Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamilioni ya watu Sudan wanahitaji msaada sasa kuliko wakati mwingine wowote: Mashirika ya UN

Mikono inaonyeshwa ikichagua dengu nyekundu na mtama wakati wa usambazaji wa chakula wa Programu ya Chakula Duniani katika eneo la IDP huko Kassala, Sudan.
© UNOCHA/Giles Clarke Wakimbizi wa ndani wakipokea msaada wa chakula Kassala Sudan

Mamilioni ya watu Sudan wanahitaji msaada sasa kuliko wakati mwingine wowote: Mashirika ya UN

Amani na Usalama

Vita ya Sudan ikitimiza miaka miwili na kuanza mwaka wa tatu mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yameonya kwamba hali inaelekea kuwa mbaya zaidi kabla ya kutengamaa.

Yamesema Sudan hivi sasa ndio janga kubwa na baya zaidi la kibinadamu duniani.

Miundombinu ya msingi Khartoum imesambaratishwa

Miundombinu ya msingi katika mji mkuu wa Khartoum imeharibiwa vibaya na mapigano, na timu za misaada zimetahadharisha kuwa msaada unahitajika haraka ili kusaidia takriban watu milioni tatu wanaotarajiwa kurejea katika mji huo.
Luca Renda, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP nchini Sudan amesema “Hali katika mji mkuu Khartoum ni mbaya sana, hasa katika maeneo ambayo mapigano yamekuwa makali, kufuatia kutekwa tena mji huo na Jeshi la Sudan.”
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva baada ya ziara ya tathmini katika mji mkuu huo, ameeleza kuwa alishuhudia “uharibifu mkubwa wa miundombinu, kukosekana kwa maji, hakuna umeme, na pia kuwepo kwa mabomu mengi yaliyosalia bila kulipuka.”
Ameongeza kuwa “Mauaji ya halaiki yanayodaiwa kufanywa na wapinzani wa Kikosi cha Msaada wa Haraka RSF na washirika wao katika kambi za Zamzam na Abu Shouk huko Darfur yanaripotiwa kuua raia 400 na wahudumu wa afya 10 kutoka shirika la Relief International.”
Amesema hili ni tukio la karibuni tu katika mzozo uliogubikwa na kiwango kikubwa cha ukatili wa kingono.
Watoto waliokimbia makazi yao na mama yao wakipiga picha katika kambi ya wakimbizi wa ndani huko Ed Damazine, Jimbo la Blue Nile, Sudan.
© Save the Children/Khalid Abdulfattah Noureldin akiwa na familia yake kambini baada ya kufurushwa na vita

Watu 80,000 wamekimbia kambi ya Zamzam: IOM

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM, watu takriban 80,000 tayari wamekimbia kutoka Zamzam, lakini idadi hiyo inaweza kufikia 400,000.
Wakazi wa kiume walikuwa walengwa wakuu na wamekuwa wakikimbilia mji mkuu wa kikanda, El Fasher, ambao bado uko chini ya udhibiti wa jeshi la Sudan licha ya mashambulizi yanayoendelea kutoka RSF.
Akizungumza kutoka Port Sudan, Mkuu wa IOM nchini humo, Mohamed Refaat, amesema “wanawake walionusurika ukatili wa kingono walimweleza jinsi walivyoshambuliwa mbele ya waume zao waliokuwa wamejeruhiwa, mbele ya watoto wao waliokuwa wakipiga kelele.”
Msichana mdogo nchini Sudan anakula Plumpy'Sup, chakula kilichoongezewa virutubisho, katika kliniki inayofadhiliwa na WFP huko El Obeid, North Kordofan.
Nearly 18 million people across Sudan are facing acute hunger. Takriban watu milioni 18 kote nchini Sudan wanakabiliwa na njaa kali.

Mahitaji ya kibinadamu yameongezeka mara dufu: UN Women

Anna Mutavati, Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake UN Women kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini amesema Kutokana na hayo, kumekuwa na ongezeko kubwa la kushangaza la asilimia 288 la mahitaji ya msaada wa kuokoa maisha baada ya visa vya ubakaji na ukatili wa kingono.
Ameongeza kuwa “Tumeshuhudia pia kile kinachoanza kuonekana kama matumizi ya ubakaji na ukatili wa kingono kama silaha ya vita”.
Pia amesema “Tumeshuhudia maisha ya wanawake na miili ya wanawake ikigeuzwa kuwa uwanja wa mapambano katika mzozo huu wa kikatili.”