Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 23 na wahudumu 9 wa misaada wauawa katika mashambulizi mapya Darfur: UNICEF

Hali ya usalama imesababisha watu wengi kutawanywa Darfur wakiwemo watoto
WFP/Abdulaziz Abdulmomin
Hali ya usalama imesababisha watu wengi kutawanywa Darfur wakiwemo watoto

Watoto 23 na wahudumu 9 wa misaada wauawa katika mashambulizi mapya Darfur: UNICEF

Amani na Usalama

Watoto takriban 23 na wahudumu 9 wa misaada wameripotiwa kuuawa katika mfululizo wa mashambulizi katika eneo la Darfur Kaskazini, Sudan, katika kipindi cha siku tatu zilizopita, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, Catherine Russell.

Amesema ghasia hizi, ambazo zimeikumba Al Fasher, kambi ya wakimbizi wa ndani ya Zamzam na kambi ya Abu Shouk, zimeonesha jinsi mgogoro unaoendelea nchini Sudan unavyoendelea kuwaangamiza raia, hasa watoto.

Kambi za wakimbizi wa ndani zavamiwa

UNICEF imethibitisha kuwa “watoto 16 waliuawa Al Fasher, watoto 6 na wafanyakazi wa misaada 9 waliuawa katika kambi ya Zamzam, na mtoto mmoja katika kambi ya Abu Shouk katika mashambulizi ya kikatili dhidi ya wakimbizi wa ndani na wahudumu wa misaada ya kibinadamu.”
Russell ameyataja matukio haya kama "Ni ya kinyama na kutaka vurugu hizo zikome mara moja.”
Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, zaidi ya watoto 140 wameripotiwa kuuawa au kujeruhiwa vibaya Al Fasher pekee, jambo linaloonesha hali ya hatari inayowakabili watoto walio katika maeneo ya vita.
Watoto waliokimbia makazi yao kutokana na vita nchini Sudan sasa wanaishi Atbara.
© UNICEF/Abdulazeem Mohamed
Watoto waliokimbia makazi yao kutokana na vita nchini Sudan sasa wanaishi Atbara.

Msaada wa Kibinadamu Wazuiwa

Taarifa ya Russel imeendelea kusema kwamba “Hali inazidi kuwa mbaya huku upatikanaji wa msaada kwa kambi ya Zamzam ukiwa umekatizwa, na vikundi vyenye silaha kuripotiwa kuvamia vijiji vya mashambani na kufanya utoaji wa misaada ya kibinadamu na bidhaa za biashara kuwa jambo lisilowezekana”.
Bi. Russe aesema Takribani watu milioni moja, nusu yao wakiwa watoto, wako kwenye hatari kubwa ya njaa na maradhi iwapo msaada wa haraka hautawafikia.
Shughuli chache za misaada zilizobakia zinaendelea kuwa katika hatari kutokana na kuongezeka kwa ghasia.

UNICEF yataka watoto na wahudumu wa misaada kulindwa

Russell amezitaka pande zote zinazohusika kwenye mzozo huo kuheshimu na kulinda raia, wakiwemo watoto na wahudumu wa misaada ya kibinadamu, kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu.
Pia ametaka mapigano yakome mara moja katika maeneo ya Zamzam na Abu Shouk ili kuruhusu msaada wa haraka na salama kuwafikia walioathirika.
"Watoto lazima walindwe dhidi ya ukatili huu usio na maana," amesisitiza Russell.
Noureldin akiwa na familia yake.
© Save the Children/Khalid Abdulfattah
Noureldin akiwa na familia yake.

Kumbukumbu ya machungu ya zamani Darfur

Mauaji haya ya sasa amesema mkuu huyo wa UNICEF “yanafananishwa na machafuko yaliyotikisa Darfur miaka ishirini iliyopita.”
Onyo la UNICEF ni kumbusho tosha la historia ya ukatili wa kinyama dhidi ya raia wa Darfur na madhara yanayoweza kutokea iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.
Russell amehitimisha kwa ujumbe mzito kwa jumuiya ya kimataifa na pande zinazozozana akisema "Kutokuchukua hatua kutasababisha mateso na vifo zaidi. Wanaohusika kwenye vita hivi wana jukumu la kisheria na la kimaadili la kuwalinda watoto na kuruhusu misaada ya kuokoa maisha kuwafikia haraka."