Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jukwaa la vijana la Umoja wa Mataifa laleta mitazamo mipya kuhusu maendeleo endelevu

Mshiriki akihudhuria Jukwaa la Vijana la Baraza la Uchumi na Kijamii (ECOSOC) lenye mada 'Vijana Mbele: Kutumia Sayansi na Ushirikishwaji wa Kijamii kwa Maendeleo Endelevu'.
UN Photo/Manuel Elías Mmoja wa Mswashiriki wa Jukwaa la Vijana la Baraza UN la Kiuchumi na Kijamii (ECOSOC) akifuatilia mijadala katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York., Marekani.

Jukwaa la vijana la Umoja wa Mataifa laleta mitazamo mipya kuhusu maendeleo endelevu

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Vijana kutoka kote ulimwenguni wanakutana jijini New York, Marekani katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa wiki hii kushiriki mapendekezo na maoni yao ya kubadilisha dunia kuwa mahali penye haki na usawa zaidi, bora zaidi, na endelevu.

Tweet URL

Wakiweka mabadiliko endelevu na ujumuishaji wa kijamii kuwa kiini cha juhudi zao, Jukwaa la Vijana la Baraza la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Kiuchumi na kijamii ECOSOC  ndilo kongamano kubwa zaidi la kila mwaka linalowaleta pamoja vijana.

“Uharaka wa kuunda mustakabali endelevu, jumuishi na wa haki kwa wote haujawahi kuwa dhahiri zaidi,” amesema Rais wa ECOSOC, Bob Rae, wakati wa kikao cha ufunguzi.

Likiandaliwa na Rais wa ECOSOC kwa ushirikiano na idara mbalimbali za Umoja wa Mataifa, jukwaa hili linatoa nafasi kwa vijana kushiriki kikamilifu katika mazungumzo na Nchi Wanachama wa UN pamoja na mashirika ya mfumo wa UN.

“Ninyi ni viongozi wa leo. Hatuwezi kusubiri kesho tunahitaji mshiriki na kuchukua hatua leo,” Bw. Rae amewaambia vijana waliokuwepo.

Vijana katika mstari wa mbele

Kaulimbiu ya mwaka huu, “Vijana katika mstari wa mbele’ inaangazia mawazo bunifu na miradi ya vijana na wengine inayolenga kuboresha afya na elimu, kupunguza ukosefu wa usawa, na kuchochea ukuaji wa uchumi, yote haya yakifanyika sambamba na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda bahari na misitu yetu.

“Ni muhimu sana kuwakilisha sauti za watu ambao hawana nafasi au fursa ya kutoa maoni yao juu ya masuala muhimu,” amesema Selvican Sahin, mshiriki kutoka Ujerumani, alipoulizwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Ujumuishaji wa kijamii

Dunia ikikabiliwa na misururu ya migogoro tata, kuna haja kubwa ya kusikia sauti za vijana. Kama mawakala na wachochezi wa mabadiliko, vijana ni wachangiaji wa haki za kijamii, maendeleo endelevu na usalama wa kimataifa.

Jukwaa hili linaangazia umuhimu wa ujumuishaji wa kijamii katika maendeleo endelevu. “Kuwaleta watu wengi mezani ni muhimu sana kwa sababu hapo ndipo unaweza kusikia matatizo yao,” Ryan Li kutoka Canada ameiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Sauti muhimu

Kwa kuleta mitazamo mipya na yenye ujasiri, vijana wanatekeleza jukumu muhimu na la kipekee kama nguvu ya maendeleo endelevu, wakisukuma ubunifu na maendeleo katika ngazi za kijamii, kitaifa na kimataifa.

Alipoulizwa kuhusu umuhimu wa uwakilishi wa vijana katika Umoja wa Mataifa, mshiriki Chaïmane Ribani anasema vijana “wanataka kuwa sehemu ya mabadiliko,” na “wanataka kushiriki katika kuunda sera za kitaifa na kimataifa.”

Ushiriki hai wa vijana katika mijadala kama hii ni msingi thabiti wa siku zijazo endelevu, zenye usawa na ujumuishi kwa vizazi vijavyo.

“Kuwawezesha vijana wetu ni uwekezaji unaoleta manufaa ya muda mrefu kwa jamii na kwa siku zijazo wanazozibuni,” amesema Philemon Yang, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, wakati wa kikao cha ufunguzi.

Jukwaa la Vijana la ECOSOC limeanza tangu Jumanne Aprili 15  na litaendelea hadi Alhamis tarehe 17 Aprili, likijumuisha vikao vinane vya mada mbalimbali vinavyolenga kuendeleza Ajenda ya 2030 ya UN na Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu (SDGs).