Vikwazo vya Israel kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa Gaza vyaang’aziwa katika ICJ
Vikwazo vya Israel kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa Gaza vyaang’aziwa katika ICJ
Sheria na Kuzuia Uhalifu
Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imeanza kusikiliza mashauri leo Jumatatu AprIli 28 kuhusu vikwazo vikubwa vinavyoendelea kuwekwa na Israel dhidi ya kazi ya Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa katika Ukanda wa Gaza na Maeneo ya Palestina Yanayokaliwa (OPT).
ICJ, iliyoko The Hague, Uholanzi na kuwa mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa, inatarajiwa kusikiliza hoja kutoka kwa mataifa 40 na mashirika manne ya kimataifa katika mchakato unaotarajiwa kudumu kwa wiki nzima.
Akimwakilisha Katibu Mkuu António Guterres, Mshauri wa Kisheria wa Umoja wa Mataifa Elinor Hammarskjöld amesisitiza wito wake wa mara kwa mara wa kutaka usitishaji mapigano, misaada ya kibinadamu kuwafikia wote wanaohitaji na mateka wote kuachiliwa.
Bi. Hammarskjöld ameeleza kuwa jumla ya mashirika 13 ya Umoja wa Mataifa yako Gaza, na akaongeza kuwa wafanyakazi 295 wa Umoja wa Mataifa wamefariki katika Gaza tangu kuanza kwa vita tarehe 7 Oktoba 2023, kufuatia mashambulizi ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas kusini mwa Israel.
Maoni ya Kisheria
Mshauri huyo wa kisheria wa Umoja wa Mataifa amesisitiza juu ya ulinzi maalum na kinga ya mashirika na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, ambayo ni muhimu ili kutekeleza majukumu yao duniani kote, ikiwemo katika Eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu, OPT.
Bi. Hammarskjöld amesema kuwa ulinzi huo unahitajika hata wakati wa migogoro ya silaha, kabla ya kusisitiza wajibu wa Israel kama nguvu inayokalia maeneo hayo kwa mujibu wa sheria za kimataifa. “Wajibu mkubwa zaidi ni kuendesha maeneo hayo kwa manufaa ya wakazi wa eneo hilo na ‘kukubali na kuwezesha mipango ya misaada,’” alisema.
“Katika muktadha maalum wa hali ya sasa katika OPT, wajibu huu unamaanisha kuruhusu na kuwezesha mashirika yote husika ya UN kutekeleza shughuli zao kwa manufaa ya wakazi wa eneo hilo,” ameongeza.
Lengo la vikao vya wiki nzima katika ICJ ni kutoa kile kinachoitwa “maoni ya ushauri” kuhusu wajibu wa Israel kama nguvu inayokalia maeneo ya Gaza na OPT kwa ujumla, kwa mujibu wa Katiba ya Umoja wa Mataifa.
Hili linatokana na mkutano wa Baraza Kuu la UN mwezi Desemba ambapo nchi wanachama zilipiga kura 137 kwa 12 kuomba maoni ya majaji 15 wa ICJ, kufuatia mashambulizi ya Israel na uhaba mkubwa wa misaada kote Gaza.
Ingawa maoni ya ushauri ya majaji wa ICJ hayalazimishi kisheria – tofauti na mashauri rasmi kati ya nchi (yanayojulikana kama "mashauri ya migogoro") – yanatoa mwanga juu ya masuala ya kisheria.
Mara baada ya mahakama kutoa maoni yake, Baraza Kuu litakuwa huru kulirejea suala hilo na kuamua hatua zaidi.
Akipokea kwa furaha vikao hivyo, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa kwa wakimbizi wa Palestina (UNRWA) Philippe Lazzarini amesisitiza kuwa mashirika ya misaada yanajitahidi kukidhi mahitaji makubwa.
Kamishna Mkuu wa UNRWA alieleza kuwa sera ya Bunge la Israel inayopiga marufuku ushirikiano wowote na maafisa wa UNRWA, ambayo imelaaniwa kwa wingi, imezuia utoaji wa misaada na huduma muhimu.
Hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa UNRWA ndilo shirika kubwa la misaada Gaza, ambapo limekuwa likitoa huduma za afya, elimu na huduma nyingine muhimu kwa miongo kadhaa.
Lakini tangu vikwazo hivyo kuanza mwishoni mwa Januari, wafanyakazi wa kimataifa wa UNRWA hawajapewa viza kuingia Israel, amesema Bwana Lazzarini.
Ndani ya Gaza, hali ya kawaida kwa Wapalestina ni uhaba mkubwa wa chakula kutokana na uamuzi wa tarehe 2 Machi wa Israel kufunga kabisa mipaka ya ukanda huo.
“Leo watu hawaishi Gaza; wanaonusurika mabomu na risasi wanakufa polepole,” alisema Jonathan Whittall, Mkuu wa Ofisi ya OCHA Gaza. Alisisitiza kuwa mashirika ya misaada hayawezi kukidhi mahitaji yanayoongezeka kufuatia uamuzi wa Israel kukata bidhaa zote za kibiashara na misaada.
“Watu hapa wanabanwa pumzi,” ameongeza. “Kile tunachokiona ni mateso yasiyo na mwisho chini ya mzingiro kamili. Kufungwa kabisa kwa muda wa karibu miezi miwili huku mashambulizi ya anga, operesheni za ardhini na maagizo ya kuwahamisha watu yanaongezeka.”