Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fahamu jinsi Haiti ilidaiwa fidia na Ufaransa ili ipate uhuru

Mnyororo wa pingu uliotumika kufungia watumwa ukiwa sehemu ya maonesho kuhusu biashara ya utumwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa (kutoka Maktaba)
UN Photo/Mark Garten Mnyororo wa pingu uliotumika kufungia watumwa ukiwa sehemu ya maonesho kuhusu biashara ya utumwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa (kutoka Maktaba)

Fahamu jinsi Haiti ilidaiwa fidia na Ufaransa ili ipate uhuru

Haki za binadamu
  • Haiti, taifa la Karibea lenye watu wa asili ya Afrika lililotawaliwa na Ufaransa
  • Miaka 200 iliyopita watumwa wakafanya mapinduzi kudai uhuru kutoka Ufaransa.
  • Sharti likawa wailipe Ufaransa fidia ya dhahabu ya dola milioni 26
  • Fidia ni kwamba wakulima wa kifaransa walipoteza 'nguvu kazi.'

Karne mbili kamili baada ya Ufaransa kuitaka Haiti illipe kiwango kikubwa cha fidia ili iweze kupata uhuru kutoka taifa hilo la Ulaya, Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa la Watu wenye Asili ya Afrika limetoa wito wa kuitaka Ufaransa irejeshe fidia hiyo iliyoidai Haiti kwa vitisho.

Wito huo umetolewa wakati wa mjadala kuhusu Deni la Kikoloni ambalo Haiti inadaiwa na Ufaransa, mjadala uliofanyika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani Alhamisi ya Aprili 17, 2025.

Haiti, taifa lililoko ukanda wa Karibea hadi sasa linaathiriwa vibaya na uhalifu wa ukoloni na utumwa.

‘Watwana’ kulipa fidia ‘mabwana’

Akizungumza kwenye mjadala huo, Monique Clesca, mwandishi wa Habari na mwanaharakati amesema "Ufaransa iliwalazimisha wale waliopigania na kupata uhuru wa Haiti, yaani waliokuwa watumwa kulipa fidia kwa wale waliokuwa wanawatawala. Yaani watwana kulipa mabwana kwa kupoteza mali zao, ambao ndio hao watumwa waliokuwa wanawafanyia kazi.”

Ikiwa ni nchi ya kwanza ya watu weusi kujikomboa kutoka katika minyororo ya utumwa kupitia mapinduzi yaliyoipatia ushindi, Haiti ilipata uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mwaka wa 1804. Hata hivyo, gharama ya kuthubutu kupinga mfumo wa utumwa haikuchukua muda mrefu kujitokeza.

Mnamo tarehe 17 mwezi Aprili mwaka 1825, chini ya tishio la mizinga ya meli za kivita za Ufaransa, Haiti ilikubali kuilipa Ufaransa fidia ya dhahabu yenye thamani ya faranga milioni 150 sawa na dola milioni 26 za wakati huo.

Fedha hizo zililenga kuwalipa fidia wakulima wa kifaransa kwa mali zilizopotea wakati mapambano ya uhuru wa Haiti, mali ambazo zinatajwa kuwa ni Pamoja na watumwa waliokuwa wanafanya kazi kwenye mashamba hayo. Lakini kiuhalisia, kiasi hicho cha fedha kilikuwa kikubwa zaidi kuliko hasara iliyopatikana.

Gharama ya kuwa uhuru: Deni mara mbili

"Mapema mno, kiwango hicho cha fedha kilikuwa mzigo mzito kwa taifa hilo la kwanza huru la watu weusi, ikisalia kugubikwa na mzunguko wa madeni.

“Wakati hatukuwa na uwezo wa kulipa tena, Ufaransa ilipuuza na ikasukuma benki zake kutukopesha pesa: ndiyo sababu tunazungumzia madeni mara mbili,” amefafanua Bi. Clesca.

Mwaka 1914, zaidi ya asilimia 75 ya bajeti ya Haiti ilikuwa ni malipo ya fidia kwa benki za Ufaransa. Ni hadi mwaka 1947, zaidi ya miaka 140 baada ya kupata uhuru wake, ndipo Haiti ilimaliza kulipa deni lake. “Ufaransa ilifanya dhuluma kubwa ambayo bado tunahisi athari zake hasi hadi leo,” amesema Bi. Clesca.

Uchunguzi wa kina wa gazeti la New York Times, uliochapishwa mwaka 2022, uliweka bayana  kwamba jumla ya fidia iliyolipwa na Haiti kwa Ufaransa ni sawa na dola milioni 560 za sasa. Kiasi ambacho, kulingana na makadirio ya baadhi ya wataalamu wa chumi, kingeongeza zaidi ya dola bilioni 20 kwenye uchumi wa Haiti iwapo kingalisalia nchini humo.

Haiti ya leo: Urithi wa deni

Benki ya Dunia inasema kuwa ikiwa Haiti inawakilisha mabadiliko makubwa katika historia ya ukombozi wa binadamu, nchi hiyo leo inakabiliwa na vurugu zinazoendeshwa na magenge yenye silaha, ambayo yanamiliki asilimia 85 ya mji mkuu wake, Port-au-Prince.

Halikadhalika ni taifa maskini zaidi katika Amerika ya Kusini na Karibea huku taasisi zake zikiwa zimedhoofika.

Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa la Watu wenye Asili ya Afrika linasema chanzo cha matatizo ya Haiti ni dhahiri kinatokana na historia yake.

"Migogoro inayoendelea ya haki za binadamu nchini Haiti, inatokana na urithi wa utumwa, ukoloni, malipo ya deni, vitisho na uingiliaji wa kijeshi,” limesema Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa kuhusu Watu wenye Asili ya Afrika, lililoanzishwa mwaka 2021ambalo ni chombo cha ushauri cha Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu.

Haki iliyocheleweshwa

Kujibu tuhuma hizo, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, alitangaza, Alhamisi, kuundwa kwa tume ya wanahistoria wa Ufaransa na wa Haiti ili kutathmini athari za fidia ya Haiti. Tume hii itakuwa na jukumu la kutoa mapendekezo.

Wakati akikaribisha tangazo hili, Martin Kimani, Mwenyekiti wa Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa la Watu wenye Asili ya Afrika, amesema kwamba ufanisi wa tume mpya utategemea nia yake ya kutambua kikamilifu ukubwa wa madhara ya deni lililowekwa na Ufaransa.

“Tunatoa wito wa urejeshaji wa kiasi cha fedha na hatua za kurekebisha ili kutatua tatizo la maendeleo duni ya Haiti,” amesisitiza Bw. Kimani, wakati wa mjadala wa Jukwaa hilo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, uliofanyika siku ya mwisho ya kufungwa kwa Jukwaa hilo Alhamisi ya APrili 17, 2025.

Wito wa kurejesha fedha - Kauli ya Haiti

Kulingana na vyombo vya habari, Rais wa Ufaransa kwa sasa hajazungumzia fidia ya kifedha inayowezekana, kama inavyodaiwa sio tu na Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa kuhusu watu wenye asili ya Afrika, bali pia mamlaka za Haiti.

“Historia ya ukoloni inaleta majukumu ambayo yanapaswa kubebwa kwa pamoja na Ufaransa na jumuiya ya kimataifa,” amesema Pierre Ericq Pierre, Mwakilishi wa Kudumu wa Haiti katika Umoja wa Mataifa, alishiriki mjadala huo.

Kwa Mwakilishi huyo wa Kudumu wa Haiti, mizizi ya kimuundo ya ukosefu wa usawa unaoendelea nchini mwake inahusiana sana na historia yake ya kikoloni na kulazimishwa kwa deni hili, ambalo wahaiti wanaliita zaidi 'fidia.' Kwa hivyo, ni jambo la kawaida kwake kwamba kiasi kilicholipwa kirejeshwe kwa Haiti. Amesema, “hii si kulipiza kisasi, ni kitendo cha ukweli na haki.”