Shambulio la kombora laua watu Ukraine, Katibu Mkuu UN ashutumu
Shambulio la kombora laua watu Ukraine, Katibu Mkuu UN ashutumu
Amani na Usalama
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameonesha mshtuko mkubwa na huzuni kufuatia shambulio la kombora lililotekelezwa na majeshi ya Urusi katika jiji la Sumy, Ukraine, leo Jumapili, tarehe 13 Aprili. Shambulio hilo, lililotokea katika Siku ya Matawi na mwanzoni mwa Wiki Takatifu, limeripotiwa kuua watu wasiopungua 34, wakiwemo watoto wawili, na kuwajeruhi karibu watu 100 wengine.
Katika taarifa iliyotolewa jioni Jumapili saa za NewYork, Marekani na msemaji wake, Stéphane Dujarric, Katibu Mkuu amelaani vikali shambulio hilo, akilitaja kuwa ni sehemu ya “mfululizo wa mashambulio ya kusikitisha” ya karibuni yanayolenga maeneo ya raia nchini Ukraine. Mashambulizi haya yameendelea kusababisha vifo vya raia na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya kiraia.
“Katibu Mkuu anakazia kuwa mashambulio dhidi ya raia na mali za kiraia ni marufuku chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu,” taarifa hiyo imesema. “Mashambulio ya aina hii, popote yanapotokea, yanapaswa kusitishwa mara moja.”
Katibu Mkuu amerejea wito wake wa kudumu wa kutaka usitishaji mapigano wa kweli, na amethibitisha tena msaada wa Umoja wa Mataifa kwa juhudi za dhati zinazolenga amani ya haki, ya kudumu, na ya kina. Amesisitiza kuwa suluhisho lolote lazima liheshimu kwa ukamilifu uhuru, mamlaka kamili, na ukamilifu wa eneo la Ukraine, kwa mujibu wa Katiba ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa, na maazimio husika ya Umoja wa Mataifa.
Shambulio la Sumy limezua ghadhabu kimataifa, na kuongeza shinikizo la kimataifa kwa wahusika wawajibike na kwa mzozo huu kumalizika, wakati vita nchini Ukraine vinaingia mwaka wa tatu.