Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wajumbe wa UN wanavyosongesha diplomasia nyuma ya pazia

Balozi Yabesh Monari wa Kenya akizungumza na Assumpta Massoi wa Habari za UN Kiswahili wakati wa mahojiano katika studio.
UN News Balozi Yabesh Monari wa Kenya (kushoto), Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa akizungumza na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

Wajumbe wa UN wanavyosongesha diplomasia nyuma ya pazia

Masuala ya UM

Ndoto ya waasisi wa Umoja wa Mataifa yam waka 1945 ya kuona vita vinakomeshwa duniani inasalia kuwa swali kubwa zaidi la kizazi chetu.

Ni kauli ya Balozi Yabesh Monari, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa wakati akihojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kuhusu nafasi ya wajumbe katika kufanikisha maono ya mwaka 1945 huko San Francisco nchini Marekani.

Hoja hiyo inazingatia kuwa tarehe 25 mwezi Aprili kila mwaka ni siku ya wajumbe wanaowakilisha nchi zao kwenye Umoja wa Mataifa, ikikumbuka tarehe 25 mwezi Aprili mwaka 1945 wakati wajumbe wapatao 850 wanaowakilisha nchi 50 waasisi wa Umoja wa Mataifa, walikutana wakati Vita Kuu ya Pili ya Dunia ikiendelea kusaka ‘muarobaini’ wa vita na ndipo Umoja wa Mataifa ukazaliwa kupitia Chata iliyopitishwa miezi miwili baadaye yaani tarehe 25 Juni 1945.

Mwanamume akiwa mezani akisaini Mkataba wa UMOJA WA MATAIFA wakati wa Mkutano wa San Francisco mwaka 1945, akiwa amezungukwa na wajumbe wengine.
United Nations India ikitia saini Mkataba wa Umoja wa Mataifa, Juni 26, 1945

Balozi Monari anasema, “waasisi wa Umoja wa Mataifa walitaka kuona dunia ambamo bunduki inawekwa mbali na badala yake majadiliano yanatumia. Ndoto hiyo bado ni muhimu leo kama ilivyokuwa mwaka wa 1945.”

Hata hivyo amesema ili ndoto hiyo ifanikiwe “tunapaswa kuwekeza tena katika mfumo wa ushirikiano wa kimataifa. Lazima tuimarishe zana za kidiplomasia kuzuia migogoro kabla haijaanza, na kuhakikisha ushirikishwaji wa kweli wa mataifa yote hasa zile za kusini mwa dunia au zile zinazoendelea.”

Mabadiliko anayoona yanapaswa kufanyika

Mathalani amesema linahitajika Baraza la Usalama lenye uwakilishi mpana, mfumo wa maendeleo unaojibu kwa haraka changamoto za karne hii na taasisi zinazowajibika na zenye uwezo wa kusuluhisha migogoro, kushughulikia mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha haki kwa wote.

“Lakini zaidi ya yote lazima kurejesha imani ya watu kwa taasisi za kimataifa, imani kwa sheria za kimataifa. Imani kwamba hakuna taifa lililo juu ya mkataba wa Umoja wa Mataifa. Hivyo ndivyo tutakavyoheshimu urithi wa San Francisco si kwa maneno tu bali kwa vitendo,” amesema Balozi Monari.

Je siku nzima ya wajumbe inakuwa namna gani

Naibu huyu Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa amefafanua kuwa “tunaanza na mikutano ya ndani kwa ndani kwenye ubalozi tukijadili mikutano ya siku hiyo tukizingatia mwongozo kutoka serikali kuu huko nyumbani Kenya na kupanga msimamo wetu katika mazungumzo. Baadaye tunahudhuria mikutano mbalimbali. Kikao cha Baraza Kuu, mazungumzo yasiyo rasmi, vikao vya Baraza la Usalama au mikutano ya pande mbili na mabalozi wenzetu.”

Amesema nyuma ya kila hotuba kuna kazi ya kidiplomasia ya kimyakimya.

Alipoulizwa nini wanazingatia hadi kufikia muafaka wa jambo kwa kuzingatia nchi 193 wanachama wa UN kila moja inakuwa na misimamo tofauti wakati mwingine, Balozi Monari amesema, “mazungumzo lazima yalingane na azimio ya kimataifa. Kulingana na sheria ya Umoja wa Mataifa, kwa sababu Umoja wa Mataifa kazi yake ni kuleta nchi zote pamoja. Kwa hivyo mazungumzo yote yanakuwa ni lugha kwa watu wote ya pamoja katika misingi ya kimataifa.”

Alipoulizwa iwapo ana mfano wa tukio ambamo kwalo kulikuwa na mvutano lakini baadaye waliafikiana, Balozi Monari akataja wakati Kenya ilikuwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

“Hii ilikuwa kati ya mwaka 2020 na 2021. Mojawapo ya masuala tata yalikuwa jinsi ya kushughulikia migogoro mikubwa huku tukizingatia uhuru wa nchi. Kuna wakati wajumbe waliogawanyika kuhusu migogoro kama ile ya Ethiopia na Ukraine.”

Anasema Kenya ilisimama kidete kutetea mipaka ya mataifa na kutatua migogoro kwa amani. “Tulichagua njia ya maelewano na tukasimama kusimamia haki bila kuleta mgawanyiko. Hatua hii ilitambuliwa na kuheshimiwa na mataifa.”

Jengo la makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York, likiwa na safu ya bendera za kimataifa zinazoelekea mbele.
UN Photo/Manuel Elías Jengo la makao makuu ya Umoja wa Mataifa lenye bendera za Nchi Wanachama mbele, Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York.

Ujumbe wake kwa siku ya kimataifa ya wajumbe

Kwanza ametambua na kuwapongeza wale wote wanaofanya kazi kwa bidii nyuma ya pazia kuhakikisha diplomasia inafanya kazi.

“Diplomasia ya pande nyingi ni kazi ya kila siku ya kuandika rasimu za Azimio. Kujadiliana maneno na kutafuta muafaka. Kwa upande wa Kenya tunaamini katika nguvu ya mazungumzo haya. Tunaamini kuwa Umoja wa Mataifa bado ni tumaini bora zaidi kwa dunia yenye haki, amani na maendeleo endelevu.”

Sikiliza mahojiano yote hapa.