Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko na migogoro yanachochea dharura ya Kibinadamu DRC, UNHCR yaonya

Mkimbizi akiwa amebeba mali zake baada ya kuvuka kuingia Uganda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© UNHCR/Yonna Tukundane
Mkimbizi akiwa amebeba mali zake baada ya kuvuka kuingia Uganda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mafuriko na migogoro yanachochea dharura ya Kibinadamu DRC, UNHCR yaonya

Msaada wa Kibinadamu

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inakabiliwa na janga kubwa la kibinadamu huku mchanganyiko wa migogoro na majanga ya hali ya hewa ukisababisha mateso makubwa kwa jamii, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limeonya leo Aprili 15.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Ofisi za Umoja wa Mataifa za mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa UNHCR, Eujin Byun ameelezea hali mbaya katika Jimbo la Tanganyika, ambako mvua kubwa zisizo na kikomo zimesababisha mafuriko makubwa yaliyowafurusha karibu watu 10,000 kutoka makazi yao katika wiki za hivi karibuni. Mafuriko haya yanakuja wakati eneo hilo likikabiliwa na wimbi la wakimbizi wa ndani wapatao 50,000 waliokimbia machafuko katika jimbo jirani la Kivu Kusini tangu Januari.
 
“Mafuriko haya yanaonesha janga la ‘mgogoro maradufu’ — ambapo mishtuko ya hali ya hewa inazidisha mateso yanayosababishwa na vita na uhamishaji wa watu,” amesema Byun.
 

Mto wavunja kingo

 
Mto Rugumba ulifurika na kuvunja kingo zake, na kuathiri maeneo makubwa ya Kalemie na Nyunzu. Nyumba, shule, na mashamba vimesombwa, na kuwaacha maelfu bila makazi wala riziki. Mazao muhimu kama mihogo, mahindi na karanga yameharibiwa, jambo linalozidisha uhaba wa chakula katika eneo hilo.
Maji yaliyotuama na yaliyochafuliwa pia yameongeza hofu ya milipuko ya magonjwa. Visa vya kipindupindu katika Jimbo la Tanganyika vimeripotiwa kuwa mara sita zaidi ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
 
Katika maeneo mbalimbali ya DRC, hali ni ya kutia wasiwasi mkubwa. Tathmini za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa watu milioni 2.3 katika majimbo ya Kivu Kusini, Kivu Kaskazini, Ituri, na Tanganyika wako hatarini kukumbwa na baa la njaa katika miezi ijayo iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
 

Msaada unaendelea

 
UNHCR na wadau wake wa kibinadamu wanaendelea kutoa misaada ya dharura, ikiwa ni pamoja na makazi ya muda, maji safi, chakula na huduma za afya. Hata hivyo, juhudi hizi zinakwamishwa na ukosefu mkubwa wa ufadhili. Hadi sasa, shirika hilo limepokea asilimia 20 tu ya fedha zinazohitajika kwa ajili ya shughuli zake za kuokoa maisha nchini humo.
 
Wakati huohuo, uhamaji wa watu unaendelea kuvuka mipaka ya DRC. Takriban wakimbizi wa DRC 120,000 wamekimbilia Burundi, Tanzania na Uganda, huku zaidi ya wakimbizi 5,500 wakiwasili Uganda wiki iliyopita pekee. Licha ya machafuko yanayoendelea, baadhi ya wakimbizi wamerudi DRC kutokana na hali ngumu katika nchi za mwenyeji, ikiwemo uhaba wa chakula, makazi na huduma muhimu.
 
“Kurejea kwa wakimbizi kwenye maeneo ya migogoro kutokana na kukata tamaa kunadhihirisha umuhimu wa kuongeza msaada — si tu ndani ya DRC, bali pia kwa nchi jirani zinazowahifadhi,” alisema Byun.
 
Kwa kuzingatia changamoto zinazoletwa na mafuriko, migogoro, njaa, na tishio la milipuko ya magonjwa, hali ya kibinadamu nchini DRC inazidi kuwa mbaya. UNHCR inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada na ufadhili ili kuzuia madhara zaidi na kupunguza mateso ya mamilioni ya watu waliokumbwa na janga hili.
 
“Bila msaada wa haraka na wa kutosha, athari za ‘mgogoro huu maradufu’ zitazidi kuwa mbaya,” amenya Byun.