UNHCR: Watu milioni 1.4 wa Syria warejea nyumbani baada ya kuanguka kwa utawala wa Assad
UNHCR: Watu milioni 1.4 wa Syria warejea nyumbani baada ya kuanguka kwa utawala wa Assad
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR leo limeonya kwamba ukosefu wa ufadhili unaweza kuhatarisha maendeleo yaliyopatikana ikiwemo kurejea nyumbani kwa mamilioni ya watu.
Katika taarifa yake iliyotolewa mjini Geneva Uswisi shirika hilo limesema katika miezi tangu kuanguka kwa utawala wa Assad Desemba 8, 2024, zaidi ya watu milioni 1.4 wa Syria wamerejea katika makaazi yao, hatua inayobadilisha kwa kiasi kikubwa hali ya kibinadamu nchini humo.
Kwa mujibu wa Shirika hilo takribani watu 400,000 wamerejea kutoka nchi jirani, huku wngine zaidi ya milioni 1 waliokuwa wakimbizi wa ndani wakirudi makwao.
Limesema kurudi huku kwa idadi kubwa ya watu kunakuja baada ya zaidi ya muongo mmoja wa mzozo na na watu kufurushwa na kunaashiria hatua muhimu katika kurejesha hali ya kawaida nchini Syria.
Majira ya joto ni fursa muhimu kwa wanaorejea
UNHCR inasema kuwa majira ya joto ya 2025 ni kipindi muhimu kwa urejeo wa hiari wa wakimbizi.
“Hii ni fursa ambayo Wasyria wameisubiri kwa miaka mingi,” amesema msemaji wa UNHCR akiongeza kuwa “Lakini kurejea lazima kuwe kwa usalama, heshima na kudumu na hilo linahitaji makazi, ajira, na msaada wa kisheria.”
UNHCR imezindua mpango wa kusaidia wakimbizi milioni 1.5 na wakimbizi wa ndani milioni 2 kurejea nyumbani mwaka 2025, kwa gharama ya dola milioni 575. Hadi sasa, shirika hilo limesema ni dola milioni 71 pekee zilizotolewa, hali inayotishia uwezo wa shirika hilo kutoa msaada muhimu.
Ukata wa ufadhili watishia utulivu na usalama
Kupungua kwa kiasi kikubwa kwa misaada ya wafadhili kati ya 2024 na 2025 tayari kunaathiri shughuli za UNHCR.
Shirika hilo linaripoti kuwa idadi ya wafanyakazi wake nchini Syria itapungua kwa asilimia 30, jambo litakaloathiri utoaji wa huduma muhimu.
“Bila msaada wa kutosha, urejeaji wa watu milioni 1.5 unaweza usitekelezwe,” limeonya shirika hilo. Likiongeza kuwa “Na wale wanaorejea wanaweza kulazimika kuondoka tena.”
Kwa mujibu wa UNHCR “Takribani watu milioni 16.7 sawa na asilimia 90 ya wakaazi wa Syria bado wanahitaji msaada wa kibinadamu, huku zaidi ya watu milioni 7.4 wakiwa bado hawana makazi ya kudumu ndani ya nchi.”
Vituo vya jamii kukumbwa na hatari ya kufungwa
Miongoni mwa huduma zilizo hatarini ni vituo 122 vya jamii vinavyoungwa mkono na UNHCR, ambapo karibu asilimia 44 vitafungwa kufikia majira ya joto iwapo hakutakuwa na ufadhili zaidi.
Vituo hivi vinatoa msaada wa afya ya akili, msaada wa kisheria, kinga dhidi ya ukatili wa kijinsia, na elimu juu ya usalama dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini. “Vituo hivi ni mkombozi kwa wanaorejea,” limesema shirika la UNHCR. Pia limeongeza kwamba “Kufungwa kwake kutaathiri sio tu wanaorejea bali pia jamii zinazowapokea na mashirika ya ndani tunayoshirikiana nayo.”
Tumaini kupitia ubunifu na mshikamano wa kimataifa
Kwa lengo la kuwasaidia wanaorejea, UNHCR imezindua jukwaa la kidijitali linaloitwa “Syria ni nyumbani”, ambalo linatoa taarifa sahihi na mpya kuhusu mchakato wa kurejea kuanzia stakabadhi za kisheria hadi makazi, huduma za afya na elimu.
UNHCR imesisitiza kuwa “Taarifa ni nguvu. Jukwaa hili linawasaidia Wasyria kufanya maamuzi sahihi kuhusu mustakbali wao.”
UNHCR sasa inaomba mshikamano wa kimataifa, ikiwaalika wafadhili wa zamani na wapya kusaidia kurejesha matumaini nchini humo.
“Hatuwezi kuacha fursa hii ipotee,” limesema. “Kurudi nyumbani lazima kuwe chaguo la matumaini si la kukata tamaa.”