Watoto Gaza wanasukumana na mikokoteni badala ya kwenda shuleni - UNRWA
Watoto Gaza wanasukumana na mikokoteni badala ya kwenda shuleni - UNRWA
Mwaka mmoja na nusu wa mapigano kati ya jeshi la Israeli na wanamgambo wa Hamas huko Gaza, kwenye eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli, imesababisha watoto kuacha kuhangaika na vikaragosi au kalamu za kuandikia na badala yake kuhangaika kutafuta maji.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA limesema hayo kupitia chapisho kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X, zamani Twitter.
Ni harakati za kusaka maji na si elimu
Chapisho hilo likiambatanana picha, linaonesha watoto wakisukuma mkokoteni uliobeba vifaa vya kutekea maji yakiwemo mapipa, mabeseni na hata makasiki.
“Watoto hawaendi shuleni, bali wanasukuma mikokoteni kusaidia kuteka kile ambacho kitaondoa kiu yao,” limesema chapisho hilo.
Ni zaidi ya wiki sita sasa, Isareli imeweka kizuizi cha kuingizwa kwa shehena za misaada au biashara huko Gaza.
Maji safi na salama, vyakula, malazi na huduma za matibabu vimekuwa nadra, “na madhara yake kwa watoto ni makubwa,” imesema UNRWA ikipigia chepuo kurejeshwa kwa sitisho la mapigano ambalo halijatiwa tena saini tangu kumalizika kwa lile la awali la mwezi Januari mwaka huu lililokoma tarehe 18 mwezi Machi baada ya Israeli kuanza tena mashambulizi.
Huduma ya kukusanya taka yaendelea licha ya vikwazo
UNRWA kupitia chapisho lingine X linasema licha ya uhaba wa nishati ya mafuta pamoja na vizingiti vya usafiri huko Gaza, timu ya shirika hilo ya huduma za usafi na kujisafi imeendelea kukusanya taka na kusafirisha.
Katika wiki za karibuni, takribani tani 1,200 za taka zimekusanywa. “Huduma hii muhimu inachangia katika kutunza mazingira ya usafiri na usalama wa jamii zilizoko katika mazingira magumu,” imesema UNRWA.
Jumanne ya Aprili 2025, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa Gaza imegeuka uwanja wa mauaji na kwamba “zaidi ya mwezi mzima umepita bila hata tone moja la msaada kufika Gaza.”