Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vikwazo vya biashara, madeni vyaongezeka na vinadhoofisha SDGs– Guterres

Mizigo ya usafirishaji wa barabarani ikichakatwa katika bandari ya Addis Ababa, Ethiopia. (Maktaba)
UNCTAD/Abrham Grizaw
Mizigo ya usafirishaji wa barabarani ikichakatwa katika bandari ya Addis Ababa, Ethiopia. (Maktaba)

Vikwazo vya biashara, madeni vyaongezeka na vinadhoofisha SDGs– Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katika Jukwaa la Baraza la Kiuchumi na Maendeleo la Umoja wa Mataifa, ECOSOC kuhusu ufuatiliaji wa Ufadhili kwa Maendeleo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameonya kuhusu tishio linaloongezeka la vita vya kibiashara na madhara yake kwa ufadhili kwa ajili ya maendeleo duniani—hasa kwa mataifa yaliyo hatarini zaidi kiuchumi.

Akizungumza jijini New York, Marekani hii leo kabla ya Mkutano wa Nne wa Kimataifa kuhusu Ufadhili kwa Maendeleo utakaofanyika Sevilla, nchini Hispani kuanzia Juni 30 hadi Julai 3, 2025, Guterres ameelezea hali ya wasiwasi kuhusu mgawanyiko wa kiuchumi na mzigo wa madeni unaoongezeka, ambavyo amesema vinazidi kuzuia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs.

“Angalia tu vita vya biashara,” amesema Guterres. “Vikwazo vya kibiashara ni tishio la wazi na la sasa kwa uchumi wa dunia na maendeleo endelevu… Katika vita vya biashara, kila mtu anapoteza—hasa mataifa na watu walio hatarini zaidi.”

Udhibiti wa kibiashara unatishia mshikamano wa dunia

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa ongezeko la sera za udhibiti wa masoko na migogoro ya kibiashara kunachangia kusambaratika kwa mshikamano wa kiuchumi duniani.

Kwa mujibu wa makadirio ya taasisi kama Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Shirika la Biashara Duniani (WTO), kuongezeka kwa vikwazo vya biashara kunasababisha kushuka kwa kasi kwa ukuaji wa uchumi wa dunia—mwelekeo ambao unawaathiri zaidi nchi zinazoendelea.

Guterres amesisitiza kuwa biashara iliyo wazi, ya haki, na inayozingatia sheria ndiyo msingi wa maendeleo endelevu. Bila hilo, nchi zinazoendelea zinakumbwa na hali ya kutotabirika, upatikanaji mdogo wa masoko, na kucheleweshwa kwa urejesho wa uchumi.

Mzozo wa madeni: Adui badala ya chombo cha maendeleo

Zaidi ya biashara, Guterres ameangazia mzigo wa deni unaoongezeka kwa kasi katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.

Ulipaji wa madeni katika nchi zinazoendelea sasa unazidi dola trilioni 1.4 kwa mwaka, na hutumia zaidi ya asilimia 10 ya mapato ya serikali katika zaidi ya mataifa 50—na zaidi ya asilimia 20 katika mataifa 17.

“Deni linapotumiwa kwa busara na kwa haki, linaweza kuwa mshirika wa maendeleo,” ameeleza Guterres. “Badala yake, limekuwa adui.”

Ameitaka jumuiya ya kimataifa kupitisha hatua madhubuti kwenye mkutano wa Sevilla, zikiwemo kupunguza gharama za ukopaji, kufanya mageuzi katika mifumo ya marekebisho ya madeni, na kupanua wigo nchi masikini zinazoweza kunufaika na mpango wa kundi la nchi 20 zenye uchumi mkubwa zaidi duniani, G20 wa kuangalia upya madeni na ikiwezekana kuyafuta.

Guterres ametaka pia tathmini mpya za viwango vya ukopaji na uzingatiaji wa SDGs, na madhara ya mabadiliko ya tabainchi pale tathmini ya madeni inapofanyika.

Mageuzi ya taasisi za fedha za kimataifa

Guterres amependekeza kuongeza kwa kiwango kikubwa majukumu ya benki za maendeleo za kimataifa, ambazo amezitaja kama "injini" za ufadhili wa kimataifa. Ametaka uwezo wao wa kukopesha uongezeke mara tatu, na usimamizi wao uwe jumuishi zaidi ili kuhakikisha fedha zinafika mahali panapohitajika zaidi.

Amesisitiza hitaji la kuongeza ufadhili wa masharti nafuu, ushiriki wa sekta binafsi, na suluhu bunifu za ufadhili kwa ajili ya malengo ya hali ya hewa na maendeleo.

Wito wa kuchukua hatua kabla ya mkutano wa Sevilla

Kwa kuwa imesalia miaka mitano pekee kufikia ukomo wa SDGs mwaka 2030, Katibu Mkuu amesisitiza kuwa mkutano wa Sevilla unapaswa kutoa matokeo ya mabadiliko makubwa. Haya yanajumuisha ahadi za msukumo wa uwekezaji kwa ajili ya SDGs, mageuzi ya mfumo wa kifedha wa kimataifa, na uwajibikaji wa jinsi matumizi ya kijeshi yanaweza kuelekezwa kwenye maendeleo.

“Hiki ni kipindi cha maamuzi muhimu,” Guterres amehitimisha. “Hatma ya ushirikiano wa kimataifa unategemea uwezo wetu wa kufadhili maendeleo. Tuchukue hatua—kwa ajili ya watu, na kwa ajili ya sayari dunia.”

Vipengele muhimu kutoka kwa Rais wa Baraza Kuu la UN Balozi Philemon Yang

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Balozi Philemon Yang, ametumia hotuba yake kutoa wito kwa mageuzi makubwa ya mfumo wa kifedha wa kimataifa ili kufanikisha malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs ifikapo mwaka 2030.

  1. Mageuzi ya mfumo wa kifedha wa kimataifa:
    Kuharakisha mageuzi ya kina ili kuwezesha mataifa yote, hasa yanayoendelea, kupata mitaji kwa urahisi na kwa gharama nafuu.
  2. Kuimarisha ufadhili kwa maendeleo:
    Kusaka suluhisho la haraka kufunga pengo la ufadhili la kila mwaka, ambalo limefikia dola trilioni 4.2, ili kutimiza Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030.
  3. Kupunguza mtego wa madeni:
    Kushughulikia mzigo wa madeni kwa mataifa ambayo yanatumia sehemu kubwa ya mapato yao kulipia madeni badala ya kuwekeza katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
  4. Kukuza biashara ya kimataifa:
    Kuondoa vikwazo vya kibiashara na mvutano wa kibiashara duniani, ambavyo vinaathiri vibaya ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa mataifa mengi.
  5. Kuhamasisha ushirikiano wa kimataifa:
    Kushirikiana kwa karibu kati ya nchi, sekta binafsi, na taasisi za kifedha ili kuongeza uwekezaji na misaada rasmi ya maendeleo kwa nchi zinazoendelea.
  6. Kutekeleza ahadi za Addis Ababa na Mkataba wa Zama Zijazo:
    Kurejea na kuimarisha utekelezaji wa makubaliano ya awali kuhusu ufadhili wa maendeleo na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.