UN yazindua Mtandao wa Kimataifa wa Manusura wa Ugaidi (VoTAN)
UN yazindua Mtandao wa Kimataifa wa Manusura wa Ugaidi (VoTAN)
Katika hatua muhimu ya kuchagiza mapambano ya kimataifa dhidi ya ugaidi, Umoja wa Mataifa umezindua leo Mtandao wa Mashirika ya Manusura wa Ugaidi (VoTAN), mpango mpya ambao umelenga kuimarisha sauti za manusura na kuimarisha mshikamano wa kimataifa.
Akizungumza katika tukio hilo, jijini New York, Marekani, Vladmir Voronkov ambaye ni Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kukabiliana na Ugaidi, UNOCT, ameangazia nguvu ya mabadiliko ya utetezi unaoongozwa na manusura katika kupambana na misimamo mikali.
“Katika janga lisilofikirika la kibinafsi, wengi wamechagua si tu kupona, bali pia kupaza sauti zao,” amesema Voronkov, akiwahutubia wanadiplomasia, manusura na viongozi wa kijamii.
VoTAN jukwaa la kidijitali
Amesema VoTAN imekuwa jukwaa la kidijitali la kimataifa linalounganisha mashirika ya manusura, likitoa rasilimali, mbinu bora, na fursa za ushirikiano ili kuhakikisha haki za manusura zimehifadhiwa na hadithi zao zimetumika kuboresha sera.
“Mpango huu umejengwa juu ya pendekezo kuu kutoka Mkutano wa Kimataifa wa 2022 kuhusu Manusura wa Ugaidi na umeashiria mwelekeo mpya wa mikakati ya kupambana na ugaidi inayoelekezwa na waathirika,” amesema Voronkov.
Licha ya juhudi zinazoendelea za kimataifa, ugaidi umeendelea kuua watu kila siku, huku wanawake, watoto na vijana wakiwa manusura wakuu.
Vita dhidi ya ugaidi vinahitaji hatua za kimataifa
Voronkov amesisitiza kwamba kwa kuwa tishio la ugaidi ni la kimataifa, jawabu lake pia linahitaji ushirikiano wa kimataifa, na uwe ushirikiano jumuishi. “Hakuna nchi, wala raia, aliye salama,” ameonya Mkuu huyo wa UNOCT.
Kwa msaada wa kifedha kutoka Hispania, Iraq na nchi nyingine wanachama, mtandao huu unatarajiwa kuziba mapengo ya msaada na kuinua ushuhuda wa waathirika kutoka maeneo yaliyopuuzwa duniani.
Manusura kama Grace, Joseph, na Hasan, waliotoa ushuhuda wao wakati wa uzinduzi, wamewakilisha harakati zinazokua za ustahimilivu na utetezi.
“Nguvu ya mtandao huu imekuwa katika umoja wake,” Voronkov amehitimisha na kuongeza kuwa “pamoja, tunaweza kujenga siku zijazo zisizotawaliwa na hofu, bali na haki, utu, na azimio la pamoja.”