Raia 9 wauawa katika mashambulizi ya Urusi huko Ukraine usiku wa kuamkia leo UN yasikitishwa
Taarifa za kutisha na kusikitisha zimeendelea kujitokeza leo baada ya wimbi la mashambulizi ya Urusi dhidi ya mji mkuu wa Ukraine na miji mingine usiku wa kuamkia leo, huku ripoti za awali zikionyesha kuwa takriban watu tisa wameuawa na kadhaa kujeruhiwa.
Ripoti za mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa mashambulizi hayo ya hivi karibuni ya Urusi yameharibu majengo 12 katika mji mkuu Kyiv, yakisababisha uharibifu mkubwa kwa nyumba, biashara na huduma muhimu, huku simu zikiripotiwa kupigwa kutokea kwenye kifusi.
Miji mingine ya Ukraine iliyoathirika ni pamoja na Zhytomyr iliyoko magharibi mwa Kyiv na miji ya kaskazini mashariki ya Sumy ambako shambulio la kombora mchana wa tarehe 13 Aprili liliua watu 34 na Kharkiv ambako mamlaka ziliripoti mashambulizi 24 ya ndege zisizo na rubani au drone na makombora kwa jumla.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA imesema “Idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka wakati vikosi vya uokoaji vinaendelea na oparesheni za utafutaji na uokozi.”
Maendeleo haya yanakuja baada ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kuripotiwa kukataa pendekezo la Marekani la kusaka makubaliano ya amani na Urusi ambalo lingeihusisha Ukraine kukubali kupoteza maeneo yaliyotekwa wakati wa vita.
Duru zinasema hatua hiyo ingehusisha maeneo ya mashariki ya Ukraine ya Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporizhzhia, pamoja na Crimea, ambayo Urusi iliyanyakua kinyume cha sheria mwaka 2014.
“Shambulio kubwa la jana usiku la majeshi ya Urusi dhidi ya maeneo ya makazi mjini Kyiv na maeneo ya jirani ni ukiukaji mwingine wa kutisha wa sheria ya kimataifa za kibinadamu,” amesema mratibu wa misaada wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine, Matthias Schmale.
Watoto na mwanamke mjamzito walikuwa miongoni mwa zaidi ya watu 70 waliojeruhiwa katika mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani yaliyofanyika jana usiku.
Bwana Schmale amesisitiza kuwa “Matumizi haya yasiyo na maana ya nguvu lazima yakome. Raia hawapaswi kamwe kulengwa.”
Kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya raia
Likielezea ujumbe huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, limeomba kusitishwa kwa matumizi ya silaha za mlipuko katika maeneo ya raia ambazo zimesababisha ongezeko kubwa la mashambulizi dhidi ya maeneo ya raia mwaka huu.
Kulingana na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR, takriban raia 164 waliuawa mwezi Machi na 910 kujeruhiwa kote nchini Ukraine. Hii ni ongezeko la asilimia 50 ikilinganishwa na Februari 2025 ambapo watu waliouawa walikuwa 129 na waliojeruhiwa 588, na ni ongezeko la asilimia 71 ikilinganishwa na Machi 2024 ambapo watu waliouawa walikuwa 129 na waliojeruhiwa walikuwa 498.
Jumanne na Jumatano, wiki hii OCHA iliripoti kuwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na mabomu yamepiga maeneo yenye watu wengi “kote nchini, Ukraine huku mapigano katika maeneo ya mstari wa mbele yakiua raia zaidi”.
Miji iliyolengwa ni pamoja na Zaporizhzhia, ambako shambulio la bomu Jumanne liliua mtu mmoja na kujeruhi zaidi ya watu wengine 40, wakiwemo watoto saba na mwanamke mjamzito, kwa mujibu wa OCHA.
Pia majengo kadhaa ya makazi yaliharibiwa katika shambulio hilo kwenye jiji hilo lililo karibu na mstari wa mbele na ambalo lina wakazi 630,000, wengi wao wakiwa wakimbizi wa ndani kutoka maeneo mengine.
Ofisi ya OCHA pia imeripoti mashambulizi ya ndege zisizo na rubani usiku wa jana Jumatano katika maeneo ya Dnipro, Donetsk, Kharkiv, Kherson, Poltava na Odesa, yakiharibu hospitali, nyumba, maghala na kituo cha nishati.