Viongozi wa dunia washikamana kwa ajili ya hatua za dharura kuhusu mabadiliko ya tabianchi kabla ya COP30
Viongozi wa dunia washikamana kwa ajili ya hatua za dharura kuhusu mabadiliko ya tabianchi kabla ya COP30
Katika mkutano wa kilele wa dharura kuhusu mabadiliko ya tabianchi uliofanyika kwa njia ya mtandao leo Jumatano, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na Rais wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva wamewakutanisha viongozi 17 wa mataifa makubwa ya kiuchumi pamoja na yale yaliyo hatarini zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Lengo la mkutano huo wa ngazi ya juu ni kuharakisha dhamira ya kimataifa kuhusu tabianchi kabla ya mkutano wa mabadiliko ya tabianchi COP30 utakaofanyika Brazil.
Mkutano huo umekuwa sehemu ya mkakati wa pamoja wa kuhamasisha hatua madhubuti chini ya Mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi na kuongeza kasi ya mipango madhubuti ya kitaifa kuhusu tabianchi itakayotangazwa mwaka huu wa 2025.
Kikao hicho cha saa mbili, kilichofanyika kwa faragha, kimeijumuisha China, Muungano wa Ulaya, Muungano wa Afrika, Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN), na nchi za visiwa vidogo vinavyoendelea.
Bwana Guterres amesema mkutano huo ulikuwa no moja ya mikutano yenye utofauti mkubwa wa viongozi wa kimataifa waliolenga moja kwa moja masuala ya tabianchi kwa muda mrefu, na umewasilisha ujumbe wa mshikamano wa nguvu.
“Kama tulivyosikia leo, dunia inasonga mbele. Kwa kasi kubwa. Hakuna kundi wala serikali inayoweza kuizuia mapinduzi ya nishati safi,” ametangaza katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mkutanohuo wa farafgha.
Ahadi mpya za kitaifa
Guterres amesema viongozi wengi waliahidi kuwasilisha mipango mipya yenye malengo makubwa ya tabianchi, inayojulikana rasmi kama Michango Iliyoamuliwa Kitaifa (NDCs), haraka iwezekanavyo katika kile alichokiita “ujumbe thabiti wa matumaini.”
Guterres amesema kuwa Rais Xi Jinping wa Cina amethibitisha wakati wa mkutano kwamba NDCs mpya za China zitahusisha sekta zote za kiuchumi na gesi chafu zote ufafanuzi aliouelezea kuwa “muhimu sana kwa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.”
Ameongeza kuwa ahadi hizo zinatoa fursa muhimu ya kuonyesha mwelekeo thabiti kwa muongo ujao, na muhimu zaidi, kusaidia kuharakisha mpito wa haki kutoka kwenye nishati ya kisukuku kwenda kwenye vyanzo vya nishati mbadala.
Fursa ya karne ya kiuchumi
Uzalishaji wa nishati mbadala ni “fursa ya kiuchumi ya karne hii,” amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, akiielezea kama “njia ya kutoka kwenye jahanamu ya mabadiliko ya tabianchi.”
Ameongeza kuwa “Sekta ya nishati safi inakua kwa kasi ikiunda ajira na kuongeza ushindani na ukuaji duniani kote. Sayansi iko upande wetu na hali ya kiuchumi imebadilika.”
Amebainisha kuwa bei za nishati mbadala zimeshuka kwa kiasi kikubwa, jambo linalotoa “njia ya uhakika ya uhuru wa nishati na uhakika wa nishati, na kumaliza utegemezi wa mafuta kisukuku yenye gharama kubwa na zisizotabirika.”
Tangu Mkataba wa Paris wa mwaka 2015, makadirio ya kiwango cha joto duniani yamepungua kutoka zaidi ya nyuzi joto 4°C katika karne hii hadi nyuzi joto 2.6°C iwapo mipango ya sasa itatekelezwa.
Hata hivyo, kiwango hicho bado hakitoshi kufikia lengo la kuweka ongezeko la joto duniani kuwa chini ya nyuzi joto 1.5°C juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda lengo lililokubaliwa Paris na kuungwa mkono na wanasayansi wa tabianchi.
Katibu Mkuu amewasihi viongozi kuwasilisha mipango ya kitaifa inayolingana na lengo hilo, inayojumuisha gesi chafu zote na sekta zote, na kuonyesha dhamira kamili ya kufikia hali ya kutozalisha kabisa gesi chafu (net zero) kufikia mwaka 2050.
Uhamasishaji wa kimkakati
Kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina kabla ya mkutano, mkutano wa leo umekuwa “hatua nyingine katika jitihada muhimu za kudumisha kasi ya kisiasa katika mwaka huu wa mabadiliko muhimu kuhusu tabianchi”.
Afisa huyo amesema kundi la walioalikwa lilikuwa “dogo lakini la wawakilishi muhimu,” likijumuisha mataifa makubwa ya kiuchumi, nguvu za kikanda, wenyeji wa zamani wa mikutano ya COP, na mataifa yaliyo hatarini zaidi kwa madhara ya tabianchi.
“Huu ni mwaka muhimu sana,” afisa huyo amesema, akitaja kumbukumbu ya miaka 10 ya Mkataba wa Paris na tarehe ya mwisho inayokaribia kwa nchi kuwasilisha mipango mipya ya tabianchi.
“Mkutano huu ni wa kuwakumbusha viongozi kuwa tabianchi bado ni kipaumbele kikuu na kwamba ushirikiano na mfumo wa kimataifa bado vina umuhimu.”
Afisa mwandamizi wa Brazil aliyeshiriki amesema mkutano wa tabianchi wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika Belém utavuka hatua ya majadiliano na kuzingatia utekelezaji, uwazi, na utoaji wa matokeo.
“Tayari tumeshafanya majadiliano ya kutosha sasa dunia inataka kuona vitendo matokeo, mifano, suluhisho.”amesema
Afisa huyo pia amesisitiza kuwa kuonyesha matokeo halisi ni muhimu kwa ajili ya kurejesha imani katika mfumo wa kimataifa wa kushirikiana.
“Tunataka kuthibitisha kuwa mfumo wa kimataifa siyo tu kuhusu kuandaa nyaraka,” amesema, “bali kuhusu kuzifanya kuwa hali halisi.”
Wito wa haki na ufadhili
Bwana Guterres amesisitiza hitaji la kuelekeza msaada mkubwa zaidi kwa nchi zinazoendelea, ambazo ndizo zinazokumbwa na athari mbya zaidi za mabadiliko ya tabianchi licha ya kuwa na mchango mdogo katika utoaji wa hewa chafuzi duniani.
“Afrika na maeneo mengine ya dunia yanayoendelea yanapitia ongezeko la joto kwa kasi zaidi na visiwa vya Pasifiki vinashuhudia ongezeko la kasi la kina cha bahari wakati wastani wa dunia nao unaongezeka kwa haraka,” amesema.
Amezihimiza nchi kuwasilisha mpango wa kueleweka wa kuhamasisha dola trilioni 1.3 kwa mwaka kwa ajili ya nchi zinazoendelea ifikapo mwaka 2035, kuongeza mara mbili ufadhili wa kukabiliana na athari za tabianchi hadi kufikia dola bilioni 40 mwaka huu, na kuongeza michango kwa Mfuko mpya wa Hasara na Madhara ulioanzishwa katika COP28.
Hakuna kupunguza kasi ya hatua za tabianchi
Katibu Mkuu pia ametangaza tukio la ngazi ya juu la Umoja wa Mataifa litakalofanyika mwezi Septemba wiki chache kabla ya mkutano wa COP30 ili kutathmini maendeleo ya mipango ya tabianchi na ufadhili.
Ujumbe uko wazi, kwa mujibu wa Bwana Guterres, “Hatuwezi, hatupaswi, na hatutakata tamaa katika kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.”