga la kibinadamu Gaza,” amesema.

Riyad Mansour, Mchunguzi wa Kudumu wa Nchi ya Palestina kwa UMOJA WA MATAIFA, akihutubia Baraza la Usalama kuhusu hali katika Mashariki ya Kati.
UN Photo/Eskinder Debebe Riyad Mansour, Mwangalizi wa Kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama kuhusu Mashariki ya Kati.

Palestina: Hakuna uhaba wa mabomu Gaza bali mahitaji ya msingi

Riyad Mansour, Mwangalizi wa Kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, amesema Baraza la Usalama limepitisha maazimio kadhaa yenye malengo ya wazi, kusitisha umwagaji damu, kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia wanaohitaji, kuachiliwa kwa mateka na wafungwa, kuzuia kuhamishwa kwa nguvu na unyakuzi wa ardhi, na kufanikisha suluhisho la mataifa mawili.

“Dunia iliungana kuunga mkono malengo haya, lakini hali halisi ya leo ni kwamba Israeli imetangaza mzingiro wa kisasi dhidi ya Gaza ili kuwanyima Wapalestina milioni mbili  nusu yao wakiwa watoto chakula, maji, dawa, umeme na mahitaji mengine muhimu ya Maisha.”

Ameongeza kuwa “Hakuna uhaba wa mabomu yanayoanguka Gaza, lakini kuna uhaba wa makusudi wa kila kitu kingine.”

Amesisitiza kuwa usitishaji mapigano unapaswa kurejeshwa mara moja, na kwamba malengo yote ya usitishaji huo lazima yafikiwe.

Bwana Mansour ameeleza matumaini yake kuwa Marekani, Misri na Qatar kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa wanaweza kusaidia kurejesha usitishaji mapigano na kuanza kupunguza mateso ya watu wa Gaza.

“Kuna njia ya kutoka katika jinamizi hili kwa manufaa ya wote,” amesema.
“Tunataka amani, si kwa ajili yetu tu bali kwa ajili ya wote. Tumejikita katika kuheshimu utawala wa sheria za kimataifa na tunataka zitekelezwe. Tunaamini kuwa njia ya amani ndiyo itakayoleta haki kwa watu wetu, na kwamba hakuna uhalali wowote wa kuwadhuru raia iwe ni Wapalestina au Waisraeli.”