Sudan: WFP yachukua hatua kuwasaidia raia walionaswa katika mapigano Darfur
Sudan: WFP yachukua hatua kuwasaidia raia walionaswa katika mapigano Darfur
Maelfu ya watu wamefungasha virago na kukimbia mapigano huku njaa ikitishia maisha yao limesema leo Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakua duniani WFP.
Shirika hilo limesema katika taarifayake iliyotolewa leo mjini Khartoum kwamba limeanzisha harakati za dharura kupeleka msaada wa chakula kwa maelfu ya raia waliokwama kutokana na mapigano yanayoendelea katika maeneo ya Darfur, magharibi mwa Sudan.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo mpya, mapigano bado yanaendelea katika maeneo yaliyohusishwa na kuzingirwa, hali inayozidi kuhatarisha maisha ya watu waliokwishaathiriwa na ukosefu mkubwa wa chakula.
Takwimu za kushtua kutoka mashinani
Ripoti kutoka kwa maafisa wa shirika hilo mashinani zinaeleza hali ya kutisha, takriban watu 450,000 waliokuwa tayari wakikumbwa na baa la njaa na ukatili wa hali ya juu wamelazimika kukimbia makambi ya El Fasher na Zamzam katika kipindi kifupi cha wiki chache. Hali hii imeongeza kiwango cha maafa kwa jamii ambazo tayari zilikuwa hatarini.
Samatha Chattaraj, Mratibu wa Dharura wa WFP kwa Sudan, akizungumza kutoka Port Sudan katika mkutano wa kawaida wa waandishi wa habari wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva amesema "Tunafikia watu waliokimbilia maeneo salama. Tunaandaa misaada kuwafikia watu pale walipojikuta wamelazimika kukimbilia katika maeneo mbalimbali ya Darfur na Jimbo la Kaskazini.”
Mashirika ya kibinadamu chini ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kuwepo kwa wingi katika maeneo yaliyoathiriwa, yakijaribu kutoa misaada ya chakula, huduma za afya na misaada mingine muhimu licha ya mazingira hatarishi na vikwazo vya kiusalama.
WFP imeeleza kuwa jitihada za kufikisha misaada zinahitaji usaidizi wa haraka ili kuzuia janga la kibinadamu kushamiri zaidi.
WFP na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa yanatoa wito kwa jamii ya kimataifa na pande zinazohusika na mgogoro kuhakikisha upatikanaji salama wa misaada kwa raia waliokwama.
Pamoja na kutathmini mahitaji kila siku, juhudi zaidi zinahitajika kuzuia baa la njaa na kulinda maisha ya watu wanaoishi katika hali ya hatari ya kupoteza maisha limesisitiza shirika hilo.
Kuongezeka kwa mapigano
Kwa miaka miwili iliyopita, wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) wakiongozwa na Jenerali Mohamed Hamdane Daglo wamekuwa vitani na jeshi la serikali ya Sudan SAF linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhane. Mapigano yamezidi kuwa makali katika wiki za hivi karibuni karibu na mji wa El Fasher unzozingirwa, ambao ni mji mkuu wa Darfur Kaskazini.
Kwa mujibu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa lenye makao yake Roma Italia, “idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao hivi karibuni wamekwama katika miji ya El Fasher au Zamzam kwa miezi kadhaa kutokana na mzozo huo. "
WFP inafanya kila liwezekanalo kuwasaidia watu, hata wakati huu wa ongezeko la ghasia,"amesema Chattaraj.
Mwezi uliopita, watu 270,000 walioko El Fasher na Zamzam walipokea msaada kutoka WFP.
Wakati huohuo, malori yaliyobeba tani 1,600 za chakula na virutubisho kutoka WFP kwa ajili ya watu 220,000 yameanza kufika Tawila Darfur Kaskazini, ambako watu 180,000 waliokimbia El Fasher na kambi za Zamzam wamewasili katika kipindi cha wiki moja tu iliyopita.
"Msafara mwingine wa WFP kutoka Port Sudan uko njiani kuelekea El Fasher tunapozungumza sasa, ukiwa na tani 1,000 za msaada kwa takriban watu 100,000 ambao bado wamekwama katika mji huo uliozingirwa," amesema afisa huyo wa Umoja wa Mataifa.
Hali ni ya kusikitisha sana Khartoum
WFP pia imeanza kusambaza chakula kwa watu 100,000 katika eneo la Jabal Awlia, "eneo lililo kusini mwa Khartoum ambalo linakabiliwa sana na tishio la njaa."
Malori ya msaada yalifika wiki iliyopita, na huo ni msaada wa kwanza kufika Jabal Awlia tangu Desemba mwaka jana.
Misaada zaidi inatarajiwa kuwasilishwa katika eneo kubwa la Khartoum katika wiki zijazo, huku WFP ikifanya kazi kuanzisha "misingi imara ya uendeshaji itakayowezesha usambazaji wa mara kwa mara katika mji mkuu."
Afisa wa WFP ambaye amerudi hivi karibuni kutoka katika ziara ya kikazi mjini Khartoum mwanzoni mwa wiki hii amesema kuwa “ameshuhudia hali ya kusikitisha sana."
Maeneo makubwa ya jiji hilo yameharibiwa. Kiwango cha njaa na kukata tamaa ni cha juu sana, lakini watu bado wana matumaini.
"Tunatarajia kwamba watu wengi watajaribu kurudi nyumbani katika miezi ijayo. Lakini mahitaji yao ya msingi, ikiwemo chakula, ni lazima yatimizwe," amesisitiza Bi. Chattaraj.
WFP inalenga kuwafikia watu milioni 7 ifikapo mwezi Juni
Kwa ujumla, WFP iliwasaidia watu milioni 4 nchini Sudan mwezi Machi idadi ya juu zaidi kwa mwezi mmoja tangu mzozo uanze Aprili 2023, na karibu mara nne ya idadi ya watu waliopokea msaada kwa mwezi katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Hii inajumuisha watu milioni 1.6 walioko katika maeneo yaliyoainishwa kuwa katika hali ya njaa au hatarini kuingia kwenye baa la njaa.
"Tumewasaidia watu wanne kati ya watano walio katika viwango vya juu kabisa vya njaa katika maeneo yote 27 yanayokabiliwa na njaa au hatari ya njaa," amesema Chattaraj, akibainisha kuwa karibu watu milioni 25, sawa na nusu ya idadi ya watu nchini humo, wanakabiliwa na njaa kali.
Pia amesema karibu watoto milioni 5 na akina mama wanaonyonyesha wanakabiliwa na utapiamlo mkali. Sudan pia ndiyo nchi pekee duniani kwa sasa ambako baa la njaa limethibitishwa rasmi.
Lengo la WFP ni kuwafikia watu milioni 7 kufikia Juni mwaka huu, kwa kuzingatia hasa maeneo yaliyoainishwa kuwa hatarini kukumbwa na njaa au yaliyo katika hali ya njaa, pamoja na maeneo yenye viwango vya juu vya utapiamlo.
Ili kufanikisha hili, WFP inasisitiza umuhimu wa upatikanaji endelevu wa misaada ya kibinadamu na ufadhili wa ziada ili kukidhi mahitaji ya watu wa Sudan.