Majanga ya tabianchi yanachangia kuongezeka kwa unyanyasaji wa kijinsia, Ripoti ya UN yabaini
Majanga ya tabianchi yanachangia kuongezeka kwa unyanyasaji wa kijinsia, Ripoti ya UN yabaini
Bila hatua za haraka, mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuhusishwa na tukio moja kati ya kila matukio kumi ya vurugu za kimapenzi ndani ya ndoa ifikapo mwisho wa karne hii.
Hilo ndilo onyo kutoka kwenye ripoti mpya ya Mkakati wa Spotlight wa Umoja wa Mataifa, ambao umebaini kuwa mabadiliko ya tabianchi yanazidisha msongo wa kijamii na kiuchumi unaochochea kuongezeka kwa viwango vya vurugu dhidi ya wanawake na wasichana.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa hali mbaya ya tabianchi, kuhama makazi, ukosefu wa uhakika wa chakula, na kuyumba kwa uchumi ni sababu kuu zinazoongeza uwepo na ukali wa vurugu za kijinsia.
Athari hizi huathiri zaidi jamii dhaifu, ambapo wanawake tayari wanakumbwa na ukosefu wa usawa na hivyo kuwa katika hatari zaidi ya kushambuliwa.
Kila ongezeko la nyuzi joto 1°C duniani linahusishwa na ongezeko la asilimia 4.7 ya ukatili wa kimapenzi ndani ya ndoa, ripoti hiyo inasema. Katika hali ya ongezeko la joto la 2°C, wanawake na wasichana milioni 40 zaidi wanaweza kukumbwa na ukatili huu kila mwaka ifikapo 2090. Katika hali ya 3.5°C, idadi hiyo inazidi mara mbili.
‘Mkakati wa Spotlight’ ambao ni ushirikiano wa kimataifa kati ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa — unalenga kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana. Matokeo yake ya hivi karibuni yanasisitiza kuwa suluhisho la tabianchi lazima lijumuishe haki, usalama, na usawa ili kuwa na ufanisi na kudumu.
‘Janga kivuli’
Ripoti inaeleza kuwa unyanyasaji wa kijinsia tayari ni janga la kimataifa. Zaidi ya wanawake bilioni moja — angalau mmoja kati ya kila watatu — wamewahi kupitia ukatili wa kimwili, kingono, au kisaikolojia katika maisha yao. Takwimu hizi huenda zikawa chini ya uhalisia, kwani ni takriban asilimia saba tu ya waathiriwa wanaotoa taarifa rasmi kwa polisi au huduma za afya.
Mkakati wa Spotlight umebaini kuwa kuna ongezeko la vurugu baada ya majanga ya tabianchi. Mnamo mwaka wa 2023 pekee, watu milioni 93.1 waliathiriwa na majanga yanayohusiana na tabianchi na mitetemeko ya ardhi, huku wanawake takriban milioni 423 wakikumbwa na ukatili wa kimapenzi ndani ya ndoa. Kadri mishtuko ya tabianchi inavyoongezeka na kuwa kali zaidi, hatari ya ukatili inatarajiwa kuongezeka kwa kasi.
Kwa mfano, utafiti mmoja uliotajwa kwenye ripoti ulibaini ongezeko la asilimia 28 ya mauaji ya wanawake majumbani wakati wa mawimbi ya joto.
Athari nyingine ni pamoja na ongezeko la ndoa za utotoni, usafirishaji haramu wa binadamu, na unyanyasaji wa kingono — hasa baada ya kuhama makazi kutokana na mafuriko, ukame, au kugeuka jangwa kwa maeneo.
Jamii za pembezoni
Mzigo wa janga hili haugawanywi kwa usawa. Wanawake na wasichana wanaoishi katika umaskini ikiwa ni pamoja na wakulima wadogo na wakazi wa maeneo yasiyo rasmi mijini wako katika hatari zaidi.
Wanawake wa asili, wenye ulemavu, wazee, au wale walioko kwenye jamii ya LGBTQ+ hukumbwa na hatari nyingi kwa pamoja, huku wakikosa huduma, hifadhi, au ulinzi.
Katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, makadirio yanaonesha kuwa ukatili wa kimapenzi ndani ya ndoa unaweza kuongezeka karibu mara tatu, kutoka wanawake milioni 48 mwaka 2015 hadi milioni 140 ifikapo 2060, iwapo joto litaongezeka kwa nyuzi 4°C. Hata hivyo, chini ya hali ya kudhibiti joto hadi nyuzi 1.5°C, asilimia ya wanawake wanaoathirika inaweza kupungua kutoka asilimia 24 mwaka 2015 hadi asilimia 14 mwaka 2060.
Ripoti pia inatoa tahadhari kuhusu vitisho vinavyozidi kuongezeka dhidi ya watetezi wa haki za binadamu wa mazingira, hususan wanawake. Wengi hukumbwa na unyanyasaji, kashfa, mashambulizi ya mwili, au hata kuuawa kwa kupinga matumizi mabaya ya ardhi au uchimbaji wa rasilimali.
Huko Guatemala, wanawake waliotoa taarifa kuhusu ukataji miti haramu walifukuzwa kwa nguvu na nyumba zao kuchomwa moto. Nchini Ufilipino, wale waliopinga shughuli za uchimbaji walikumbwa na utekaji na mashambulizi ya kifo.
Wito wa dharura kwa sera za tabianchi zinazojumuisha usawa wa kijinsia
Licha ya uzito wa suala hili, ni asilimia 0.04 tu ya msaada wa maendeleo unaohusiana na tabianchi unaolenga usawa wa kijinsia. Ripoti inasema pengo hili ni ushahidi wa kushindwa kutambua jinsi vurugu za kijinsia zinavyotathmini ustahimilivu wa tabianchi na haki ya kijamii.
Mkakati wa Spotlight unatoa wito wa kuingizwa kwa mikakati ya kuzuia Unyanyasaji wa Kijinsia Majumbani (GBV) katika ngazi zote za sera za tabianchi kutoka mikakati ya mitaa hadi mifumo ya ufadhili wa kimataifa.
Mifano kutoka nchi kama Haiti, Vanuatu, Liberia, na Msumbiji imeonesha jinsi programu zinaweza kubuniwa kushughulikia vurugu na kujenga ustahimilivu kwa wakati mmoja.
Mifano hiyo ni pamoja na kuwafundisha wakunga kazi mpya katika sekta ya kilimo janja kwa tabianchi, kuhakikisha kuwa misaada ya majanga inajumuisha huduma za GBV, na kusaidia kliniki za afya zinazotembea katika maeneo ya maafa.
Ripoti inasisitiza kuwa hatua bora dhidi ya tabianchi lazima zitangulize usalama, usawa, na uongozi wa wanawake na wasichana.
Kumaliza vurugu dhidi ya wanawake na wasichana, ripoti inahitimisha, si tu suala la haki za binadamu ni muhimu kwa kufikia maisha yenye haki, endelevu, na yenye ustahimilivu dhidi ya tabianchi.