Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zambia yaendelea kuwakirimu wakimbizi licha ya changamoto za ukame na rasilimali: UNHCR

Mwanamke katika shamba la nanasi akikagua nanasi nchini Zambia.
UNDP Mkimbizi Mkulima wa mananasi nchini Zambia.

Zambia yaendelea kuwakirimu wakimbizi licha ya changamoto za ukame na rasilimali: UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Zambia inaendelea kuwahifadhi zaidi ya wakimbizi 106,000, wengi wao wakiwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Burundi, pamoja na wakimbizi wa zamani kutoka Rwanda na Angola, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, ambalo limesema kwa kuzingatia sera yake jumuishi, nchi hiyo inakuza mshikamano na wakimbizi na kuwawezesha kujitegemea kupitia makazi maalum na ushirikiano na jamii za wenyeji. 

Shirika hilo la wakimbizi limesema katika makazi kama Mayukwayukwa na Maheba ambayo ni moja ya kambi kubwa zaidi ya wakimbizi nchini Zambia familia za wakimbizi zilizolazimika kukimbia makwao zinajumuishwa ili ziweze kujikimu na kuishi kwa utangamano na wenyeji wanaowahifadhi. 
 
Moulid Hujale, ni afisa habari msaidizi wa UNHCR anasema“Selikali ya Zambia inajumuisha wakimbizi katika huduma za kitaifa kama vile elimu na hata programu za msaada wa kilimo  ili kuongeza uzalishaji”
 
Amebainisha kuwa kwa kufanya hivyo Zambia imeonesha mshikamano wa dhati kwa jamii hizo za wakimbizi kwa kuhakikisha kuwa wanapata fursa ya kujenga upya maisha yao, kujikwamua kiuchumi na kuishi kwa heshima.
Miriam Mwanza, mkulima nchini Zambia, anatabasamu huku akiwa ameshika mahindi yaliyovunwa na jembe katika shamba la alizeti na mahindi.
© UNICEF/Karin Schermbrucker Huko Chipata, Zambia, wanawake wanajifunza kuhusu lishe na jinsi ya kupanda mazao yanayohimili mabadiliko ya tabianchi.
Hata hivyo, UNHCR inasema nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika pamoja na ukarimu wake bado inakumbwa na athari za ukame mkali uliotishia uhakika wa chakula na kuyumbisha uchumi na katika hatua za kukabiliana na hali hiyo, Moulid ansema UNHCR inashirikiana na serikali ya Zambia kuunganisha makazi ya wakimbizi kwenye gridi ya taifa ya umeme. Tunajua muundo huu wa ujumuishwaji na maisha endelevu vinagharimu fedha, Lakini hiki ndicho hasa wakimbizi wanachokihitaji, hivyo tunahitaji msaada wako ili kufanikisha hili”.
 
Licha ya mafanikio yaliyopatikana hadi sasa Zambia katika kuwakirimu wakimbizi,  UNHCR imeonya kuwa uhaba wa fedha inaokabiliwa nao  unatishia kuathiri mafanikio hayo na hasa utoaji wa huduma muhimu kwa familia hizo zilizolazimika kufungasha virago na kusaka usalama Zambia. 
Sasa limetoa ombi la msaada wa haraka wa kimataifa ili kuendelea kufanikisha huduma za kuokoa maisha zinazohitajika sana na wakimbizi hao.