Bendera ya Syria yenye nyota tatu yapandishwa UN, Baraza la Usalama laijadili Syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Asaad Al-Shaibani, akiinua bendera mpya ya nchi hiyo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.
Bendera ya Syria yenye nyota tatu yapandishwa UN, Baraza la Usalama laijadili Syria
Amani na Usalama
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Geir Pedersen, amesisitiza umuhimu wa kuunga mkono mchakato wa mpito wa kisiasa nchini Syria, akibainisha kuwa hali bado ni tete sana licha ya maendeleo ya hivi karibuni.
Ameyaeleza hayo wakati wa kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo Aprili 25 wakati wa kujadili hali nchini Syria, kikao ambacho kwa mara ya kwanza kilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Asaad Al-Shibani (mamlaka za mpito).
Kabla ya kikao hicho na mabalozi kadhaa pamoja na mjumbe wa Umoja wa Mataifa Geir Pedersen, Al-Shibani ameshuhudia kupandishwa kwa bendera ya Syria yenye nyota tatu miongoni mwa bendera za nchi wanachama katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.
Umoja wa Mataifa watoa wito wa kuungwa mkono kwa mpito wa kisiasa Syria
Geir Pedersen, amesisitiza umuhimu wa kuunga mkono mchakato wa mpito wa kisiasa nchini Syria. Amesema ushiriki wa Waziri wa Syria, Al-Shibani, katika kikao cha leo cha Baraza la Usalama unaonesha maendeleo makubwa ambayo Syria imepata katika miezi ya hivi karibuni. Ameeleza kuthamini kwake kwa kujitolea kwa waziri huyo katika kuimarisha utulivu wa kikanda na ushirikiano wa kujenga katika ngazi ya kimataifa.
Mwanamke akiwa ameshikilia bendera mpya ya Syria nje ya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani wakati wa tukio la kuipandisha kwa mara ya kwanza kwenye eneo hilo.
Ni miezi minne na nusu pekee tangu kuanguka kwa utawala wa zamani, jambo ambalo linaashiria mwanzo wa sura mpya katika historia ya Syria. Pedersen amesema kuwa mengi yamefanyika ambayo yanastahili kupongezwa na kuungwa mkono, "lakini changamoto bado ni kubwa, na hali bado ni tete sana. Kuna haja ya ushirikishwaji zaidi wa kisiasa na kazi zaidi katika nyanja ya kiuchumi."
Geir Pedersen, Mjumbe Maalum wa UN kwa Syria akihutubia Baraza la Usalama la UN lililokutana 25 Aprili 2025 kujadili Syria.
Ameeleza kuwa kwa mabadiliko makubwa katika maeneo hayo mawili, mchakato wa mpito wa kisiasa Syria unaweza kufanikiwa. "Bila hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa kushindwa, jambo ambalo linaweza kuleta athari mbaya."
Hatari ya matumaini kufifia
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kibinadamu, Joyce Msuya, amesema kuwa changamoto tata zinazoikumba Syria zinatokea katikati ya "moja ya migogoro mikubwa ya kibinadamu duniani," ambapo takriban robo tatu ya wakazi wake wanakumbwa na umaskini, zaidi ya nusu wanakabiliwa na uhaba wa chakula, na takribani watu milioni saba bado hawana makazi ndani ya nchi.
Akipongeza kupungua kwa mapigano, Bi. Msuya amesisitiza haja ya kuzingatia "kupunguza migogoro iliyobaki na kuhakikisha ulinzi wa raia pamoja na miundombinu ya kiraia."
Joyce Msuya, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, OCHA akihutubia Baraza la Usalama lililokutana 25 Aprili 2025 kujadili hali ya Syria.
Amesema kuwa hali ya usalama iliyoboreshwa katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Aleppo na kaskazini mashariki mwa Syria katika wiki za hivi karibuni—kufuatia makubaliano kati ya mamlaka za mpito na Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria—imeleta manufaa dhahiri kwa raia, ikiwa ni pamoja na kazi inayofanywa na UNICEF na washirika wengine katika kupanua upatikanaji wa nishati kutoka Bwawa la Tishrin.
Hata hivyo, amebainisha kuwa ripoti za matukio yanayowaathiri raia katika maeneo ya pwani bado zinaendelea kuripotiwa, licha ya kuboreshwa kwa hali ya usalama huko, na kwamba mashambulizi ya anga ya Israel na uvamizi katika mikoa ya kusini bado yanaendelea, na yamesababisha vifo vya raia katika baadhi ya matukio.