Ni miaka 39 tangu janga la nyuklia la Chernobyl tusilisahau asilani: Schmale
Amani na Usalama
“Asilani tusisahau kilichotokea Chernobyl,” amesema Matthias Schmale, Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine.
Leo dunia ikiadhimisha kumbukumbu ya miaka 39 tangu utokea janga la nyuklia la Chernobyl, Matthias Schmale, ametoa wito wa kutafakari upya na kuchukua hatua za dharura dhidi ya vitisho vya sasa vya nyuklia.
“Madhara bado yapo hadi leo,” amesema Schmale katika taarifa yake kuhusu siku hii iliyotolewa mjini Kyiv Ukraine na kuongeza kuwa “tunapokumbuka familia zilizopoteza wapendwa wao, afya zao na makazi yao tuzingatie hilo.”
Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya Janga la nyuklia la Chernobyl inaendelea kuwa kumbusho la huzuni la athari za muda mrefu za moja ya maafa makubwa ya nyuklia duniani.
Alichokishuhudia alipotembelea Chernobyl
Schmale alitembelea hivi karibuni kinu cha nyuklia cha Chernobyl na mji ulioachwa wa Prypiat, akielezea hali aliyoshuhudia kuwa ya kusikitisha.
“Ni vigumu kuelezea hisia za kusimama mahali ambapo maisha yalikuwa yakichanua, shule, nyumba, bustani na sasa kimya kimetawala,” amesema.
Hata hivyo, kati ya ukimya huo, Schmale aliona watu walioko mstari wa mbele wakijitahidi kudhibiti athari za muda mrefu za janga hilo.
“Nimekutana na watu wanaofanya kazi kwa bidii kusaidia kudhibiti matokeo ya janga hili. Hatuwezi kusahau kazi yao ya thamani, inayotuweka salama.”
Vitisho vipya katika wakati wa vita
Schmale ameeleza pia tukio la hivi karibuni la Februari 2025, ambapo ndege isiyo na rubani ya Urusi iliharibu kifuniko cha kinga katika eneo la Chernobyl, na kusababisha moto ulioamsha hofu mpya ya mionzi.
“Hii ilikuwa kazi ya pamoja ya kimataifa ya kulinda ubinadamu,” ameeleza akiongeza kuwa “Uharibifu wake ni tishio lisilosemeka katika vita ambavyo tayari ni vya kutisha.”
Wito wa uwajibikaji wa kimataifa
Akihitimisha taarifa yake, Schmale almeoa onyo kali na wito wa hatua za kimataifa.
“Ni lazima tusisitize kuwa shughuli za kijeshi karibu na vituo vya nyuklia zikomeshwe na zisiwepo tena.”
Amesisisitiza kuhusu msaada unaoendelea wa Umoja wa Mataifa katika kulinda kkinu cha Chornobyl dhidi ya hatari zaidi.
“Janga la Chernobyl ni onyo kwetu sote,” almesema na kuhitimisha taarifa yake kwa wito kwa jumuiya ya kimataifa kulinda usalama wa nyuklia katikati ya hali tete ya kisiasa duniani.