Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNHCR atoa wito mzito kwa Baraza la Usalama kuhusu watu wanaofurushwa makwao

Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Wakimbizi UN , akiwafahamisha wajumbe wa Baraza la Usalama UN .
UN Photo/Loey Felipe Filippo Grandi Kamishina Mkuu wa wakimbizi wa Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama.

Mkuu wa UNHCR atoa wito mzito kwa Baraza la Usalama kuhusu watu wanaofurushwa makwao

Wahamiaji na Wakimbizi

"Huu ni msimu wa vita na migogoro" amesema Filippo Grandi Kamishina Mkuu wa wakimbizi wa Umoja wa Mataifa, akilihimiza leo Baraza la Usalama kurejea katika jukumu lake la kulinda raia na kudumisha amani duniani.

Katika hotuba yake ya mwisho kwa Baraza hilo, mjini New York Marekani Filippo Grandi, abaye pia ni Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, anayemaliza muda wake mwishoni mwa mwaka huu, ametoa onyo kali kuhusu kuongezeka kwa mizozo duniani, watu kufurushwa makwao kwa nguvu, na kuporomoka kwa misaada ya kibinadamu.

"Huu ni msimu wa vita. Huu ni wakati wa misukosuko," amesema Grandi , akitaja migogoro kuanzia Sudan hadi Ukraine, DRC Myanmar hadi Haiti.

Amelaani kupuuzwa kwa sheria za kimataifa za kibinadamu na akaonya kuwa “Watu milioni 123 wamelazimika kuhama makwao sasa, hii ni dalili ya wazi ya kushindwa kwa  utashi wa kisiasa kuzuia na kumesha vita, hilo ndilo jukumu lenu kuu" amewaambia wajumbe wa Baraza.

Ameongeza kuwa "Na ni jukumu ambalo, naomba mnisamehe kusema tena kwamba, Baraza hili limeshindwa kulitekeleza mara kwa mara."

Wakimbizi wapya wa Sudan wakisubiri kusajiliwa kabla ya kuhamishiwa katika Kambi ya Wakimbizi ya Karsi huko Birao katika Jamhuri ya Afrika ya Kati mnamo Desemba 12, 2024.
© UNFPA/Karel Prinsloo Wakimbizi kutoka Sudan wanakusanyika katika kambi ya wakimbizi ya Korsi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, mwaka 2024.

Janga la wakimbizi Sudan: Hofu huachwa mpakani

Grandi ameeleza simulizi za kusikitisha za wakimbizi wa Sudan "Kuvuka mpaka kulimaanisha kuipa kisogo hofu."

Akielezea janga la kibinadamu Sudan, Grandi amesema mtu mmoja kati ya watatu Sudan amefurushwa kutoka nyumbani kwake kutokana na vurugu zinazoendelea "zisizofafanulika kwa maneno."

Katika ziara yake nchini Chad, alikutana na wanawake na watoto waliokimbia mashambulizi Darfur.

Amesema "Waliripoti vitendo vya kutisha, lakini zaidi ya yote, waliwasilisha hofu ya Kuvuka mpaka, licha ya mateso yote waliyojua wangekutana nayo, lakini hilo lilimaanisha kuiacha hofu nyuma."

Grandi amesisitiza kuwa, huku nchi kama Chad na Sudan Kusini zikifungua mipaka yao licha ya changamoto kubwa walizonazo, msaada wa kibinadamu haukidhi mahitaji.

"Ombi la msaada kwa wakimbizi wa kanda hii limefadhiliwa kwa asilimia 11 pekee," amelalamika, akionya kuwa kutelekeza mataifa yanayopokea wakimbizi kutazidisha ukosefu wa utulivu wa kikanda.

The referenced media source is missing and needs to be re-embedded.

DRC: Migogoro inayoendelea na athari kwa wakimbizi

Ingawa Grandi hakuzungumzia kwa kina hali ya DRC katika hotuba yake ya ya leo ameelezea wasiwasi wake kuhusu migogoro inayoendelea Mashariki mwa nchi hiyo, hususan katika maeneo ya Kivu.

Amesisitiza kuwa ukosefu wa utii kwa sheria za kimataifa za kibinadamu na ukiukwaji wa haki za binadamu vimesababisha watu wengi kukimbia makazi yao kwa hofu.

Ameongeza kuwa, "Mapigano ya ukatili, ukiukwaji wa haki za binadamu, ukatili wa kijinsia ukiwemo ukatili wa kingono  vimewalazimu raia kukimbia kwa hofu."

Maelfu ya wakimbizi Ukraine wanahitaji haki ya amani

Grandi ameonya kwamba endapo "Minong’ono ya mashambulizi haitokoma Ukraine, na usalama kuhakikishwa, watu hawatakuwa tayari kurejea".

Akiangazia Ukraine, Grandi ameelezea mnepo wa raia waliopoteza makazi yao licha ya mashambulizi yasiyokoma, lakini akasisitiza kuwa ni amani ya kudumu pekee itakayowawezesha zaidi ya watu milioni 10 waliotawanywa kuanza upya maisha yao.

"Bila kukomesha mashambulizi kabisa, na watu kupata makazi bora, huduma na kazi hawatakuwa tayari kurejea."

Grandi amewataka wote wanaohusika katika mazungumzo ya amani kuzingatia hali ya familia zilizotawanywa, akionya kuwa suluhisho lazima lijengwe juu ya usalama wa muda mfupi na wa muda mrefu.

Mtu aliyekimbia makazi yake nchini Myanmar akikusanya vitu vya dharura kutoka kwenye rundo la masanduku kwenye makazi baada ya tetemeko la ardhi.
United Nations UNHCR inawasaidia wakimbizi wa ndani katika Chan Thar Kone baada ya tetemeko kubwa la ardhi lililoikumba Myanmar. (Maktaba)

Myanmar ni changamoto kubwa hatua madhubuti zahitajika

Katika taarigfa yake kwa Baraza hilo la Usalama kuhusu Myanmar Grandi amekiri kuwa ni changamoto kubwa lakini amehimiza mazungumzo mapya.

"Ni jambo la hatari, lakini ni lazima kuchukua hatua," amelihimiza Baraza kuunga mkono juhudi mpya za mazungumzo kwa ajili ya kuvunja "miaka minane ya mkwamo" ambayo imewaacha wakimbizi wa Rohingya milioni 1.2 wakihangaika makambini.

Amesema "Nusu ya wakimbizi ni watoto chini ya umri wa miaka 18, wamepokonywa fursa lakini wameunganishwa na dunia kupitia mtandao," Amelionya hilo akielezea hatari ya kuongezeka kwa misimamo mikali nchini humo.

Amesisitiza kuwa, licha ya changamoto, "mazungumzo na pande zote ni hatua ya kwanza muhimu" kwa kurejesha msaada wa kibinadamu kwa usalama.

Syria: Mwanga wa matumaini katikati ya magofu

Grandi ameliambia Baraza la Usalama kwamba “Kwa mara ya kwanza katika miongo kadhaa, kuna mwangaza wa matumaini kwa Wasyria waliotawanywa."

Kwa nadra, Grandi amegusia dalili za matumaini kuhusu Syria, akielezea kuwa watu waliolazimika kuhama makwao wameanza kurejea polepole tangu Desemba mwaka jana.

"Tangu Disemba 8, idadi ya wale wanaorejea imekuwa ikiongezeka polepole lakini kwa uthabiti," amesema.

Hata hivyo, amehimiza Baraza la Usalama kuchukua hatua za kutathimini na kupunguza hatari kama kulegeza vikwazo, kusaidia ujenzi wa awali, na kuhakikisha huduma za msingi zinapatikana.

Ameonya kwamba "Ni lazima mtangulize maslahi ya watu wa Syria kuliko siasa za zamani zisizo na maana tena".

Mwonekano mpana wa chumba cha Baraza la Usalama UMOJA WA MATAIFA huku wajumbe wakiwa wameketi kuzunguka meza kuu, huku Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Wakimbizi UN , akitoa taarifa fupi.
UN Photo/Manuel Elías Mtazamo mpana wa mkutano wa Baraza la Usalama ukisikiliza hotuba ya Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi.

Wito wa mwisho: Misaada ni msingi wa utulivu

Katika ujumbe wake wa kuaga, Grandi anayetarajiwa kumaliza muhula wake 31 Desemba mwaka huu wa 2025 ameonya kwamba "Kupunguza misaada tayari kunakatili maisha."

Ametoa wito wa kuzuia kupungua kwa msaada wa kimataifa na kuporomoka kwa mshikamano wa kimataifa.

Amesisitiza kuwa "Misaada ni utulivu. Kusitisha au kupunguza bajeti za misaada ya kibinadamu kunamaanisha kuwaacha watu waliotawanywa bila pa kutegemea na kudhoofisha utulivu wenu wenyewe."

Amewakumbusha wajumbe wa Baraza kuwa watu kufurushwa makwao ni sehemu ya historia za mataifa yote yaliyopo mezani. "Mmekuwa wakimbizi. Mmehifadhi wakimbizi," amesema. "Sasa mnaketi hapa na jukumu la kumaliza vita, na kuleta amani. Lazima mfanikiwe. Mnadeni kwa wakimbizi, lakini pia kwa nafsi zenu."