UN yaomba msaada kulinda fursa za kudumisha utulivu Syria baada ya miaka 14 ya vita
UN yaomba msaada kulinda fursa za kudumisha utulivu Syria baada ya miaka 14 ya vita
"Syria iko njia panda, na inastahili fursa ya kuendelea kufanikisha mchakato jumuishi wa kisiasa” amesema afisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akisisitiza tena onyo kwamba hatua za hivi karibuni za Israel ndani ya Syria zinahujumu juhudi za kujenga Syria mpya yenye amani na yenye uhusiano mwema na majirani zake, na kuiletea hali ya kuyumba katika wakati huu nyeti.
Katika taarifa yake kwa Baraza la Usalama, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Mashariki ya Kati na Asia na Pasifiki, Khaled Khiari, amezungumzia tangu kuanguka kwa serikali ya Bashar al-Assad tarehe 8 Desemba 2024 kuhusu ukiukaji wa Israel wa makubaliano ya kutenganisha majeshi yaliyowekwa mwaka 1974 kati ya Israel na Syria.
"Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekuwa wazi katika kulaani vitendo vyote vinavyokwenda kinyume na makubaliano hayo."
Khiari amebainisha kuwa mashambulizi ya anga ya Israel yanayokadiriwa kufikia mamia yameripotiwa kote nchini Syria tangu tarehe hiyo kusini magharibi, pwani ya Syria, kaskazini mashariki mwa Syria, Damascus, Hama na Homs na kwamba maafisa wa Israel pia wamezungumzia nia ya Israel ya kubaki ndani ya Syria kwa muda usiojulikana.
"Matukio kama haya yanayofanyika ndani ya Syria hayawezi kupuuzwa kwa urahisi. Tayari yanatishia mchakato dhaifu wa mpito wa kisiasa wa Syria."
Amesisitiza kuwa dhamira ya Baraza la Usalama ya kulinda mamlaka ya Syria na himaya ya ardhi yake inazidi kuwa ya muhimu, akiongeza kuwa “Fursa ya Syria kupata utulivu baada ya miaka 14 ya mzozo inapaswa kuungwa mkono na kulindwa, kwa ajili ya Wasyria na Waisraeli. Hii ndiyo njia pekee ya kufanikisha amani na usalama wa kikanda.”
Ameongeza kuwa hatua za muda mfupi za kiusalama na mafanikio ya kijeshi yasije yakadhoofisha matarajio ya makubaliano ya amani kati ya majirani hao wawili na uthabiti wa muda mrefu katika mipaka yao inayotambulika kimataifa.
Hali ya wasiwasi imetanda
“Hali katika eneo la operesheni za Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Uangalizi wa Kutenganisha Majeshi (UNDOF) bado ni tete, na inaendelea kuonyesha ukiukaji mkubwa wa makubaliano ya kutenganisha majeshi ya mwaka 1974, hasa kwa kuingia kwa jeshi la Israel katika eneo tenganishi tangu tarehe 8 Desemba,” amesema Jean-Pierre Lacroix, Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa.
Amebainisha kuwa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linashikilia vituo 12 katika upande unaojulikana kama “Bravo” au “B” mstari unaotenganisha eneo tenganishi na ardhi ya Syria, na kuongeza kuwa IDF inaendelea kujenga vizuizi ili kuzuia harakati kando ya mstari wa kusitisha mapigano.
Ameongeza kuwa IDF “inaendelea kuweka vikwazo kadhaa juu ya harakati za wafanyakazi wa UNDOF na Kikundi cha Waangalizi cha milima ya Golan katika ene tenganishi. Pia inaendelea kuweka vikwazo kwa harakati za wakazi wa maeneo ya karibu.”
Ameendelea kusema kuwa “Wakazi wa baadhi ya maeneo walifanya maandamano kupinga usumbufu unaosababishwa na shughuli za jeshi la Israel, ikiwemo kilimo, kukamatwa kwa raia, na kunyakuliwa kwa idadi kubwa ya mifugo. Baadhi ya wakazi pia waliiomba UNDOF itake jeshi la Israel kuondoka kwenye vijiji vyao.”
Jukumu la msingi kwa utulivu wa eneo hilo
Kwa mujibu wa Lacroix, UNDOF inaendelea kuratibu na pande zote mbili, ikijadili masuala mahususi yanayoathiri shughuli zake, pamoja na malalamiko yaliyowasilishwa kwake na wakazi wa eneo tenganishi.
Amebainisha kuwa katika mawasiliano na uongozi wa UNDOF, maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la Israel IDF, walithibitisha kuwa uwepo wao katika eneo tenganishi "ni wa lazima ili kulilinda dhidi ya kile wanachokiita vikundi vya kigaidi'" na wamefahamisha kuwa Israel haina nia ya kumiliki maeneo ya Syria.
Amefafanua zaidi kuwa UNDOF inaendelea kuimarisha utaratibu wake wa uratibu kupitia mipango mipya ya mawasiliano na mamlaka za Syria, "ikiwemo kuimarisha taratibu za kubadilishana taarifa na kufanya mikutano ya mashauriano kwa kawaida."
Lacroix amesisitiza kuwa ni muhimu kwa pande zote kutekeleza majukumu yao chini ya makubaliano ya kuondoa majeshi ya mwaka 1974, na kuongeza kuwa "matendo yote yanayokiuka makubaliano hayo hayakubaliki."
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza hitaji la kikosi cha UNDOF kuwa na uhuru wa kutembea katika eneo lake la operesheni, akisisitiza kuwa jukumu hilo "linabaki kuwa la msingi kwa utulivu wa Golan na eneo zima kwa ujumla."