Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakibunifu: Uelewa bado ni mdogo lakini ni jambo muhimu sana ulimwenguni – Wakili Joshua Msambila

Siku ya Kimataifa ya Hakibunifu
WIPO Siku ya Kimataifa ya Hakibunifu

Hakibunifu: Uelewa bado ni mdogo lakini ni jambo muhimu sana ulimwenguni – Wakili Joshua Msambila

Na Anold Kayanda - New York, Marekani
Utamaduni na Elimu

Aprili 26 ni Siku ya Kimataifa ya Hakibunifu - siku ambayo ni fursa kwa ulimwengu kukumbushwa umuhimu wa haki kwa watu wanaobuni mambo mbalimbali duniani. Ili kufahamu zaidi kuhusu Hakibunifu tumezungumza na mtaalamu wa Sheria za Sanaa na Hakimiliki, Wakili Joshua Msambila wa nchini Tanzania, kwanza anaeleza kilichomsukuma yeye kujikita katika eneo hili la sheria.

“Kilichonisukuma hasa katika mawanda mapana ya taaluma ya sheria na kuamua kujikita na masuala ya Hakibunifu ni kwamba nimegundua nchi yetu ina wabunifu wengi na wanafanya kazi za kipekee na mataifa ya nje yenye uelewa mkubwa kuhusu Hakibunifu yananufaika sana.” 

Sikiliza kwa kina hapa:

Audio file

 Anaeleza mwanasheria Joshua Msambila akiongeza kwamba, “kama watu wetu ambao ni wabunifu wangefahamu hii ingewasaidia katika kujikomboa katika umaskini kwasababu kazi za kibunifu zina thamani kubwa na zinaweza zikamsaidia mbunifu kujikomboa katika umaskini kwa kuingiza mapato kwa kutumia haki mbalimbali zinazohusiana na kazi yake ya kubunifu.”

Wakili Msambila ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Tanzania Artists Rights Organization (TARO) inayotetea haki za kisheria za wasanii nchini Tanzania anafafanua zaidi ni kwa namna gani mbunifu anaweza kujikwamua kiuchumi iwapo atatambua haki za ubunifu wake.

Watu kitu ambacho hawakifahamu ni kwamba kila kazi ya kiubunifu, sanasana hizi kazi za sanaa zina haki tisa. Mfano unachora picha unauza yote, ukiuza yote unauza haki zote tisa.

 "Ukishauza haki zote tisa zinahama zinaenda kwa mtu mwingine wewe hautatumia tena ile picha. Uliyemuuzia anaichapisha anaitumia kwenye kalenda, anaichapisha kwenye tisheti, anaichapisha kwenye vitabu anajiingizia pesa. Anaichukua picha hiyo hiyo yenyewe anaichapisha anaiuza tu kama picha ya kupamba ndani," amesema Wakili Msambila.