Mzozo wa Sudan ukiingia mwaka wa tatu, Tume Huru ya UN yalaani mauaji ya Darfur
Mwanamke akiwa amebeba maji katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Al Houri jimboni Gedaref, Sudan
Mzozo wa Sudan ukiingia mwaka wa tatu, Tume Huru ya UN yalaani mauaji ya Darfur
Amani na Usalama
Tume huru ya Umoja wa Mataifa ya kusaka ukweli kuhusu Sudan imelaani mauaji ya watu zaidi ya 100 yaliyotekelezwa katika kambi za wakimbizi wa ndani huko Darfur mwishoni mwa wiki na kuonya kwamba mzozo mkubwa unaoendelea nchini humo unaweza kuwa mbaya zaidi huku vita vikielekea kuingia mwaka wa tatu.
Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo Aprili 14, siku moja kabla ya kutimia miaka miwili kamili ya vita vya sasa vya Sudan, Tume hiyo imesisitiza wito wake kwa pande zinazopigana kusitisha mapigano mara moja na kuacha kushambulia raia, na kuzitaka nchi nyingine kutochochea vita hivyo na kuhakikisha kuwa sheria ya kimataifa ya kibinadamu inaheshimiwa.
“Sudan inaingia mwaka wake wa tatu wa mzozo; ni lazima tutafakari hali mbaya nchini humo na kuenzi maisha ya Wasudan wote waliopotea au kubadilika milele,” anasema Mohamed Chande Othman, mwenyekiti wa Ujumbe huo wa Utafiti wa Ukweli. “Dunia imeshuhudia miaka miwili ya mzozo usio na huruma ambao umewanasa mamilioni ya raia katika mazingira ya kutisha, wakiwekwa katika hali ya ukatili bila matumaini ya mwisho. Katika ongezeko la kauli za chuki na vurugu zinazoongozwa na misingi ya kikabila, tunahofia kuwa sura za giza zaidi za mzozo huu bado hazijafunuliwa.”
Mnamo tarehe 15 Aprili 2023, wakazi wa mji mkuu Khartoum walisikia milio ya risasi na milipuko, ikiashiria mwanzo wa mapigano makali kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Kikosi cha waasi cha Rapid Support Forces (RSF), ambacho kilienea kwa haraka kote nchini. Tangu wakati huo, maelfu ya raia wameuawa, wengine wakikumbwa na ubakaji na ukatili wa kingono, uhamishaji wa kulazimishwa, njaa, uporaji na uharibifu wa makazi, vituo vya afya, masoko na miundombinu mingine ya kiraia. Idadi isiyojulikana ya Wasudan pia hawajulikani walipo, huku wafanyakazi wa misaada na watetezi wa haki za binadamu wakiendelea kutishiwa na kushambuliwa.
Tume hii ya kufanya utafiti wa ukweli, iliyoundwa na Baraza la Haki za Binadamu mwezi Oktoba 2023, imeendelea kuchunguza ukiukwaji wa haki uliofanyika wakati wa mzozo, ikiwemo kwa kukusanya ushuhuda kutoka kwa mashahidi na manusura wa ukatili mkubwa nchini humo. Ujumbe huo umepata taarifa za moja kwa moja kuhusu ukatili uliofanyika El Fasher na maeneo ya karibu katika Darfur Kaskazini, ikiwemo mashambulizi ya makusudi dhidi ya raia kwa mabomu, uporaji mkubwa na kuchomwa kwa mali za raia, mashamba na mazao.
Manusura kutoka kambi ya Zamzam, kusini mwa El Fasher – mojawapo ya kambi kubwa zaidi za wakimbizi wa ndani nchini Sudan yenye idadi ya watu wanaokadiriwa kufikia 750,000, nusu yao wakiwa watoto kwa mujibu wa UNICEF – walielezea hali ya kuzingirwa ambayo imepunguza sana uwezo wao wa kupata chakula, maji, dawa na uhuru wa kutembea. Hali hizi zinaendelea hadi leo, na upatikanaji wa misaada ya kibinadamu katika kambi hiyo bado ni mgumu mno, hali iliyosababisha watoto kufa kwa njaa kwa mujibu wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP).
Manusura walieleza jinsi walivyokuwa wakizuiwa, kudhalilishwa, kuporwa na kuwekwa kizuizini katika vituo vya ukaguzi karibu na El Fasher na kambi ya Zamzam. Walitoa ushahidi kuhusu uporaji wa mali, mifugo na chakula, mauaji ya watu kadhaa na kuchomwa kwa vijiji vingi karibu na El Fasher, ikiwemo maeneo ya kaskazini kati ya Kutum na Anka mnamo Oktoba 2024, na Abu Zerega, Shagra, na Golo mnamo Desemba 2024 na Januari 2025. Matukio haya mengi yamehusishwa na RSF.
Mashambulizi ya karibuni kutoka kwa RSF – yaliyoanza tarehe 11 Aprili na kulenga makazi ya wakimbizi wa ndani ya Zamzam na Abu Shouk, pamoja na mji wa El Fasher – yamesababisha vifo vya zaidi ya watu mia moja, wakiwemo wahudumu tisa wa afya kutoka shirika la Relief International.
Matukio ya kutisha
Ujumbe pia umepokea taarifa za kutisha kuhusu mashambulizi ya kisasi yaliyofanywa na SAF na washirika wake katika maeneo waliyoyarejesha kutoka RSF. Wanachunguza matukio hayo, ikiwemo ripoti za watu kuwekwa kizuizini na kunyongwa au kuuawa bila kupitia mahakama, hasa katika maeneo ya Al-Dinder na Sinja katika jimbo la Sennar, na Wad Madani katika jimbo la Al-Gezira kati ya Septemba 2024 na Januari 2025.
Maeneo mapya yaliyodhibitiwa na SAF huko Khartoum, ambapo SAF ilitangaza udhibiti kamili tarehe 7 Aprili, yameripotiwa kushuhudia vitendo vya kisasi vikali kutoka kwa SAF na washirika wake, wakiwemo watu kunyongwa hadharani bila kesi za haki na kukamatwa kwa idadi kubwa ya watu katika maeneo kama Al-Kalakla na sehemu nyingine za kusini mwa Khartoum, huku hatima ya waliokamatwa ikiwa haijulikani.
Mkutano London
Kesho Jumanne, karibu mataifa 20, mengi yakiwa na ushawishi kwa pande zinazopigana, yatakutana London kujadili hali ya kibinadamu nchini Sudan.
Ujumbe wa Utafiti wa Ukweli unazihimiza nchi hizi kubuni na kusaidia hatua za kuwalinda raia na kuhakikisha kuheshimiwa kwa haki za binadamu na sheria ya kimataifa ya kibinadamu na pande zote.
“Mauaji ya halaiki ya raia yaliyotokea katika kambi za Zamzam na Abu Shouk wikendi hii ni ya kutisha,” anasema Mona Rishmawi, mjumbe wa Tume hiyo.
“Mashambulizi ya makusudi dhidi ya raia, wahudumu wa afya na miundombinu ya afya ni uhalifu wa kimataifa. Matendo haya yanaonesha haja ya haraka ya kuzuia kuongezeka zaidi kwa mzozo na kuwalinda raia pamoja na mifumo ya uokoaji wanayoiamini.”
“Nchi zina wajibu si tu kuheshimu bali kuhakikisha kuwa Mikataba ya Geneva inaheshimiwa,” anasema Rishmawi. “Hii inamaanisha kuwa nchi hazipaswi kufadhili vita wala kutoa silaha, kwani jambo hilo linaweza kuwahamasisha na kuwasaidia wapiganaji kuendeleza ukiukaji. Ujumbe wetu wa Utafiti wa Ukweli tayari uligundua mwaka jana kuwa kuna sababu za kuamini kuwa pande zote mbili zimehusika katika uhalifu wa kivita, na kwa upande wa RSF, pia uhalifu dhidi ya binadamu.”
Njaa kali
Inakadiriwa kuwa watu milioni 24.6 nchini Sudan – zaidi ya nusu ya idadi ya watu nchini humo – wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku karibu milioni nane wakikabiliwa na njaa kali. Hali ya njaa katika kambi ya Zamzam ilithibitishwa mwezi Agosti 2024 na imeenea hadi kambi za Abu Shouk, Al Salam na milima ya Nuba Magharibi. Zaidi ya raia milioni 12 wamehamishwa, ikiwemo zaidi ya milioni 8.5 waliohamishwa ndani ya nchi na zaidi ya milioni 3.5 waliokimbilia nje ya nchi. Idadi hizi zinaongezeka kila siku.
“Ushuhuda tuliopokea karibuni kuhusu uhaba wa chakula na njaa unaonesha kuwa hali hizi huenda zimesababishwa kwa makusudi,” anasema Joy Ngozi Ezeilo, mjumbe wa Tume hiyo na kuongeza kwamba, “athari za mzozo kwa Wasudan wote, hasa wanawake na watoto, ni mbaya na ya muda mrefu. Wengi wamepoteza wapendwa wao na wamesalia na majeraha ya kiakili kutokana na ukatili waliopitia bila msaada wanaouhitaji kwa dharura. Hii inasisitiza tena umuhimu wa kuwalinda raia, wakiwemo wahudumu wa kibinadamu na watetezi wa haki za binadamu, misaada ya kibinadamu, uwajibikaji kwa uhalifu huu wa kikatili, na kushughulikia athari kubwa za mzozo kwa raia wa Sudan kupitia haki na fidia, ikiwemo msaada wa kijamii na kisaikolojia.”