Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fahamu kuhusu Hakibunifu

Majalada ya hakimiliki ya kimataifa (IP) ya Hatimiliki, Alama ya Biashara (Trademark) na miundo ya hakibunifu yalifikia viwango vipya vya juu mnamo 2021, yakionyesha uthabiti wa mfumo ikolojia wa ulimwengu wa uvumbuzi wakati wa janga la COVID-19.
WIPO
Majalada ya hakimiliki ya kimataifa (IP) ya Hatimiliki, Alama ya Biashara (Trademark) na miundo ya hakibunifu yalifikia viwango vipya vya juu mnamo 2021, yakionyesha uthabiti wa mfumo ikolojia wa ulimwengu wa uvumbuzi wakati wa janga la COVID-19.

Fahamu kuhusu Hakibunifu

Utamaduni na Elimu

Mwaka 2000, nchi wanachama wa WIPO (Shirika la Umoja wa Mataifa la Hakibunifu) waliteua tarehe 26 Aprili – siku ambayo Mkataba wa WIPO ulianza kutumika mwaka 1970 – kuwa Siku ya Kimataifa ya Hakibunifu kwa lengo la kuongeza uelewa wa jumla kuhusu haki hizo.

Tangu wakati huo, Siku ya Kimataifa ya Hakibunifu imekuwa fursa ya kipekee ya kusherehekea michango ya wavumbuzi na wabunifu duniani kote na kuchunguza jinsi Hakibunifu inavyosaidia katika ustawi wa muziki, sanaa na ubunifu wa kiteknolojia unaounda dunia yetu.

Siku hii pia inasisitiza umuhimu wa mfumo wa Hakibunifu ulio na uwiano, unaotambua na kuthamini kazi za wavumbuzi na wabunifu huku ukihakikisha jamii inanufaika kutokana na ubunifu na akili zao. Haki za miliki huwezesha watafiti, wavumbuzi, wafanyabiashara, wabunifu, wasanii na wengine kulinda kisheria matokeo ya ubunifu wao na kupata faida ya kiuchumi kutokana nayo.

Kaulimbiu ya Siku ya Kimataifa ya Hakibunifu kwa mwaka 2025 ni "Hakibunifu na Muziki: Sikiliza midundo ya Hakibunifu".

Muziki ni njia ya uelezaji ya ubunifu iliyo ya kipekee na ya ulimwenguni kote, lugha ya sauti inayovuka mipaka na tamaduni, ikigusa mioyo, kuchochea fikra na kuhamasisha watu kuchukua hatua. Hata pale ambapo hatufikirii kwa makusudi, midundo na marudio ya muziki huwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Muziki hutuweka pamoja, huchochea hatua, huamsha hisia za ndani na kuchangia mabadiliko tunayoyataka kuona duniani.

Siku ya Kimataifa ya Hakibunifu
WIPO
Siku ya Kimataifa ya Hakibunifu

Siku ya Kimataifa ya Hakibunifu 2025 inaangazia wabunifu, wavumbuzi na wajasiriamali wanaovuka mipaka ya ubunifu na uvumbuzi ili kuleta mawazo mapya katika ulimwengu wa muziki, na jinsi Hakibunifu zinavyosaidia kuendeleza mazingira yenye muziki hai, tofauti na yenye manufaa kwa kila mtu, kila mahali.

Kusoma zaidi bofya hapa

Kampeni ya mwaka huu ni fursa ya kuhamasisha vizazi vijavyo vya wabunifu, wavumbuzi na wajasiriamali kuendelea kuleta mawazo mapya na ya kusisimua katika ulimwengu wa muziki ambayo yanatajirisha maisha yetu.

Hakibunifu ni nini?

Hakibunifu ni mali au haki inayotokana na ubunifu wa akili ya binadamu, ambayo hulindwa kisheria ili kumpa mbunifu haki ya kipekee ya kuitumia kwa muda fulani. Hii inahusisha mambo kama:

Uvumbuzi (hulindwa kwa kupitia hataza/patenti)

Kazi za fasihi na sanaa (hulindwa kwa hakimiliki)

Miundo (hulindwa kwa haki za ubunifu wa miundo)

Alama, majina na picha zinazotumika kibiashara (hulindwa kwa alama ya biashara)

Nchi wanachama wa WIPO zilipitisha mkataba mpya wa haki miliki, rasilimali za kijeni na maarifa ya jadi yanayohusiana nayo.
© WIPO/Emmanuel Berrod
Nchi wanachama wa WIPO zilipitisha mkataba mpya wa haki miliki, rasilimali za kijeni na maarifa ya jadi yanayohusiana nayo.

Aina kuu za Hakibunifu:

1. Hakimiliki – Hulinda kazi asilia za ubunifu kama vitabu, muziki, filamu, programu za kompyuta na sanaa.

2. Hatimiliki (Patent) – Hutoa ulinzi kwa uvumbuzi mpya au mbinu mpya, kumpa mvumbuzi haki ya kipekee kwa muda maalum (mara nyingi miaka 20).

3. Alama ya Biashara (Trademark) – Hulinda vitu vinavyotambulisha chapa kama majina ya biashara, kaulimbiu, na nembo.

4. Siri za Biashara (Trade Secrets) – Hulinda taarifa za kibiashara ambazo ni siri na zinampa mmiliki faida ya kiushindani, kama vile mapishi au mbinu za uzalishaji.

5. Ubunifu wa Kiwandani (Industrial Design) – Hulinda muundo wa nje wa bidhaa, kama vile umbo la chupa au simu.