Elimu, afya na fursa ziko hatarini kutokana na pengo la kidijitali katika jinsia: UN
Elimu, afya na fursa ziko hatarini kutokana na pengo la kidijitali katika jinsia: UN
Teknolojia za mageuzi kama vile akili mnemba AI, zinaendelea kuunda upya uchumi wa dunia, lakini mamilioni ya wanawake na wasichana bado wameachwa nyuma katika ulimwengu wa kidijitali wakinyimwa si tu fursa za maendeleo, bali pia nafasi ya kuamua mustakabali wao kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
"Kuziba pengo hili si jambo la hiari umesisitiza Umoja wa Mataifa ukiongeza kuwa Mwaka 2024, kulikuwa na wanawake milioni 189 wachache zaidi kuliko wanaume waliokuwa mtandaoni."
Kwa mujibu wa Doreen Bogdan-Martin, ambaye ni Mkuu wa Shirika la Mawasiliano la Umoja wa Mataifa ITU, tofauti hii si suala la upatikanaji pekee, bali inaonesha vikwazo vya kimuundo vya muda mrefu,
“Hizo ni fursa nyingi mno zilizopotea za kujifunza, kujipatia kipato, na kushiriki katika kuunda mustakabali wa kidijitali wa pamoja,” amesema Doreen katika ujumbe wake wa Siku ya Kimataifa ya Wasichana katika TEHAMA (ICT) inayoadhimishwa kila mwaka mwezi Aprili.
Amesisitiza kuwakuunganishwa pekee hakutoshi kuhakikisha mabadiliko ya kweli ya kidijitali.
“Kuunganishwa kidijitali lazima kuwe kwa maana, kuwa na uwezo wa kumudu vifaa na huduma za kidijitali, kuwa na ujuzi wa kutumia teknolojia na kujihisi salama katika mazingira ya mtandaoni. Kila mtu anastahili nfursa ya kustawi katika dunia inayozidi kuwa ya kidijitali.”
Mauddhui ya siku ya wasichana katika ICT 2025
Siku ya Wasichana katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA, au ICT huadhimishwa kila mwaka katika Alhamisi ya nne ya mwezi Aprili, kwa lengo la kuwahamasisha wasichana kujiingiza katika taaluma za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati au STEM.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011, zaidi ya wasichana na wanawake vijana 417,000 wameshiriki katika zaidi ya matukio 11,500 yaliyofanyika katika nchi 175 duniani kote.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Wasichana katika TEHAMA kwa Mabadiliko Jumuishi ya Kidijitali”.
Shirika la ITU linatoa wito wa kuongezwa kwa uwekezaji katika elimu ya kidijitali kwa wasichana na kupanua wigo wa upatikanaji wa teknolojia.
ITU imesisitiza kuwa wanawake vijana wengi zaidi wanapaswa kuwa wazalishaji wa teknolojia na si watumiaji tu katika dunia ya kidijitali.
“Iwe wewe ni mjasiriamali unayeanzisha kampuni ya AI, mwalimu unayejumuisha ujuzi wa kidijitali katika darasa lako, au mtunga sera unayeunda mustakabali wetu wa pamoja wa kidijitali, unaweza kusaidia kuhakikisha kila mwanamke na msichana anapata fursa ya kuunganishwa, kuunda, na kuongoza katika maeneo ya kidijitali,” amesisitiza Bi. Bogdan-Martin.
Kuna pengo kubwa linalotishia kuwaacha wasichana nyuma: ECW
Akiongeza sauti yake katika siku hii ya wasichana katika TEHAMA Mkurigenzi wa Mfuko wa Elimu Haiwezi Kusubiri ECW, Yasmine Sherif amesema “Kuna Pengo la kidijitali duniani, linalotishia kuviacha vizazi vizima vya wanawake na wasichana nyuma”
Ameendelea kusema kuwa “Leo, tunawaweka wanawake na wasichana katikati ya juhudi zetu za pamoja tunapoadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wasichana katika TEHAMA. Tunathibitisha upya dhamira yetu ya kutumia nguvu ya elimu kama chombo cha mabadiliko, na kuwapa wasichana hawa mafunzo, ujuzi na rasilimali wanazohitaji ili kuwa sehemu ya mapinduzi ya kidijitali yanayounda dunia yetu. Leo, lazima tujitolee upya kufadhili elimu yao”.
Ameongeza kuwa pengo la kidijitali linaonekana wazi zaidi katika maeneo ya mstari wa mbele ya mizozo ya silaha, mabadiliko ya tabianchi, na ukimbizi wa kulazimishwa.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO, “kote duniani, kuna pungufu ya wanawake milioni 244 wanaotumia mtandao ikilinganishwa na wanaume, hali ambayo inawanyima elimu, ajira na nafasi ya kuleta ubunifu”.
Kwa mfano,shirika hilo limesema barani Afrika, “vikwazo vya kitamaduni, gharama kubwa na vizuizi vya uhamiaji vinawazuia wasichana wengi kupata teknolojia na elimu ya kidijitali.”
UNESCO imeongeza kuwa kwa hakika, katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa kila wanaume 100 wanaojua kutumia lahajedwali ni wanawake 40 tu wenye ujuzi huo.
Takwimu mpya kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF “zinaonyesha kuwa asilimia 90 ya wasichana balehe na wanawake vijana hawako mtandaoni. Hii ni sawa na 9 kati ya 10 wanaonyimwa upatikanaji wa taarifa na fursa zisizo na kikomo ambazo mtandao unatoa.”